Na GABRIEL MUSHI
UMBALI mrefu na tatizo la usafiri ni mojawapo ya mambo yanayoelezwa kuchangia kuendeleza ukatili wa kingono kwa wanawake na wanafunzi nchini.
Hali hiyo inatajwa kuwa mbinu rahisi kwa madereva wa bodaboda na magari wakiwamo utingo kuitumika kama mtego wa kuwanasa watoto wa shule za msingi na sekondari ambao husafiri umbali mrefu kuisaka elimu.
Kwa mujibu wa matokeo ya tafiti zilizotolewa Agosti mwaka huu, na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, kumekuwa na matukio ya ukatili wa kingono 2,059 yaliyoripotiwa kwenye vituo vya polisi, ukilinganisha na kipindi cha miezi 6 cha mwaka 2016, ambapo kulikuwa na matukio 2,859.
Kutokana na hali hiyo, kelele zimeendelea kupazwa katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini ambayo yameanza Novemba 25 hadi Desemba 10 mwaka huu.
Taasisi mbalimbali zinazoshughulika na utetezi wa wanawake, zimeendelea kutumia fursa hiyo ikiwamo Jukwaa la Utu kwa Mtoto (CDF) kupitia mradi wa ‘Tuwezeshe Akina Dada’ kueleza yanayowasibu wanawake.
CDF hivi karibuni waliandaa mdahalo uliotoa wasaa kwa watoto wa kike na wanawake kufunguka kuhusu dhahama wanazozipata ndani ya jamii.
Mbali na kudadavua mambo mbalimbali yanayochangia muendelezo wa ukatili wa kingono nchini, wanasema suala la umbali mrefu kuelekea katika shule mbalimbali nchini limechangia kuendelea kuwapo kwa ushawishi wa kushiriki ngono kwa baadhi ya wasichana na mwishowe kupata mimba.
Pia ukosefu wa miundombinu ya kutosha kama vile hosteli na magari ya kuwabeba wanafunzi, imechangia ongezeko la vitendo hivyo kwa kuwa madereva wa bodaboda na utingo wa daladala ‘makondakta’ nao hujinyakulia nafasi hiyo kuwarubuni wasichana kwa kuwapa huduma ya usafiri bure ‘lifti.’
Mmoja wa wazungumzaji katika madahalo huo, Eva Chuwa anasema mazingira nayo yamechangia walimu wa kiume kuwa na matamanio kwa wanafunzi wa kike.
“Pia malezi ya watoto wa kike yana changamoto kwa sababu wana tamaa, wanatamani kupata vitu vizuri kwa kupitia njia ambazo si salama ndio maana huishia kudanganywa na madereva bodaboda kwa kuwapa lifti matokeo yake hukatiza ndoto zao.
Madhara ya ukatili wa kingono
Euphonia Edwar ambaye ni mhitimu wa shahada ya Sayansi ya Kilimo na Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) anasema pamoja na wanafunzi wengi kukatishwa masomo kutokana na mimba za utotoni, pia hukosa nafasi ya kuendelea na masomo.
“Kama tunavyofahamu, sheria za nchi yetu zimekataza mwanafunzi kuendelea na masomo baada ya kugundulika kuwa amepata ujauzito, hivyo ndoto za mtoto wa kike huyeyuka labda apate nafasi nyingine katika elimu ya ufundi.
“Lakini pia wasichana wengi huathirika kisaikolojia pindi wanapokumbwa na matatizo hayo ya kingono. Ila tusisahu pia hali ya usumbufu wa kumtaka kingono mtoto wa kike nayo huwaharibia umakini darasani.
Nini kifanyike kuzuia ukatili wa kingono?
Elizabeth Benedickt ambaye ni mmoja wa wanafunzi wa mafunzo ya sheria kwa vitendo kutoka Shule Kuu ya Sheria nchini, anasema kutokana na kasi ya serikali kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu nchini, umefika wakati sasa wa kuongeza kasi ya ujenzi wa mabweni.
“Lakini pia kuwapo kwa ujenzi wa shule karibu na jamii kutasaidia kupunguza umbali mrefu wa kufuata elimu. Hali hii itasaidia watoto wengi kupenda elimu na hata kutopata usumbufu wakati wanaelekea au kurudi shuleni.
“Pia sheria za kuwalinda watoto wa kike zifuatiwe, kwa sababu zikifuatwa kuanzia kwa walimu na wadau wengine hali itakuwa shwari. Pia adhabu kali zitolewe kwa walimu wanaobainika kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanafunzi,” anasema.
Aidha, Efratha Kristos ambaye ni mmoja wa wanafunzi waliohitimu elimu ya sekondari hapa jijini Dar es Salaam, anasema ni vema elimu ikatolewa hasa maeneo ya vijijini kwa sababu maeneo mengi hawajui nini kinachotakiwa kufuatwa pindi kunapotokea matukio ya ukatili wa kingono.
“Elimu ya kutosha ikitolewa hali itakuwa tofauti kama ilivyotokea mabadiliko katika jamii ambazo zimeanza kuacha kukumbatia mila na utamaduni wa kukeketa watoto wa kike.
“Pia jamii na serikali kwa ujumla iwajibike kuhakikisha kuwa wasiachana wapata fursa sawa ya kupata elimu. Kwa mfano, jamii ya makabila kama Wakurya na Wamasai wanaona si muhimu kwa watoto wa kike kupatiwa elimu.
“Nakumbuka kuna siku nikiwa kule mkoani Manyara akina mama wa jamii Kimasai walinifuata kuniomba nikazungumze na watoto wao wa kike kwa kuwa wamekataa kuendelea na masomo licha ya kuwa wapo darasa la sita. Watoto hao walitaka kuolewa. Hali hiyo inaonesha dhahiri kuwa baadhi yao hujifelisha makusudi ili wasiendelee na masomo,” anasema.
Ofisa Mradi wa Tuwezeshe Akina Dada, Nancy Minja anasema kupitia mradi huo ambao umeanza nchini Uingereza na sasa katika nchi za Afrika Mashariki wataendeleza elimu ya jinsia kwa watoto wa kike ili kuwaokomboa katika ukatili wa kingono.
“Mradi huu uliofadhiliwa na Waingereza umedhamiria kuhakikisha taasisi binafsi ikiwamo CDF tunashirikiana na serikali kama vile kuanzisha klabu mbalimbali mashuleni kutoa elimu ya kujitambua, kujua sheria na haki za mtoto wa kike ili kuzuia vitendo hivi.