LEONARD MANG’OHA NA ERRICK MUGISHA-DAR ES SALAAM
BARAZA Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF), limefikia uamuzi wa kujitoa katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24.
Kujitoa kwa chama hicho kunafanya idadi ya vyama vilivyosusia uchaguzi huo kufikia sita hadi sasa.
Vyama vingine ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, UPDP na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).
Akitangaza uamuzi huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba alisema sababu za kujitoa katika uchaguzi huo ni kutokana na zaidi ya asilimia 98 ya wagombea wao kuondolewa.
Profesa Lipumba alisema baraza la uongozi wa chama hicho limetafakari kwa kina na kuona hakuna umuhimu kushiriki uchaguzi baada ya hoja zao tatu walizoziwasilisha serikalini kutofanyiwa kazi.
“Kwa kuwa wagombea wetu wameshaondolewa katika ushindani na ushiriki katika uchaguzi huu kwa zaidi ya asilimia 98, ni wazi kuwa na chama kimeondolewa, hivyo hatuoni namna kwa chama zaidi ya kung’atuka kwani hatuwezi kushiriki bila kuwa na wagombea.
“Kwa vile tayari Serikali ya CCM imeshakiondoa chama chetu katika uchaguzi huu, Baraza Kuu la Uongozi limefanya uamuzi wa kung’atuka moja kwa moja kwa masilahi ya chama chetu na taifa kwa ujumla.
“Tunatoa wito kwa wale wagombea wachache walioteuliwa waandike barua za kujiondoa, Tamisemi isitumie nembo za CUF katika uchaguzi huu.
“CUF inawataka wanachama wake wote nchini kutoshiriki kwenye uchaguzi huu kwa namna yoyote ile, kwa kuwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wamewaondosha na kuwanyima fomu wagombea wetu,” alisema.
Profesa Lipumba alisema kuwa chama hicho hakiutambui uchaguzi huo na kwamba viongozi watakaochaguliwa watawahesabu kuwa si halali.
Alisema kutokana na kile alichokiita kuwa ni ubakaji wa demokrasia, uongozi wa taifa wa chama hicho utazunguka nchi nzima kujadili na wananchi kuhusu kadhia hiyo.
Profesa Lipumba alisema pamoja na uamuzi huo wa kususia uchaguzi, baraza hilo limeiagiza kamati tendaji ya chama kuchukua hatua mbili za msingi ili kuokoa taifa, ikiwamo kukutana na jumuiya ya kimataifa kueleza ubakaji wa demokrasia unaofanywa na CCM pamoja na kuandaa kongamano na viongozi wa dini kujadili hatima ya taifa.
Kutokana na kile alichokiita kuwa ni ubabaishaji wa kauli za Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema chama hicho kilichukua hatua mbalimbali kwa njia rasmi na zisizo rasmi za kumkumbusha na wasimamizi wa uchaguzi juu ya kuzingatia kanuni za mwongozo na misingi ya uchaguzi, uhuru na haki hatua ambazo hazikuzaa matunda chanya.
Profesa Lipumba alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kufanya mkutano na vyombo vya habari akiitaka serikali kupitia kwa Waziri wa Tamisemi kutangaza kurudiwa upya kuchukua na kurudisha fomu za uteuzi wa wagombea na kuongeza siku za kutekeleza hilo.
Pili ni kurejeshwa majina ya wananchi wote walioondolewa katika orodha ya wapigakura na kuruhusu wagombea wote waliochukua fomu na kudhaminiwa na vyama vya siasa wateuliwe kugombea nafasi walizoazimia kugombea ili kunusuru uchaguzi huo.
“Hata hivyo pamoja na nia njema ya mwenyekiti na uzuri wa mapendekezo yake kwa masilahi ya siyo tu ya CUF bali ya vyama vyote vya siasa na Tanzania kwa ujumla, Serikali ya CCM imeshindwa kuheshimu na kufanyia kazi mapendekezo haya,” alisema Profesa Lipumba.
WASIO NA SIFA WATATOLEWA
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Lewis Mnyambwa, amewataka wagombea wa nafasi hizo kutambua taratibu za urudishwaji wa majina kwenye vituo vyao zitazingatia kanuni saba zilizowekwa na tume.
Akizungumza na MTANZANIA jana ofisini kwake kuhusu mwenendo mzima wa uchaguzi katika manispaa hiyo, Mnyambwa alisema ofisi yake inazingatia kanuni zilizowekwa na kumtaka mgombea azifuate na si vinginevyo.
Alifafanua kuwa katika kanuni za uchaguzi za mwaka 2019 imekuwa ikizingatia vipengele saba ambavyo hivyo kama kuna mgombea amevikosea atapoteza sifa ya kuwania nafasi hiyo.
Akivitaja baadhi ya vipengele kuwa kama siyo raia wa nchi hii, hujajiandikisha katika eneo husika, kujiandikisha mara mbili, kutokudhaminiwa na chama chake, amejidhamini mwenyewe, kurejesha fomu zaidi ya mgombea mmoja kutoka kwenye chama husika na kujitoa mgombea kwa mujibu wa kanuni ya uchaguzi.
Mnyambwa alisema kuwa hakuna mtu atakayeonewa bali kanuni ndizo zinazozingatiwa, hivyo ni vema wagombea wakalitambua hilo ili baadhi yao wasijione kama wameonewa na kuwa vitabu vya miongozo jinsi ya ujazaji fomu vilitolewa kwa kila chama kwa lengo wavisome kabla ya kuzijaza fomu hizo.
Aidha alisema Manispaa ya Songea ina mitaa 95 na 33 wagombea wa CCM wamepita bila kupingwa, huku mitaa ambayo kama wagombea wake watakidhi vigezo itakuwa imebaki 62 ambayo na vyama vya upinzani wagombea wake walichukua fomu.
“Inanishangaza sana baadhi ya viongozi wa vyama kulalamikia mchakato wa uchaguzi wakati hata vyama vyao havijasimamisha wagombea jambo ambalo linachafua ofisi ya usimamizi wa uchaguzi bila sababu za msingi,” alisema Mnyambwa.