Munich, Ujerumani
MSHAMBULIAJI wa timu ya Bayern Munich, Robert Lewandowski, atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nne kutokana na kuumia kwenye mchezo dhidi ya Chelsea, Jumanne wiki hii hatua ya 16 bora, hivyo anaweza kuukosa mchezo wa marudiano.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, alipata tatizo la goti kwenye mchezo huo huku timu yake ya Bayern Munich ikifanikiwa kushinda mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.
Katika mchezo huo Lewandowski alihusika kwenye mabao mawili yaliyofungwa na nyota wa zamani wa Arsenal, Serge Gnabry kabla ya yeye mwenye kupachika bao la tatu.
Lewandowski aliweza kumaliza dakika zote 90, lakini baada ya mchezo kumalizika alipatwa na maumivu ya goti na kutakiwa kuwa nje kwa kipindi hicho chote mara baada ya kufanyiwa vipimo na daktari wa timu.
Kutokana na hali hiyo, Lewandowski ataukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Chelsea huko nchini Ujerumani mchezo ambao utapigwa Machi 18.
Hata hivyo mchezaji huyo ataikosa michezo mingine ya Ligi Kuu nchini Ujerumani dhidi ya Hoffenheim, Augsburg, Union Berlin pamoja na robo fainali ya DFB-Pokal dhidi ya wapinzani wao Schalke.
Hiyo ni habari njema kwa Chelsea ambao wanahitaji kwenda kupindua matokeo, hata hivyo ni jambo ambalo linaonekana kuwa ngumu japokuwa soka ni mchezo wa makosa na chochote kinaweza kutokea.
Raundi ya kwanza hatua ya 16 bora ya Ligi hiyo ya Mabingwa ilifikia mwisho juzi huku Manchester City wakiwafuata Real Madrid nchini Hispania na kuwapa kipigo nyumbani cha mabao 2-1, wakati huo timu ya Lyon wakiwa nyumbani wakashinda bao 1-0 dhidi ya wababe wa soka nchini Italia, Juventus.
Katika mchezo wa huo wa Real Madrid, nahodha wao Sergio Ramos ambaye ni beki wa kati alioneshwa kadi nyekundu kutokana na utovu wa nidhamu, hivyo ataukosa mchezo wa marudiano dhidi ya Man City kwenye Uwanja wa Etihad.