Na SHOMARI BINDA,
TUNDU Lissu, wakili anayemtetea Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya katika kesi ya kupinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana juzi alikuwa kivutio mjini hapa katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza.
Watu wengi waliofurika mahakamani walikuwa na shauku ya kumwona Lissu hasa kwa jinsi alivyokuwa akimhoji aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Lucy Msoffe, ambaye ni shahidi upande wa mshitakiwa (mjibu maombi).
Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Lissu: Shahidi, mueleze Mheshimiwa Jaji siku ya tarehe 24 Oktoba 2015, siku moja kabla ya uchaguzi ulilala saa ngapi?
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, siku hiyo nililala kati ya saa 8 au saa 9 hivi usiku. Nilifanya hivyo   kuhakikisha siku ya Oktoba 25   upigaji kura unakwenda vizuri bila tatizo lolote kutokea.
Lissu: Shahidi, mueleze mheshimiwa Jaji siku ya Uchaguzi Mkuu, 25 Oktoba2015 ulianza kupokea masanduku ya kupigia kura kutoka kwenye vituo saa ngapi hadi saa ngapi?
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, siku hiyo nilianza kupokea masanduku ya kupigia kura saa 11 jioni hadi usiku wa manane saa 7 hadi saa 8.
Lissu: Mueleze mheshimiwa Jaji siku ya Oktoba 25, 2015 ulilala saa ngapi?
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, siku hiyo sikulala kabisa.
 Lissu: Mueleze Jaji siku ya kuhesabu kura kama ulilala hata kidogo tu.
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, siku hiyo sikulala kabisa hata kidogo tu.
Lissu: Shahidi, kuanzia tarehe 24 hadi 26 Oktoba 2015 ulilala saa mbili tu, ni kweli au si kweli?
Msimamizi: Kweli na nilikuwa nimechoka sana.
Lissu: Mueleze mheshimiwa Jaji kama wewe ni Mungu usiyekosea.
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, mimi siyo Mungu nisiyekosea.
Lissu: Kama usingesahihisha idadi ya watu watu waliojiandikisha, zingebadilisha matokeo ya kura alizopata mgombea wa CCM Wassira?
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji zisingebadili matokeo ya kura alizopata mgombea wa CCM.
Lissu: Je, kama usingesahihisha hizo tarakimu zingebadili kura alizopata mgombea wa Chadema, TLP, DP na ACT?
Je, zingebadili idadi halali ya waliopiga kura Jimbo la Bunda Mjini? Ingebadili kura halali? Ingebadili kura zilizokataliwa?
Msimamizi: Zisingebadili kabisa.
Lissu: Mueleze mheshimiwa Jaji kama usingesahihisha zingeleta athari kwenye matokeo.
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji zisingeleta athari yoyote ile. Na zisingebadili kura alizopata Wassira wala Esther Amos Bulaya. Hazikuathiri kwa namna yoyote kwa wagombea wengine walioshiriki uchaguzi wa ubunge Jimbo la Bunda Mjini. Idadi halali ya vituo vya kupigia kura vilivyoidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi vilikuwa 190.
Lissu: Mueleze Jaji kama uliwahi kupeleka orodha nyingine ya vituo vya kupigia kura tofauti na hiyo ya 190.
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, sikuwahi kupeleka orodha nyingine ya vituo vya kupigia kura, tofauti na hii ya 190 ioiyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Lissu: Shahidi namba moja ambaye pia ni mlalamikaji namba nne wa kesi hii, Ascetic Malagila, aliiambia Mahakama kwamba ulimpelekea orodha nyingine ya vituo 199 vya kupigia kura, Jimbo la Bunda Mjini ni kweli au si kweli?
Msimamizi: Mheshimiwa Jaji, siyo kweli. Na vyama vyote vya siasa nilivyovipelekea orodha ya vituo 190 vya kupigia kura, vilileta mawakala wao 190.
Akijibu swali la wakili anayewatetea waleta maombi kwenye kesi hiyo, Costantine Mutalemwa, aliyeuliza kwa nini alikuwa akifuta tarakimu hizo na hakuzifuta kwenye kiapo chake,Msoffe alijibu kwa kusema angepata muda angeweza pia kubadilisha kwenye kiapo chake.
Awali Msoffe alisema Bulaya alishinda kwa halali na alimtangaza mshindi.
Alisema katika fomu namba 24B ya kutangaza matokeo aliyoisoma  baada ya   kuhesabu kura kukamilika, Bulaya,aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alipata kura 28,568 na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, alipata kura 19,126.