Elizabeth Joachim, Dar es salaam
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema chama hicho hakitawavumilia wanaopora mali za chama hicho na kuzihamishia Chama cha ACT Wazalendo.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Jumanne Machi 19, Jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba amesema hatua hiyo ni utapeli na wizi wa wazi, hivyo chama chake kitafuata utaratibu wa kisheria kuzirejesha.
“Hili ni jambo la kisheria, mali za chama zitaendelea kuwa za chama, hao wanaobadili rangi majengo ya chama ninawaambia, akili za Maalim Seif wachanganye na zao, kwa sababu jinai itawahusu wao binafsi na huyu maalim hatakuwa nao,” amesema Profesa Lipumba.
Aidha, Profesa Lipumba amesema kuna watu wenye fikra nzuri ambao walikuwa wanaungana na Maalim Seif lakini hawawezi kubadilisha maamuzi yao na kumfuata ACT.
“Nataka kuwambia wale wote ambao mlikuwa sambamba na Maalim Seif wenyeviti, madiwani, wabunge na wanachama wa CUF tujumuike na tuwe pamoja katika kukijenga chama chetu,” amesema.