30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU AIBUA HOJA, MASWALI MAPYA

Na Mwandishi Wetu

HATUA ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kulinyooshea Bunge kidole kutokana na kukaa kimya kuhusu fedha za matibabu anazotakiwa kupewa kwa mujibu wa sheria pamoja  na kuelekeza lawama kwa uongozi wa  juu wa chombo hicho, ni kama amezua maswali mengine mapya.

Lissu ambaye anauguza majeraha katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kwa takribani miezi mitatu baada ya kupigwa risasi na watu ambao hadi sasa vyombo vya dola vimeshindwa kuwabaini, mbali na kulituhumu Bunge kwa kutompatia fedha za matibabu alimtaja moja kwa moja kwa jina Spika wake, Job Ndugai,  kama mtu ambaye ameshindwa kulisimamia jambo lake sawa sawa.

Katika mahojiano aliyoyafanya kwa nyakati tofauti na chombo cha habari kimoja hapa nchini na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, mara tu baada ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kufika kumjulia hali, Lissu pamoja na kueleza maendeleo yake kiafya, alimshutumu Ndugai kutofika kumwona wala kutuma mtu yeyote.

MTANZANIA Jumamosi jana liliwasiliana na Spika Ndugai kuhusu madai hayo ya Lissu, lakini katika hali ya kushangaza alikaa kimya.

Mwandishi wa habari hii awali alimpigia simu Ndugai na baada ya kutopokea kwa muda mrefu alimtumia ujumbe mfupi  wa maandishi ambao mbali na kujitambulisha alimtaka apokee simu ndipo alipojibu kwamba yupo Afrika Kusini na endapo ana maswali yoyote amtumie kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani.

Miongoni mwa maswali ambayo alitumiwa Ndugai yanasomeka kama ifuatavyo:- Tundu Lissu anakutuhumu kutokwenda kumuona na wala kumtuma mtu yeyote, unaweza pengine kulifafanua hilo?

Pili, hili la matibabu kulipiwa na Bunge pamoja na kulipwa posho kama mgonjwa hili nalo limekaaje?

Baada ya kutumiwa maswali hayo, simu ya Ndugai haikupatikana tena na hata ilipopatikana baadaye alipopigiwa hakupokea.

Lissu alikaririwa na BBC akisema kuwa  yeye kama kiongozi mkubwa ndani ya Bunge, hakuna kiongozi yeyote wa mhimili huo aliyefika kumwona na wala hajapewa fedha yoyote licha ya kustahili kwa mujibu wa sheria.

“Kikubwa zaidi mimi ni mgonjwa wa Bunge, ni kiongozi wa Bunge ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ni Msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, ni mtu mkubwa ndani ya Bunge mpaka leo  Spika hajaja, hajatuma mtu yeyote,” alisema Lissu.

Mwandishi wa BBC alipomweleza kwamba huenda hao ambao hawajafika kumwona wanasubiri aanze kujisikia nafuu, Lissu alisema:

“Wanasubiri nife ndio waje kwenye mazishi, mpaka sasa hivi Bunge halijaonyesha ‘role’ yake kwa namna yoyote ile kwa sababu mimi ni mbunge natakiwa nitibiwe na Bunge, hawajatoa hata senti kumi hadi sasa hivi kwa sababu mimi ni mbunge nina haki ya kupewa posho ya wanaokwenda nje kutibiwa sijapewa hata senti tano hata kuulizwa,” alisema Lissu.

Jana gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) likimkariri Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai, akisema amemwandikia barua kaka yake Lissu  Novemba 27, mwaka huu akimtaka aeleze stahiki ambazo mdogo wake anastahili kupewa na mhimili huo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi jana, kaka yake Lissu, Alute Mughwai, alisema amezungumza na Katibu huyo wa Bunge amemhakikishia amemtumia barua hiyo ingawa alikuwa bado hajaipata hadi kufikia jana.

Alute alisema ingawa barua ambayo aliituma yeye kwenda kwa Bunge kupitia Kampuni ya DHL ilichukua siku moja, hivyo kama Bunge limetuma kweli barua hiyo ana imani itamfikia na yeye ataifanyia kazi.

Hii si mara ya kwanza kwa suala la  fedha za matibabu ya Lissu kuzua maswali, kwani itakumbukwa mara tu baada ya kiongozi huyo kukumbwa na mkasa huo, Bunge lilieleza wazi kuwa endapo atahitaji kulipiwa gharama itabidi afuate taratibu zao ambazo ni kupelekwa Muhimbili na kisha nchini India.

Jambo hilo lilizua maneno hasa baada ya uongozi wa juu wa Chadema kutotaka kumpeleka Lissu Muhimbili kutokana na hali yake ilivyokuwa mbaya na hivyo kumpeleka moja kwa moja katika Hospitali ya Nairobi, nchini Kenya.

Hata katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari alipozungumzia maendeleo ya matibabu ya Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alilishutumu Bunge na Serikali kwa ujumla kutaka kudhulumu haki ya Mbunge huyo  ya kutopatiwa fedha za matibabu kama ilivyo kwa wabunge wengine ikiwamo wale ambao hawafuati utaratibu huo ilioutaja Bunge.

Ni wakati huo ndio ambao Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipojitokeza na kusema kuwa Serikali ipo tayari kumgharamia matibabu Lissu endapo itaombwa kufanya hivyo.

Tangu Mwalimu atamke hayo, kumekuwa na ukimya mkubwa kuhusu suala hilo hadi sasa Lissu mwenyewe alipoliibua na kuahidi kulisimamia kwa sababu ni haki yake.

MTANZANIA Jumamosi jana lilimtafuta Mwalimu bila mafanikio kujua suala hilo lilikofikia hasa ikizingatiwa kuwa familia  ya Lissu ilikwishawahi kusema imepeleka maombi hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles