26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

LISSU ALINYOSHEA KIDOLE BUNGE, POLISI

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAKATI Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akitimiza miezi mitatu katika Hospitali ya Nairobi, Kenya anakouguza majeraha ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana, jana alituma waraka mzito kwa Jeshi la Polisi na Bunge.

Katika waraka huo, Lissu alieleza mshangao wake kwa Jeshi la Polisi kwa jinsi lilivyo kimya pasipo kueleza mwenendo wa uchunguzi lililoeleza kuufanya dhidi ya watu waliomshambuliwa.

Katika waraka huo alioutoa jana kwa umma, Lissu pia alililaumu Jeshi la Polisi kwa kutotaja majina ya waliohusika na shambulio dhidi yake huku akilifananisha shambulio hilo na ugaidi.

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, mwaka huu nje ya nyumba yake iliyoko Area D, mjini Dodoma wakati akirejea kutoka bungeni.

WARAKA WA LISSU

“Ndugu zangu Watanzania. Salaam za upendo na shukrani kwenu wote.

“Leo ni mwezi wa tatu tangu kufanyika kwa jaribio la kuniua la Septemba 7.

“Tangu siku hiyo nimetembelewa na mamia ya Watanzania na watu wengine kutoka nchi mbalimbali duniani.

“Nimeombewa sala na mamilioni ya Watanzania na watu wengine wengi kutoka nchi nyingine walioguswa na tukio hili.

“Nimetembelewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi na viongozi wengine wa Serikali ya Kenya na taasisi zake pamoja na wabunge wa Tanzania na wa Kenya, majaji na wanasheria wa nchi mbalimbali.

“Hata hivyo, hadi sasa Jeshi la Polisi la Tanzania halijataja linamshuku nani kuhusika na kitendo hicho cha kigaidi.

“Hadi sasa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania hajamwomba Mwanasheria Mkuu mwenzake wa Kenya ruhusa ya mimi kuhojiwa na Polisi wa Kenya juu ya shambulio hilo kama inavyotakiwa na sheria husika za nchi yetu.

“Polisi wa Tanzania hawana mamlaka ya kunihoji nikiwa Kenya au kwingineko nje ya mipaka ya Tanzania.

“Hadi sasa Bunge la Tanzania na uongozi wake haujachukua hatua yoyote ya kunitembelea hospitalini nilikolazwa wala kunihudumia kwa namna yoyote ile.

“Sheria ya uendeshaji wa Bunge inasema ni wajibu wa Bunge kumhudumia mbunge kwa matibabu na huduma nyingine anapokuwa hospitalini ndani au nje ya Tanzania.

“Kwa kila namna, ninauguzwa na chama changu, Watanzania na watu wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa michango yao, sala zao na mapendo yao kwangu. Nawashukuruni sana na Mungu wetu awabariki sana,” aliandika Lissu katika waraka wake.

ATAKA UCHUNGUZI KUTOKA NJE

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, alisema tukio la kushambuliwa kwake linahitaji uchunguzi huru kutoka nje ya nchi.

“Mambo yote haya yanatilia nguvu hoja yetu juu ya ulazima wa uchunguzi huru wa shambulio hili la kigaidi. Likiachiwa kwa Serikali ya Tanzania peke yake ukweli hautakaa ujulikane.

“Ninaendelea vizuri na matibabu na madaktari watakaposhauri nitaanza hatua nyingine ya matibabu yangu. Mungu ni mwema, nitasimama na kutembea tena.

“Nitarudi nyumbani ili kuendelea na kazi ambayo imempendeza Mungu kuokoa maisha yangu ili niweze kuitenda.

“Kumekuwa na matukio mengi ya kutisha kama hili na mengine mabaya zaidi. Nchi yetu inahitaji ukombozi ili maovu haya yakomeshwe kabisa.

“Hili ni jukumu letu sote tunaojiona kuwa wazalendo halisi wa Tanzania.  “Nawashukuruni sana na Mungu wetu awabariki sana,” aliandika Lissu. 

KATIBU WA BUNGE

MTANZANIA lilipomtafuta Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai kuzungumzia hatua ya Bunge kutomtibu Lissu lakini alijibu mara moja kuwa yupo kikaoni.

Hata alipoulizwa atafutwe baada ya muda gani alisisitiza yuko kikaoni.

“Nimekwambia nipo kikaoni,” alisema Kagaigai kisha kukata simu

POLISI

Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alipoulizwa alisema ni vema Jeshi la Polisi likaachwe lifanye kazi yake kitaalamu.

“Suala la uchunguzi ni nyeti, hatuwezi kusema tunawatilia shaka watu Fulani hadi pale tutakapokamilisha uchunguzi wa kuweza kuwabaini.

“Na pindi tunapokamilisha uchunguzi tutapeleka taarifa yetu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)  ambaye ana wajibu wa kufungua mashtaka na kufikisha mahakamani.

“Ndiyo waandishi mtaruhusiwa kuandika kwamba hawa watu wamekamatwa kwa kosa Fulani, yeye (Lissu) anaweza kusema lolote, kazi ya polisi ni ya kitaaluma haiwezi kuingiliwa na mtu yoyote na kazi ya uchunguzi tuachiwe (Polisi),” alisema Mwakalukwa

Akizungumzia waraka wa Lissu, alisema hauhusiani na uchunguzi wa polisi isipokuwa kama kuna ushahidi upelekwe kwa mpelelezi wa kesi hiyo ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto.

Desemba 5, mwaka huu Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alimtembelea Lissu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Mwinyi anakuwa Rais mstaafu wa kwanza kwenda kumwona Lissu hospitalini tangu alipolazwa.

Kabla ya Mwinyi, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alimtembelea Lissu hospitalini hapo Novemba 28, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles