NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KWA miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko toka kwa wazazi,wadau,wanafunzi na hata serikali juu ya ufaulu usioridhisha wa wanafunzi wa kidato cha nne.
Ufaulu huu usioridhisha unakaribia kukubalika katika jamii ya kitanzania kwani sababu zilizotolewa ni nyingi na hakuna dalili kuwa zinafanyiwa kazi.
Awali kulikuwa na viwango vinavyoeleweka katika ufaulu na hivyo mwanafunzi aliyepata chini ya hapo alihesabika kuwa amefeli na hakukuwa na namna nyingine zaidi ya kurudia darasa au kwenda shule za binafsi.
Lakini pia kabla ya kufikia hatua ya kufanya mtihani wa darasa la saba kila mwalimu mkuu na walimu wote wa darasa husika walifanya kila wawezalo kuhakikisha wanafunzi wanafaulu.
Wajinga walikuwepo hata wasiojua kusoma na kuandika lakini walimu bado walikuwa na idadi kamili ya wanafunzi wao wanaowategemea katika mwaka huo.
Hali hii ilianza kubadilika taratibu kuanzia mwaka 1995 zilipoanza kujengwa shule za sekondari katika maeneo ya vijijini na mitaani maarufu kama “shule za kata”.
Msisitizo wa ujenzi wa shule hizo ulishika kasi mwaka 2005 ambapo shule nyingi zilijengwa na idadi ya wanafunzi wanaochaguliwa kuingia kidato cha kwanza ikaongezeka kwa zaidi ya asilimia 200.
Hapa ndipo neno ‘kufaulu’ lilibadilishwa na kuwa ‘kuchaguliwa’.
Kuna tofauti kati ya kufaulu na kuchaguliwa; anayefaulu ni lazima afikie viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa matakwa ya hatua husika.
Kufaulu ni lazima ufanye kazi ya ziada badala ya kusubiri rehema za Mwenyezi Mungu. Tunapokuja kwenye neno kuchaguliwa; hapa kuna bahati, rehema za Mungu, mahitaji na kadhalika.
Hapo ndipo kiwango chetu cha kufaulu kilipoanza kuporomoka kwani wanafunzi wanachaguliwa kujaza nafasi zilizopo hata kama hawakufaulu.
Ujenzi wa shule za kata ulikuwa ni mpango mzuri lakini yapo maswali mengi ya kujiuliza. Moja ya maswali hayo ni kwa nini hatukujenga shule kulingana na mahitaji ya ufaulu?
Lakini pia ni kwa nini tunawachukua wanafunzi wanaochaguliwa badala ya wanaofaulu?
Ukweli ni kuwa ufaulu haujapungua na wala idadi ya wanaofeli haijaongezeka kwani idadi ya waliokuwa wanafaulu mwaka 1994 ni sawa na waliofaulu mwaka 2014. Tofauti iliyopo kati ya mwaka 1995 na 2014 ni idadi tu ya watahiniwa ambao ndiyo hao wanaochaguliwa bila kufaulu.
Nionavyo mimi wanafunzi hawajafeli kwa sababu hawajawahi kufaulu mahala popote.
Labda nitoe mfano kidogo unaonihusu mimi.
Machi mwaka 2011 nikiwa mwalimu katika moja ya shule hapa Dar es Salaam tuliwaandikia barua wazazi na walezi wote kuwa yeyote ambaye mtoto wake alichaguliwa na hajaripoti shule afike shuleni na mtoto wake au kama ameamua kumpeleka shule binafsi afike na uthibitisho vinginevyo atashtakiwa kwa mujibu wa sharia.
Mzee mmoja mwenye umri zaidi ya miaka 60 alifika shuleni akiwa na mjukuu wake ambaye alichaguliwa kujiunga na shule yetu lakini alikuwa hajaripoti.
Mzee huyo alijitambulisha mbele yetu tukiwa walimu watatu na akauliza mara tatu kutaka kuthibitisha kama kweli sisi ni walimu.
Tukamjibu sisi ni walimu, akatuuliza kama kweli tumesoma tukamjibu kuwa tumesoma.
Kwa kuwa alikuwa akiuliza akiwa na hasira tukamwelekeza ofisini kwa mkuu wa shule lakini alikataa kwenda akituambia “Nyie si mmesema ni walimu? Tukamjibu tena kwa mara nyingine.
Akafungua mkoba wake akatoa barua tuliyomwandikia, tukaitambua kuwa ni barua yetu. Mazungumzo yalikuwa marefu lakini shida yake ni kuwa mjukuu wake alikuwa hajuwi kusoma wala kuandika hivyo hakuwa tayari kumlipia na zaidi alitaka kumuona Rais jambo ambalo lilikuwa nje ya uwezo wetu.
Mzee alituambia tumjaribu mjukuu wake na endapo ataweza kusoma na kuandika yeye atakuwa tayari kumlipia bila tatizo. Mwalimu mmoja alimchukuwa mwanafunzi yule na kuanza kumjaribu kadiri ya maelezo ya mlezi.
Tulichokigundua ni kuwa yule mwanafunzi alikuwa hajuwi kusoma wala kuandika, lakini kutokana na baadhi ya wazazi na walezi kutopenda kuwasomesha watoto wao tulimuuliza shule ya msingi alikosoma na kwa bahati nzuri ilikuwa shule ya jirani tukaamua kumpigia mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Mwalimu mkuu akatuthibitishia ya kuwa huyo ni mwanafunzi wake lakini ni kweli uwezo wake wa kusoma ni mdogo ingawa amefaulu. Huo ni mfano halisi uliokuja mbele yangu mimi binafsi. Yule mzazi alirudi nyumbani na mjukuu wake na taratibu zingine zilifuata.
Kwa nini nimeamua kuwapa mfano huu; ni kwamba wanafunzi wa aina hii wapo wengi na ndiyo hawa wanaomaliza kidato cha nne kisha tunalalamika kuwa hawajafaulu. Watafauluje wakati hawajawahi kufaulu?
Lakini pia Kitendo cha kuwachanganya wanafunzi waliofaulu na waliochaguliwa kinawavunja moyo wale waliofaulu kwani hawaoni matunda ya jitihada zao za kusoma kwa bidii.
Hilo ni moja lakini pili suala la mitaala na vitabu vinavyotumika kuwafundishia wanafunzi shule za msingi zimethibitishwa na nani?
Kama huamini hebu nenda duka la vitabu umwambie muuzaji akupe kitabu cha kiswahili darasa la tatu, utaulizwa kitabu cha mwandishi yupi? Maana yake ni kwamba kuna vitabu vingi sokoni lakini vyenye ujuzi tofauti.
Leo hii ni rahisi kusikia mtu aliyesoma miaka ya 1980 au 1990 akikumbuka hadithi Sungura (sizitaki mbichi hizi), siku ya gulio katerero, kibanga ampiga mkoloni, Juma na Rose na hata Mnenge na Mandawa.
Umewahi kujiuliza kwa nini hadithi hizo hazisahauliki?
Jibu ni kwamba ziliandaliwa kwa utalaamu wa hali ya juu kulingana na umri wa wanafunzi na ujuzi unaotakiwa katika darasa fulani. Leo hii hali ni tofauti kabisa, kila mmoja anajiandikia kitabu chake kisha anakifikisha kwenye maduka tayari kuingia sokoni.
Leo hii mwanafunzi wa darasa la tano hawezi kuchora ramani ya Tanzania na kuonesha mikoa yote kama ilivyokuwa hapo kabla kwani hata kitabu cha ramani kiitwacho ATLAS hakipo, kilichopo kinaonesha mikoa 21 ya Tanzania bara na mitano ya visiwani.
Mkoa pekee mpya kwenye ramani hiyo ni Mkoa wa Manyara. Lakini pia kwenye Atlasi hiyo idadi ya nchi za Afrika ni tofauti na hali halisi kwani nchi ya Sudan ni moja na wala si kusini na kaskazini.
Kwa mazingira hayo tunategemea ufaulu wa aina gani kama kila mwanafunzi anasoma kitabu chake mwenyewe na kila mwalimu anafanya anavyojua mwenyewe?
Namkumbuka mwalimu wangu wa sayansi kimu darasa la sita 1991, Mwalimu Cecilia Nyambaya alinifundisha kupika chakula cha mtoto mchanga kwa kutumia viazi vitamu na pia nikiwa darasa la tatu alinifundisha kunyoosha nguo kwa kutumia pasi ya mkaa ambapo tulikuja na nguo zilizojikunja kisha tunanyoosha.
Elimu ilikuwa na malengo kwa kila hatua,walimu walikuwa na moyo wa kufundisha,uhusiano wa wazazi na walimu wa shule za vijijini ulikuwa mkubwa sana na hali halisi ilionesha walimu kuwa na unafuu wa maisha tofauti na wanakijiji.
Hali hiyo ni kinyume chake kwa sasa. Mwanafunzi aliyechaguliwa hawezi kufaulu kwa miujiza.