Na Mwandishi Wetu, Arusha
JESHI la Polisi mkoani Arusha, limemtaka Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuripoti kituo kikuu cha jeshi hilo bila kukosa.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Lema alisema akiwa njiani kulekea Arusha jana, alipokea taarifa za wito wa polisi wa kumtaka aripoti haraka vinginevyo watatumia nguvu kumtafuta.
“Nimepata taarifa za wito na wanasisitiza nifike leo (jana) mimi ndiyo naingia Arusha, kwa hiyo lazima nionane na wakili wangu kwanza ili kujua namna nitakavyokwenda kwao (polisi).
“Sababu za kuitwa polisi ninaona ni vita baina ya nuru na giza,” alisema Lema
Hatua ya Lema kuitwa Polisi imekuja siku moja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro kutoa onyo kwa baadhi ya watu wakiwamo wana siasa kuingilia suala la kutekwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’ kwa ajenda alizoziita wanazijua wao.
Pamoja na hali hiyo, IGP Sirro, alionya watu hao na kuwataka kuacha mara moja huku akitilia shaka uzalendo wao.
Oktoba 16, mwaka huu Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, alisema njia pekee ya Serikali kujiondoa katika lawama tukio la kutekwa
kwa mfanyabiashara ‘Mo Dewji’ ni kuruhusu vyombo vya nje kufanya uchunguzi.
Kauli hiyo alitoa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya Chadema Kinondoni, Dar es Salaam.
Alisema haitakuwa aibu kwa Serikali kuhusisha vyombo vya nje kwa kuwa hata mataifa yaliyoendelea huwa yanaomba msaada inapobidi.
Alisema mazingira ya eneo ambalo Mo Dewji alietekwa kuna ulinzi wa hali ya juu, kushangazwa na mfanyabiashara huyo kutopatikana hadi sasa.
Lema pia amemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kutozuia watu kujadili tukio hilo.
Hatu hiyo ilitangulia siku moja na uamuzi wa familia ya Dewji kutangaza dau la Sh1bilioni kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwake.
Mbali na Lema pia Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) alihoji hatua kwa hatua ya polisi kushindwa kueleza ukweli alipo Mo kutokana na eneo alipotekewa mfanyabiashara huyo kuwa na kamera za CCTV zaidi ya 30.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Radhaman Ng’anzi alipotafutwa kuzungumzia wito wa Lema, simu yake iliita bila kupokelewa.