TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) Tanzania, Michael Dunford, amesema asilimia 35 ya watoto walio chini ya miaka mitano wamedumaa kutokana na kukosa lishe bora hali inayochangiwa na matumizi ya nafaka pekee katika kuandaa lishe yao.
Alisema lishe duni pia inawakumba wanawake walio katika umri wa kuzaa ambao asilimia 45 huwa na upungufu wa damu jambo ambalo huhatarisha uzazi.
Dunford alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara ya binti mfalme wa Jordan, Princess Sarah Zeid.
Alisema wazazi huandaa chakula cha mtoto kwa kutumia mahindi pekee, hivyo kukosa virutubisho muhimu.
Dunford alisema viashiria vinaonesha watoto wengi wanashindwa kukua vizuri kimwili, kiakili, kushindwa kuelewa masomo darasani na kukosa nguvu za kufanya shughuli za kiuchumi wawapo wakubwa.
“Kiashiria kingine cha udumavu ni upungufu wa damu.
“Zaidi ya asilimia 50 ya wanawake na watoto wanakabiliwa na upungufu huo ambao husababisha kuugua mara kwa mara na kushindwa kuchangia katika ukuaji wa uchumi,” alisema Dunford.
Alisema kutokana na hali hiyo waliona ni muhimu kukutana na Waziri wa fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ili kupata utayari wa Serikali kuongeza bajeti katika sekta ya lishe.
“Tumekutana na wafanya maamuzi akiwamo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto (Dk. Faustine Ndugulile) ili kuona kama kuna utayari wa kisiasa katika kuondokana na hali hii,” alisema Dunford.
Alisema kuna tofauti kati ya usalama wa chakula na usalama wa lishe bora kwa jamii, hivyo kuandaa mradi wa kutoa elimu ya lishe kwa jamii, hasa mikoa ya Dodoma na Singida ambayo ndiyo imeathirika zaidi.
“Mradi huu unatekelezwa Bahi na Chamwino mkoani Dodoma na Ikungi na Singida Vijijini mkoani Singida,” alisema Dunford.
Kwa upande wake, Princess Sarah alisema amefurahishwa na utayari wa Serikali kukubali kutoa ushirikiano wa kupambana na hali hiyo.
Alisema kama balozi wa WFP na mbobezi wa lishe kwa watoto na wajawazito, atatumia majukwaa mbalimbali duniani kupata miradi itakayosaidia kuondoa utapiamlo na lishe duni.
“Mtarajie mengi, kwa kutumia majukwaa mbalimbali nitashawishi jamii ya kimataifa kuleta miradi ya kupambana na hali hii,” alisema Sarah.
Alisema alipotembelea mikoa ya Dodoma na Singida kupitia mradi wa Boresha Lishe unaotekelezwa na WFP kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), wananchi wamepokea elimu ya unyonyeshaji.
“Nimefurahishwa wananchi kupokea mradi huu, wamejifunza umuhimu wa kunyonyesha, kuandaa chakula lishe kwa watoto na jamii nzima,” alisema Sarah.
Alisema mradi huo pia umetoa elimu kuhusu matumizi salama ya vyoo, ikiwa ni pamoja na kuosha mikono baada ya kutoka ili kuepuka magonjwa ya tumbo na kuharisha.
“Nimevutiwa zaidi kuhusu utunzaji wa fedha kwa njia ya vikoba vya asili kwa ajili ya kupata lishe kwa jamii, hii itawasaidia wanawake kukabiliana na ukosefu wa chakula bora kwao na jamii nzima,” alisema Sarah.