24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

LHRC YATUHUMU POLISI KUVURUGA UCHAGUZI

Na JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelituhumu Jeshi la Polisi kuwa lilihusika na uvunjifu wa amani wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani wa marudio uliofanyika Novemba 26 mwaka huu.

Akitoa ripoti ya LHRC kuhusu tathmini ya ukikwaji wa haki za binadamu katika uchaguzi huo jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema kulikuwa na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu na taratibu zinazosimamia uchaguzi nchini.

Uchaguzi huo ulihusisha kata 43 zilizo katika Halmashauri 36 kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi baada ya madiwani waliokuwapo kufariki, kujiuzulu na wengine kutenguliwa.

Henga alisema wakati wa uchaguzi huo kulikuwa na vitendo vya matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, watu kutekwa, kupigwa, kukamatwa na kujeruhiwa kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi ambavyo viliwatia hofu wapiga kura.

“Vitendo hivi viliripotiwa kufanywa na vyombo vya dola, watu wasiojulikana na wafuasi wa vyama vya siasa ikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na vingine vya upinzani,” alisema Henga.

Henga alisema wakati wa uchaguzi yaliripotiwa matukio ya kutekwa na kukamatwa kwa wanachama wa Chadema aliowataja kuwa ni Eliza Nyenza na Martha Francis walipokuwa wakienda kupiga kura katika Kata ya Kitwiru, Iringa mjini.

Alisema tukio hilo linalosadikika kutelekezwa na kikosi cha ulinzi cha CCM (Green gard).

Alilitaja tukio jingine kuwa ni la kushambuliwa kwa gari la Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Daddy Igogo huku polisi wakiwa wanamshikilia Meya wa manispaa hiyo, Alex Kimbe.

“Katika Jimbo la Kawe, Mfuasi wa CCM alivamiwa na kujeruhiwa na watu wanaosadikika kuwa ni wafuasi wa Chadema na katika Kata ya Makiba, wakala wa Chadema aliyejulikana kwa jina la Rashid Jumanne na Mwenyejkiti wa chama hicho Tawi la Valeska, Nickson Mbise walijeruhiwa vibaya baada ya kushambuliwa kwa mapanga asubuhi wakielekea katika vituo vya kupiga kura.

“Pia vitendo vingine viliripotiwa kutokea kwenye Kata za Nyabubhinza, Maswa na Simiyu ambako mawakala katika vituo nane kati ya 13 walikamatwa na polisi akiwamo Diwani wa Chadema, Zakayo Chacha Wangwe. Na Wilaya ya Itilima Simiyu Katibu wa CCM alilazwa hospitalini baada ya kushambuliwa,” alisema Henga.

Kata nyingine aliyoitaja kukumbwa na matukio yaliyovuruga uchaguzi ni Kimweri wilayani Meatu na kwamba polisi walimkamata Katibu wa Chadema aliyekuwa akiratibu uchaguzi katika Kata ya Saranga mkoani  Dar es Salaam, Perfect Mwasiwelwa na Meya wa Manispaa ya Ubungo, Bonface Jacob.

“Huko Bumbuli na Tanga mawakala wa Chadema katika vituo 13 waliondolewa vituoni na kupelekwa kituo cha polisi. Hakuna sababu iliyotolewa kuhusu kukamatwa kwao na pia katika kata sita Jimbo la Arumeru Mashariki, mawakala wote walitolewa nje ya vituo.

Alionya kuwa vitendo hivyo vina viashiria vyote vya kukandamiza demokrasia na kwamba ipo hatari ya kukuza utamaduni wa kulipiziana visasi na chuki za kisiasa kitu ambacho kitasababisha uvunjifu wa amani nchini.

“Kituo kinatoa wito kwa serikali na vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaobainika kuhusika kwa namna moja au nyingine katika uvunjifu wa haki za binadamu na kuvuruga uchaguzi.

“Pia kinatahadharisha matukio hayo yasipokemewa na jamii nzima ni kiashiria kibaya na msingi mbaya utakaoathiri chaguzi zijazo ukiwamo uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020,” alisema Henga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles