25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Laini milioni 15 zisizosajiliwa kwa alama za vidole hatarini kufutwa kabisa

Asha Bani – Dar es Salaam

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), James Kilaba, amesema hadi sasa laini za simu milioni 33 sawa na asilimia 74 zimesajiliwa kwa alama za vidole, huku milioni 15 zikiwa hatarini kufutwa zikibainika kutotumika muda mrefu.

Kwa mujibu wa TCRA laini zilizokuwa zinatumika nchini ni milioni 48, huku zilizosajiliwa kwa alama za vidole hadi sasa zikiwa milioni 33, jambo linalomaanisha milioni 15 hazijasajiliwa kwa alama za vidole.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Usalama Mtandaoni iliyowakutanisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu, Kilaba alisema idadi ya laini zilizosajiliwa kwa alama za vidole inaongezeka siku hadi siku.

Kuhusu laini ambazo bado hazijasajiliwa, alisema; “kuna baadhi ya watu hadi sasa hawajasajili kwa alama za vidole, pia hawana mpango wa kusajili, zikiendelea kukaa muda mrefu zitafutwa kabisa.”

Januari 20, mwaka huu Serikali ilianza kwa awamu kuzima laini ambazo hazijasajiliwa ambapo  walianza na 900,000 na huku wakiendelea kidogo kidogo kwa kufuata utaratibu waliojiwekea.

Kuhusu usalama mtandaoni, Kilaba alisema hadi kufikia Desemba 2010 idadi ya watumiaji wa mtandao wa intaneti ilikua milioni 26.7 huku gharama za huduma ya mawasiliano zikipungua kwa kiasi.

“Mtakubaliana na mimi kwamba maendeleo huja na faida na madhara pia, tuchukue mfano wa barabara nzuri ya lami inapokamilika kujengwa, kiukweli inaongeza tija kwani magari kwenda kwa mwendo kasi, lakini kama hakutakuwa na utaratibu zaidi, ajali nyingi zitatarajiwa kutokea, hivyo kusababisha kupoteza rasilimali watu na pesa.

“Katika nyakati hizi mtandao wa intaneti ni uti wa mgongo wa uchumi wa kidijitali, ukirahisisha utekelezaji wa shughuli nyingi za kijamii na kichocheo kikubwa cha uvumbuzi na hivyo kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi na ustawi wa watu wake,’’alisema Kilaba.

 Alisema pamoja na mtandao wa intaneti kuwa chanzo kikuu cha habari mbalimbali  za kuelimisha na kuburudisha, lakini ni nyenzo muhimu ya kunganisha, kuwasiliana na kubadilishana taarifa mbalimbali.

“Tumeshuhudia pia watu wengi wakiinuka kiuchumi kwa kutumia mtandao, wengi wameweza kufanya biashara na kuinua maisha, pia kuboresha utoaji wa huduma kupitia mifumo mbalimbali ya kielektroniki kwenye tozo za Serikali, ankara maji, umeme, malipo ya ada,’’ alisema.

Kilaba pia alisema pamoja na manufaa mbalimbali, lakini matumizi mabaya ya mtandao yanaweza kusababisha  athari kwa watumiaji na hata miundombinu inayotumika kutoa huduma mtandaoni na matokeo yakawa kupoteza fedha, na hata ukosefu wa huduma mbalimbali.

Alisema kundi la watu wasio wema wamekuwa wakitumia mitandao kuwalaghai vijana na kusababisha unyanyasaji wa kijinsia.

“Uwezo wa mtandao kuficha utambulisho wa mtumiaji umewawezesha watu wenye nia ovu kujifanya ni vijana wadogo na kuwashawishi vijana kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo,” alisema Kilaba.

Pia alisema wizi wa utambulisho ni moja ya tukio baya mtandaoni na hutokea pale ambapo picha na taarifa za  mtu binafsi ikiwa ni pamoja na majina, tarehe ya kuzaliwa, sehemu anakotoka zinatumika kwa kutumia mtandao.

“Takwimu zinaonyesha vijana wengi wameingia kwenye hatari hii ya kiusalama kutokana na kushirikiana nywila  za akaunti zao, suala ambalo ni miongoni mwa matukio ya kiusalama yanayowakabili vijana katika miaka ya hivi karibuni,’’ alisema Kilaba.

Pia alisema katika kutambua umuhimu wa mtandao katika kuongeza tija na ufanisi na mchango kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Serikali imefanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha usalama wa mitandao na watumiaji wake unaimarika.

Alizitaja jitihada hizo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kituo cha mwitikio wa kukabiliana na majanga ya kompyuta (TZ-CERT) ambacho kitakuwa na majukumu ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi bora na salama ya mtandao na mifumo ya Tehama.

Naye mmiliki wa mtandao wa kijamii ambaye pia ni mtangazaji wa kituo cha Radio Clouds, Milard Ayo, amewataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa, hasa ya kujipatia kipato na si kukomenti kwa jazba na matusi katika kurasa za watu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles