27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Lembeli: Tutasafisha Wizara ya Ardhi

lmblNa Elizabeth Mjatta
IKIWA ni takriban wiki tatu tangu Rais Jakaya Kikwete amuondoe kazi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imesema itahakikisha viongozi wanaofanya vitendo vya kifisadi katika wizara hiyo wanaondolewa.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli, wakati wa ziara ya kukagua eneo la kituo cha huduma cha mfano kilichopo Luguluni eneo la Mbezi Luisi, kitakachoendelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Alisema wizara hiyo ni moja ya wizara iliyojaa urasimu katika utendaji wake wa kazi huku akitolea mfano wa kitendo chake cha kugawa viwanja mara mbili na kutoa vibali kwenye maeneo ya wazi.
“Sasa sisi kama Kamati ya Bunge ambayo kazi yetu kubwa ni kuishauri Serikali, tutahakikisha tunaisimamia iwaondoe katika nafasi za kazi wale wote waliojikita katika kazi za kifisadi katika wizara hiyo,” alisema Lembeli.
Alisema pamoja na mambo mengi yaliyojitokeza katika umilikishwaji wa eneo hilo, wanaamini NHC ambao wamepewa dhamana hiyo watafanya kazi yao kwa ufanisi mkubwa katika kuendeleza eneo la mradi.
“Mchakato wa kuchukua eneo hili ambalo litajengwa takriban miji 259, ulitokana na mpango wa kuboresha miji wa mwaka 1979, ambapo mwaka 2011 Rais Kikwete alichukua eneo hili kutoka kwa wananchi lengo likiwa kuliendeleza, kulikuwa na changamoto nyingi lakini bahati nzuri wakazi wote walilipwa na hadi leo hii tunaona hakuna aliyerudi tena,” alisema Lembeli.
Alisema kamati inaridhishwa na utendaji wa NHC na wanaamini mradi huo utaanza mapema baada ya shirika hilo kukabidhiwa mkataba rasmi.
Akizungumzia mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya NHC, Zakhia Meghji, alisema wamekabidhiwa rasmi mkataba wa kuendeleza eneo hilo mapema Januari, mwaka huu.
“Tayari mipango ya kuanza uendelezaji imekamilika na kwa sababu tayari Serikali imeshatoa rasmi kibali naamini kazi itaanza mapema iwezekanavyo,” alisema Meghji.
Alisema eneo hilo litajengwa makazi pamoja na vitega uchumi.
“Vitajengwa vitu vingi ikiwemo hospitali, shule na uwekezaji mwingine kwa ajili ya kutoa huduma na mahitaji muhimu kwa wananchi,” alisema Meghji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles