29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

LEMA NA NASSARY  WAONGEZEWE ULINZI

Na, HUSSEIN JUMA, SHINYANGA


WALICHOKIFANYA  wabunge wawili , Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema na Mbunge wa Arumeru Kaskazini Joshua Nassary, ni kitendo ambacho si tu cha kizalendo, bali kinahatarisha maisha yao pia.

Ushahidi waliouonesha hadharani wa viongozi wa umma wakinajisi ofisi za umma kununua madiwani ni ushahidi ambao kwa namna yoyote unaibua watu mbalimbali waweze kuwafuatilia kwa kutaka aidha kulipa kisasi, kuwanyamazisha ama kuwindwa hata na watu wengine tofauti kabisa wenye chuki zao binafsi dhidi yao.

Sote pia tumeona dalili za awali zimeanza kujionesha kuwa, wabunge hawa wanawindwa. Niamini kuwa, vyombo vyetu wa ulinzi na usalama ambavyo vina dhamana ya kulinda raia na mali zao vitakuwa mstari wa mbele kabisa katika kuwalinda wabunge hawa.

Tunayo mengi sana ya kujifunza kutokana na ushahidi wa video walioutoa Watanzania hawa wawili. Biashara ya madiwani ambayo hivi karibuni imekithiri ghafla, ambapo tumesikia kila anayekihama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (chadema) au chama kingine cha kisiasa kwenda Chama Cha Mapinduzi (CCM)  anadai anahama ili ‘kumuunga mkono Rais Magufuli’ kwa kile kinachodaiwa kujali ‘wanyonge’ na kulinda ‘rasilimali’ za nchi kwa manufaa ya wananchi.

Madiwani hawa, kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, wamekuwa wakihama Chadema kwa manufaa yao binafsi kabisa tena kwa nguvu ya shinikizo la rushwa, rushwa ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa namna tofauti tofauti aidha kwa ahadi za ajira, fedha taslimu, kulipwa mishahara hewa, ulinzi na hata kuahidiwa kufutiwa mikopo waliyonayo. Yote haya yameshazungumzwa sana, lakini mimi nataka niwakumbushe Watanzania wenzangu mambo mengine ambao tunatakiwa tujifunze kutokana na ushahidi huu wa video wa  Lema na Nassary.

Hujuma ya viongozi kwenye maendeleo ya wananchi kwa sababu ya siasa. Nimesikiliza kwenye moja ya video ikimuonesha Emmanuel Mollel, mmoja kati ya madiwani saba waliohama hivi karibu kwa sababu ile ile ya kumuunga mkono Rais Mgufuli na sauti yake kusikika kuwa, shule zilizokuwa zinachomwa zilikuwa ni mbinu za kisiasa zilizofanywa na baadhi ya viongozi waliopo leo mkoani humo kwa lengo la kumshusha cheo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa wakati  huo. Video nyingine imeonesha na kusikika kuwa, kuna mitambo ya manispaa ambayo haikuwa inafanya kazi. Lakini kwa kuhama kwa diwani fulani, basi vifaa hivyo vikaahidiwa kupelekwa kufanya kazi ili kuuaminisha umma juu ya utendaji kazi wa aidha diwani huyo au viongozi wengine wa kisiasa.

Hizi ndizo hujuma ambazo wananchi wamekuwa wakicheleweshewa maendeleo kwa sababu tu ya watu wachache ambao kutokana na kucheleweshewa huko, basi wao kwa namna moja ama nyingine wananufaika. Suala hili linajibu vizuri sana swali la kwa nini baadhi ya maeneo yaliyoko chini ya upinzani yanaonekana kutokuwa na maendeleo yanayotakiwa. Jibu lake ni kwamba, maeneo haya hayana maendeleo kwa sababu kuna wapinzani. Na waleta maendeleo hawataki kupeleka maendeleo kwa sababu kuna wapinzani.

Ajira, vijana wa Kitanzania tunalia ajira. Ajira zinazotolewa zimekuwa ni chache ambazo waombaji wanakuwa wengi kuliko nafasi zilizopo. Nilipigwa na butwaa siku vijana wenzangu walivyokuwa wakigombania karatasi za ‘interview’ ya TRA. Imefikia hatua kwa sasa hadi kada ya ualimu wahitimu wanaomba ajira na bado hawapati. Niseme tu kwamba, haijalishi umesoma nini, lakini hamia CCM ndiko kuna ajira za haraka. Kwenye video inayomuonesha DC Mnyeti akijaribu kumwaminisha na kumhakikishia mmoja kati ya madiwani kuwa wao ndiyo wenye ‘influence’. DC anampa hadi mfano kwenye ajira ambazo waliwachukua hadi watu ambao hata CV hazikukamilika na wakala ajira safi maliasili. Sasa kijana mwenzangu, utaendelea kuzunguka na bahasha zako kila kona wakati wenzako wanaajiriwa ndani ya masaa kadhaa bila kujali hata CV zao; kadi zao za kijani zinawapa ajira ya haraka.

Uongozi wa kujuana. Ndugu zangu Watanzania wenzangu. Nani ambaye hajui kuwa Rais wetu anachukia kwa maneno na vitendo juu ya kujuana katika kupeana uongozi? Nadhani karibu kila Mtanzania analijua hili. Rais pia kwa maneno yake mwenyewe alisema kuwa, yeye hakusaidiwa na mtu yeyote kuingia Ikulu. Binafsi sikuamini. Mollel, mmoja kati ya madiwani hawa, anasema bayana kabisa juu ya DC Mnyeti kupata cheo hicho kuwa, yeye ndiye aliyekuwa msaada mkubwa sana katika kutembeza fomu za udhamini wa Rais. Hapa wachambuzi wa siasa mtanisaidia Je, huku si ndiyo kusaidiwa kwenyewe?

Madhara yake ni kwamba, viongozi hawa wamekuwa wakijigamba kuwa wao kwa namna yoyote ile hawawezi kung’olewa teuzi zao kwa sababu wao wapo karibu sana na Rais. Vile vile, wao wamekuwa wakijipambanua kuwa wanao ushawishi wa hali ya juu wa kumfanya mtu yeyote wamtakaye akae sehemu waitakayo au atolewe sehemu kwa sababu zao binafsi kabisa.

Ghiliba za wasaidizi wa Rais. Kutokana na ushahidi huu, Watanzania sasa tujue kuwa, wasaidizi wa Rais wetu wanampotosha sana kwa uongo na udanganyifu wa hali ya juu sana. Rais anapokuwa anahutubia na katikati ya hadhara hiyo anajitokeza kiongozi hasa mteule wa Rais na kumwambia kuwa kuna watu wanakuunga mkono kwa Juhudi zako Mheshimiwa. Watu hawa wametoka chama X wamekuja huku kuunga mkono jitihada zake, ni upotoshaji mkubwa sana ambao yawezekana Rais akashindwa kuwa na takwimu sahihi hasa katika mambo haya ya kisiasa ukizingatia yeye pia ni mwenyekiti wa chama. Sasa hebu tukumbushane jinsi wafanyakazi wa TBC walivyompotosha na kumwambia kuwa Rais Trump amemsifia, sote tuliona wafanyakazi wote tisa wakisimamishwa kazi zao kwa kuupotosha umma.

Sitaki kusema jinsi Rais wangu alivyojawa na jazba pale Arusha baada ya watu waliokuwa wameandaliwa na wateule wake kukosekana, ila niseme tu kwamba, Rais anapotoshwa na wasaidizi wake.

Fedha za umma kutumika kisiasa kwenye ofisi za umma. Kwa lugha nyepesi kabisa hapa ni kunajisi ofisi za umma. Kama tumefikia hatua  biashara ya hongo inafanyika kwenye ofisi za umma, ni dhahiri kuwa, Taifa limepata viongozi ambao wananajisi ofisi za umma mchana kweupe, kitendo ambacho kinamtia aibu na fedheha kubwa Rais wetu na kulidhalilisha Taifa kwa ujumla. Ofisi za umma nchini sasa zimekuwa sehemu stahiki za kufanyia ulanguzi wa madiwani. Zimekuwa sehemu nzuri si kwa kutekeleza maendeleo ya wananchi, bali kukwamisha maendeleo ya wananchi kwa sababu ambazo wanazijua wao. Zimekuwa sehemu nzuri za kupanga na kupangua madili.

Ofisi za umma zimedhalilishwa kwa kiasi kikubwa sana na kuzionesha si kwa Watanzania pekee, bali kwa dunia nzima kuwa ni Tanzania tu ambapo kiongozi wa umma anaweza kukaa na kujadili maadili ya ulanguzi akiwa kwenye ofisi za umma.

Ushauri kwa Rais wangu

Kwenye kitabu kitakatifu cha Kuran, Mwenyezi Mungu ametupa mambo mawili tu ili sisi tuchague; kushukuru ama kukufuru.

Kwa wataalamu wa biblia pia, Mfalme Suleimani alipoambiwa na Mwenyezi Mungu kuwa aombe chochote na Mungu atamtimizia wakati akifanya matoleo yake milima ya Gibeoni, Mfalme Suleimani aliomba vitu viwili tu; hekima na busara ili aweze kuwaongoza kwa haki watu wake.

Sina shaka kuwa, Rais wangu amejaa hekima na busara nyingi sana na amechagua ‘kushukuru’ na ndiyo maana tumekuwa tukimsikia kwa sauti ya unyenyekevu kabisa kuwa Watanzania tumuombee, nami pia naungana na Watanzania wenzangu kumuombea kwa dhati kabisa.

Pamoja na kuwa tunamuombea, lakini pia tumkumbushe pia kuwa, aina ya watu wanaomzunguka wanaweza kuwa ni chanzo cha yeye kukufuru. Anaweza kujikuta anakufuru aidha kwa ushauri mbovu wa wanaomzunguka na/au hata kwa kuwafumbia macho wale ambao Watanzania anaowaomba wamuombee wanamwambia juu ya mienendo yao mibovu; aghalabu ni wateule wake. Sasa Rais wangu akilichukulia suala hili kawaida, amekwisha.

Je, Rais wangu anasoma namna ambavyo Mfalme Belshazzar, Mwana wa Nebuchadnezzar, alivyokwisha kwa kushupaza shingo na kunajisi  Madhabahu ya Bwana? Ndiyo. Rais pia ajifunze kutokana na anguko hilo la Belshazzar ambaye alifikia hatua hadi ananywea pombe vyombo vya madhabahu na kuisifia miungu huku akiwa amezungukwa na karibu watu wote wa hovyo kabisa. Nadhani wataalamu wa Biblia hapa watakuwa wanajua kilichoandikwa ukutani mbele yake; MENE MENE TEKEL UPHARSIN.

Kwa nini Belshazzar alipata anguko hilo? Alianguka kwa sababu hakuwa na washauri wazuri, kwani karibu wote waliokuwa naye, hakuna hata mmoja aliyemshauri kutokuvitumia vyombo vya madhabahu kunywea pombe, badala yake wote walifurahia.

Sasa, sisi Watanzania tunampenda na ndiyo maana karibu kila Mtanzania kwa nafasi yake anajitahidi si tu kumuombea, bali hata kumshauri. Ushauri huu wa Watanzania asiupuuze, kwani wanaomshauri ni Watanzania ambao wana mapenzi naye na nia njema kabisa juu yake.

Kwa vyombo vyenye dhamana ya kupambana na rushwa. Ni lazima vifanye kazi bila kuangalia vinamshughulikia nani, bali vinafanya kazi kwa ajili ya  nani. Ni wakati sasa wa kuhakikisha vinaonesha kwa vitendo kuwa vyombo hivi vina meno na vinaweza kumshughulikia yeyote ili mradi tu ushahidi upo.

Ushauri wangu kwa Watanzania ni kwamba, tuendelee kuomba huku tukipaza sauti. Inaumiza Watanzania wengi pale ambapo ajira zinatolewa kwa kujuana. Inaumiza Watanzania wengi pale ambapo shughuli za maendeleo zinakwamishwa kwa hujuma za kisiasa.

Mimi nadhani, haijalishi vyama vyetu na itikadi zetu, lakini hili tusimame pamoja kuhakikisha tunalisemea na kulipigia kelele. Tukikaa kimya, tutaendelea kuona vijana wengi wanakimbilia kujificha kwenye chama na kuachana na taaluma zao kwani huko ndiko ajira zinatoka kwa wingi, tena kwa vigezo vichache sana. Tanzania ni ya Watanzania na Watanzania ndiyo wamewaweka viongozi wetu hapo walipo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles