Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
LEO ni Profesa Ibrahim Lipumba au Maalim Seif Sharif Hamad kubaki CUF.
Ndivyo unavyoweza kusema wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapotoa hukumu ya mvutano wa uongozi ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).
Hukumu ambayo inasubiriwa kwa shauku na pande zote mbili zinazovutana, inatokana na kesi namba 23/2016 iliyopo mbele ya Jaji Benhajj Masoud, ambayo itaamua iwapo Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba ni halali au laa.
Kumekuwapo na mgogoro mkubwa ambao umesabababisha kujitokeza mgawanyiko wa wanachama ambako upande mmoja unamuunga mkono Lipumba na mwingine unamuunga mkono Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu.
Taarifa zinaonyesha mpaka sasa hukumu hiyo imeahirishwa mara nnne na mara ya kwanza, ilitakiwa kusomwa Oktoba 10, 2018, iliahirishwa hadi Novemba 30, 2018, ikaahirishwa tena hadi Januari 15, 2019, ikiaahirishwa tena hadi Februari 22, 2019 na sasa imeahirishwa hadi Machi 18, 2019 ambayo ni leo.
Mmoja wa viongozi wa juu wa chama hicho, aliiambia MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana kuwa, kutokana na kujitokeza hali hiyo, wanachama wamepata wasiwasi wa kujua hatma ya uongozi ndani ya chama hicho.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, chama kinahitaji kufanya mikutano ya ndani kuteua viongozi mbalimbali watakaosimamia uchaguzi wa ndani na uchaguzi mkuu kuhakikisha wanashinda, lakini kuwapo kwa mgogoro huo kumesababisha kushindwa kufanyika mikutano.
Profesa Lipumba alijiuzulu nafasi ya uenyekiti Agosti 6, 2015 wakati chama kinaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais.
Alisema licha ya kupitia changamoto hizo, chama hicho kiliweza kufanya vizuri kwenye uchaguzi huo na kusaidia kupata wabunge wanne kutoka Zanzibar, walioingia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wabunge wa uwakilishi viti 18 kutoka Pemba na viti tisa kutoka Zanzibar.
“Mpaka sasa CUF ina madiwani zaidi ya 300 nchini na inaongoza halmashauri tano ambazo ni Newala, Tandahimba, Mtwara, Kilwa na Liwale,”alisema.
Wiki iliyopita Profesa Lipumba alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa kupata kura 516, akiwashinda wapinzani wake, Zubeir Hamis aliyepata kura 36 na Diana aliyepata kura 16.
Makamu Mwenyekiti Zanzibar, alichaguliwa Abbas Juma Mhunzi aliyepata kura 349, wakati Makamu Mwenyekiti Bara, alichaguliwa Maftah Nachuma kwa kura 231.
Juzi Baraza Kuu la Uongozi, lilimchagua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho. Baada ya kupigiwa kura Khalifa alitangazwa mshindi kwa kupata kura 37, huku mpinzani wake Masoud Said Suleiman akijipatia kura 11.