31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Hoja za Nassari zaibua mjadala

*Agoma kuulizwa maswali na waandishi wa habari

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

HATUA ya aliyekuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) kuvuliwa ubunge na namna alivyojitetea mbele ya waandishi wa habari, imeibua hoja nyingi  kwa wachambuzi, wasomi na wananchi wa kawaida.

Wachambuzi hao wametoa maoni tofauti kuhusu namna bora ya kushughulikia suala hilo, huku wakishauri Bunge kurejea uamuzi wake wa kusimamisha ubunge wa Nassari.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Nassari hakutaka kuulizwa maswali kwa kile alichokieleza amevurugwa, hivyo kabla ya kuanza kuzungumza alitahadharisha  asingepokea swali lolote.

MSEKWA

Kutokana na uamuzi huo wa Bunge na namna Nassari alivyojitetea, Spika Mstaafu, Pius Msekwa aliliambia MTANZANIA jana kuwa utetezi wa Nassari mbele ya waandishi wa habari hauna maana kwa sababu suala lake limefuata matakwa ya Katiba na taratibu za Bunge.

“Hata akijitetea mbele ya waandishi wa habari haisaidii kwa sababu hata mahakamani watu wenye hatia wanajitetea na   taratibu za Bunge  zinafahamika na inafuata matakwa ya Katiba,”alisema Msekwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. George Kahangwa alisema Bunge linaweza kurejea uamuzi wake kwa kumsikiliza Nassari.

“Nafikiri sheria na taratibu za Bunge ndizo zituongoze katika hili. Bunge linaweza kurejea uamuzi wake na wakutane na Nassari kwa sababu sisi sote ni Watanzania, hakuna jambo ambalo linashindikana katika mazungumzo,”alisema Dk. Kahangwa.

  Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco), Profesa Gaudence Mpangala alisema anatazama uamuzi wa Bunge katika sura mbili.

“Kwanza nalitazama kwa upande wa  utawala kwa sababu mkuu wa kitengo chochote kama Spika kabla ya kuchukua uamuzi lazima ajiridhishe kama kweli Nassari anastahili kuchukuliwa hatua.

“Kwa namna nilivyomsikiliza Nassari akijitetea ni wazi huyu mtu hastahili kuvuliwa ubunge kukiwa na utawala ambao ni bora.

“Pili suala hili pia ninalitazama katika siasa kwamba tangu awamu hii ya tano, wabunge wa upinzani wamekuwa wakikandamizwa.

“Mfano ni namna baadhi yao wanavyowekwa mahabusu na baadaye mahakama inakuja kueleza kuwa hawana hatia.

“Haya yote ni mambo ya  siasa, lakini katika hili sasa spika anatakiwa kuwa neutral awatreat wabunge kwa usawa kwa sababu kwa alivyoeleza Nassari hakustahili.

“Lakini kwa sababu ya jazba za  siasa basi limetokea hilo, sasa ni vema Nassari akajitetea katika hali ya  sheria mahakamani,”alisema Profesa Mpangala.

  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana alisema hatua ya Nassari kuzungumza na waandishi wa habari ni porojo tu kwa sababu anatakiwa aende mahakamani.

“Lazima tuheshimu mamlaka zilizopo na uamuzi kama huu haujawahi kutokea. Tunaamini spika wetu ni mwangalifu ana wanasheria hivyo ni wazi spika amejiridhisha.

“Hayo anayoyazungumza Nassari hayatoshelezi mahitaji ya  sheria, solution (ufumbuzi) si kuzungumza na vyombo vya habari bali anatakiwa kwenda mahakamani, zaidi ya hapo ni porojo tu,”alisema Dk. Bana.

Mwandishi wa Habari Mwandamizi, Ansbert Ngurumo aliandika katika mitandao ya  jamii akieleza kushangazwa kwa kitendo cha Nassari kukataa kuulizwa maswali.

“Nassari amekataa kuulizwa maswali. Kosa! Nadhani sasa tuweke sharti. Kama mtu hana ubavu wa kujibu maswali asiite ‘press conference’. Aandike ‘statement’ aisambaze kwenye media. Basi!

“Hii ‘precedent’ inayowekwa ni hasi kwa taasisi. Mtu unasafiri kutoka Arusha hadi Dar es Salaam kwa ajili ya ‘press conference’, halafu unagomea maswali ya waandishi wa habari? Tukemee tabia hii ndani na nje ya chama,” aliandika Ngurumo.

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob naye aliandika katika mitandao ya  jamii, akisema kitendo cha Nassari kupoteza ubunge katika mazingira hayo kina athari kwa chama na kwamba ni bora angejiunga na CCM moja kwa moja.

“Na athari yake imelenga kutengeneza propaganda ya  uchaguzi 2020 … vijana wengi watakumbana nayo kuwa branded kuwa wanataka ubunge siyo kwa ajili ya kwenda kufanya kazi bali ‘kula bata’.

“Ajenda ambayo ndiyo iliyotoa wazee bungeni na kuwapa fursa vijana, inarudishwa kwa vijana kupitia Nassari.

“Ukiamini hilo angalia tayari propaganda inayoendelea Arumeru kuitishwa vikaovya  wananchi na kurekodiwa,”aliandika Meya Jacob.

ALIYOZUNGUMZA NASSARI

Akizungumza  na waandishi wa habari, Nassari alisema anakusudia kwenda mahakamani kudai haki ya uwakilishi wa wananchi wa Arumeru baada ya Spika   Ndugai kutangaza kwamba hana sifa za kuendelea na ubunge.

Vile vile alisema Spika bado anayo nafasi ya kurejea uamuzi wake  wananchi wa Arumeru Mashariki waendelee kuwa na mwakilishi katika Bunge.

Akijitetea, Nassari alisema mara ya mwisho alihudhuria mkutano wa Bunge wa Septemba lakini hakuhudhuria mkutano wa Novemba na Januari kwa sababu alikuwa anamuuguza mke wake nje ya nchi.

“Sijaita hii press   kumshambulia yeyote lakini bado naamini hii si sahihi hata kidogo.

“Nilifanya jitihada za kuwasiliana na Spika nikamtumia email nikiwa Marekani kumjulisha hali ya mke wangu.

“Nasikitika kwa uamuzi alioufanya, nawapa pole wananchi wangu wa Arumeru, haki yao tutaitafuta kwenye vyombo vya sheria,”alisema Nassari.

Akizungumza huku akitokwa na machozi, Nassari alisema alikuwa akimwuguza mke wake kutokana na matatizo aliyokuwanayo na kwamba alijaliwa kupata mtoto wa kike Januari 27 mwaka huu, siku moja kabla ya kuanza   mkutano wa Bunge la Januari.

“Pamoja na huzuni ya kuvuliwa ubunge, bado nina furaha ya kupata mtoto, kuwa mbunge hakuondoi majukumu mengine ya  familia.

“Nakumbuka Spika Ndugai alihudhuria harusi yangu mwaka 2014, alikuwa anajua sina mtoto na nilimjulisha juu ya matatizo ya mke wangu.

“Alitakiwa kujiridhisha kwa kuniita na kunihoji badala ya uamuzi alioufanya,”alisema.

  Nassari alisema ndani wiki mbili kuanzia sasa ataeleza kinachoendelea kuhusu kusudio lake la kwenda mahakamani na kwamba atatoa nyaraka zinazoonyesha kuwa alihudhuria Bunge la Septemba mwaka jana.

Alhamisi   iliyopita, Spika   Ndugai alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage kumuarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi.

Katika taarifa yake, Spika alieleza sababu za Nassari kuvuliwa ubunge kuwa ni kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge   mfululizo.

Taarifa hiyo ilitaja mikutano hiyo kuwa ni mkutano wa 12  wa Septemba 4 hadi 14, 2018), mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, 2018 na ule wa 14 wa Januari 29 hadi Februari 9 mwaka huu.

Taarifa hiyo ilisema: “Uamuzi huo wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 71(1) (c).

“Ibara hiyo inaeleza kuwa ‘Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

“Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, kuwa, ‘kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge.

“Mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataiarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi”.

Kuvuliwa ubunge wa Nassari kunafanya Chadema kupoteza wabunge wanane tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Kati yao saba walijiuzulu uanachama wa chama hicho na baadaye kuteuliwa tena kuwania nafasi zao kupitia CCM.

Wabunge hao ni   Dk. Godwin Mollel (Siha-Chadema), Mwita Waitara (Ukonga-Chadema), Julius Kalanga (Monduli-Chadema).

Wengine ni Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF), Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF), Pauline Gekul (Babati Mjini-Chadema), James ole Millya (Simanjiro-Chadema), Chacha Marwa (Serengeti-Chadema) na Joseph Mkundi (Ukerewe-Chadema).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles