NA JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM
TANGU Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana huku akiapa kutekeleza ahadi yake ya kutumbua majipu, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa haipiti kati ya wiki moja na mbili pasipo Serikali yake kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi wa umma wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali.
Tayari watumishi wanaokadiriwa kufikia 160 wameadhibiwa na wengine kusimamishwa kazi kimyakimya au hadharani katika wizara na taasisi mbalimbali za umma.
Katika uchunguzi wake, gazeti hili limebaini kuwa mwezi huu wa Februari ndio unaoongoza kwa kuwa na orodha ndefu ya watumishi waliotimuliwa, wakifikia takribani 60.
Pamoja na hilo, wafanyakazi mbalimbali wa baadhi ya taasisi za umma waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wameeleza kufanya kazi kwa hofu kubwa, wengi wakijenga imani kwamba hawajui kesho yao ikoje.
Katika hilo, gazeti hili linazo taarifa ambazo hazijathibitishwa na mamlaka husika, kwamba wapo watumishi ambao wamesimamishwa kazi kimyakimya. Kwa mfano Wizara ya Nishati na Madini ambako inaelezwa Kamishna wa Madini, Mhandisi Paul Masanja na Kamishna wa Nishati, Mhandisi Hosea Mbise nao wamesimamishwa kazi.
Ifuatayo ni orodha ya watu waliosimamishwa kazi na kutangazwa waziwazi tangu Serikali ya Magufuli iingie madarakani.
Â
Desemba 7, 2015
Sindano ya utumbuaji majipu ilianzia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk. Shaaban Mwinjaka, baada ya kutenguliwa uteuzi wake na Rais Magufuli ili kupisha uchunguzi dhidi ya matumizi mabaya ya kiasi cha Sh bilioni 13 katika Shirika la Reli Tanzania (TRL).
Aidha kutokana na utendaji mbovu na hatua kutochukuliwa katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).
Rais Magufuli alivunja pia Bodi ya Bandari na kutengua uteuzi wa Mwenyekiti wake, Profesa Joseph Msambichaka na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe.
Pamoja na hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwasimamisha kazi wasimamizi wanane wa bandari kavu (ICD) ambao ni Happygod Naftali, Juma Zaar, Steven Naftali Mtui, Titi Ligalwike, Lydia Prosper Kimaro, Mkango Alli, John Elisante pamoja na James Kamwomwa.
Pia watumishi wa TPA waliohusika kutoa makontena bandarini walisimamishwa kazi akiwamo Shaban Mngazija, aliyekuwa Meneja Mapato ambaye kwa sasa amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Fedha.
Waziri Mkuu aliwataja maofisa wengine kuwa ni Rajab Mdoe, aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mkuu wa Bandari Kavu (ICD), ambaye amehamishiwa Makao Makuu kuwa Naibu Mkurugenzi Co- Operate Service, Ibin Masoud, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Apolonia Mosha, Meneja Bandari Msaidizi wa Fedha.
 Novemba 9, 2015
Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kukuta madudu yaliyokuwa yakiendelea jambo lililomfanya kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Hussein Kidanto.
 Novemba 21, 2015
Tumbua tumbua ya majipu ilihamia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya Waziri Mkuu, Majaliwa kufanya ziara ya kushtukiza bandarini na kumsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rished Bade.
Kadhia hiyo pia iliwakumba watumishi wengine, wakiwamo Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki na Habibu Mponezye wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, Haruni Mpande, Hamisi Ali Omari wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano na Mkuu wa Kitengo cha Bandari Kavu (ICD In-Charge), Eliachi Mrema.
 Novemba 29, 2015
Waziri Mkuu Majaliwa aliwafukuza kazi wafanyakazi watatu wa TRA; Anangisya Mtafya, Msajigwa Mwendengele na Robert Nyoni.
Desemba 16, 2015
Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea akidai haendani na kasi yake.
Watumishi wengine wanne wa Takukuru pia walisimamishwa kazi ambao ni Mary Mosha, Ekwabi Mujungu, Doreen Kapwani na Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha kusafiri kutoka kwa Rais au Katibu Mkuu Kiongozi.
Siku hiyohiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Mussa Iyombe, alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Mhandisi Mussa Natty kwa tuhuma za kukosa uadilifu katika ubinafsishaji wa eneo la ufukwe wa bahari la Coco na malalamiko ya wananchi juu ya viwanja katika eneo la Kinondoni, ulioambatana na usimamizi duni wa watumishi, hasa sekta ya mipango miji na ardhi.
Tuhuma nyingine ilikuwa ni usimamizi mbaya uliosababisha barabara za Manispaa ya Kinondoni kujengwa chini ya kiwango na kutochukua hatua kwa watendaji wa manispaa waliokuwa chini yake.
 Desemba 17, 2015
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alimtimua kazi mkandarasi aliyekuwa anajenga mfereji wa Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es Salaam.
 Desemba 22, 2015
Siku hiyo ilikuwa mbaya kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Miliki ya Rasimali za Reli (RAHCO), Benhadard Tito ambapo Serikali iliivunja Bodi ya Wakurugenzi na kutengua uteuzi wake.
 Januari 5, 2016
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, aliwatimua wakurugenzi wote wa Bodi ya NARCO yenye dhamana ya kusimamia ranchi za taifa.
Hiyo ilikuwa ni baada ya bodi hiyo kushindwa kutelekeza mradi wa NARCO na kupendekeza kujengwa kwa mradi mwingine kama huo ndani ya eneo hilohilo la ranchi ya Ruvu.
 Januari 6, 2016
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alitangaza kuwasimamisha kazi Mkurugenzi wa Mipango na Matumizi endelevu ya Rasilimali za Misitu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mohammed Kilongo, pamoja na maofisa wa misitu wa mikoa yote nchini kupisha uchunguzi wa ubadhirifu uliobainika.
 Januari 15, 2016
Rais Magufuli alimsimamisha kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Faisal Issa kwa tuhuma za utovu wa nidhamu aliouonyesha wakati wa kikao cha Kamati ya Usalama ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza alikuwa mmoja wa waliokuwamo katika kikao hicho.
 Januari 21, 2016
Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Eliakimu Maswi kuwa Kaimu Naibu Kamishna wa TRA na kumrejesha kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara.
Siku hiyo hiyo, aliwasimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, Sylvester Ambokile na Kamishna wa Uhamiaji anayeshughulikia utawala na fedha, Piniel Mgonja ili kupisha uchunguzi kutokana na dosari zilizobainishwa na  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, alipotembelea Idara ya Uhamiaji.
 Januari 23, 2016
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, alimsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa mradi wa mabasi yaendeyo haraka Dar es Salaam (DART), Asteria Mlambo.
 Januari 25, 2016
Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Dickson Maimu aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya taifa (NIDA).
Pamoja na Maimu, wengine waliosimamishwa ni wasaidizi wake, Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph Makani; Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande; Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Pia alitengua uteuzi wa Mhandisi Madeni Kipande, kabla ya kuthibitishwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Siku hiyo pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, January Makamba, alimwachisha kazi Heche Suguta ambaye ni wakili daraja la pili katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na wenzake wawili kwa kukiuka miiko ya kazi katika kusimamia kiwanda cha kusindika minofu ya punda kilichopo Dodoma.
Mbali na Suguta, wengine waliosimamishwa ni Ofisa Mazingira Mwandamizi, Dk. Eladius Makene  na Ofisa Mazingira, Boniface Kyaruzi.
 Januari 29, 2016
Rais Magufuli alimtimua Mkurugezi Mtendaji Mkuu wa Mji wa Bariadi, Erica Mussika, kwa kushindwa kusimamia mradi wa barabara wa Sh. bilioni 9.192 unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
 Februari 10, 2016
Baada ya Serikali kubaini wizi wa takribani shilingi milioni 700 katika Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kupitia kampuni ya wakala wa ukatishaji tiketi ya Salama World Travel iliyopo visiwa vya Comoro, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa ATCL, Steven Kasubi ili kupisha uchunguzi.
 Februari 12, 2016
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alimwondoa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro (Kinapa), Erastus Lufungulo na kutoa maagizo mazito kwa kampuni za wazawa.
Februari 13, 2016
Waziri Mkuu, Majaliwa aliwasimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Mafuta, Bernadina Mwijarubi, ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kutotumia mita kupima nishati hiyo.
 Februari 15, 2016 Â
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu, aliwasimamisha kazi wakurugenzi wa Bohari ya Dawa ya Taifa (MSD) kwa ubadhirifu wa fedha takribani shilingi bilioni 1.5.
Waliosimamishwa kazi ni Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Joseph Tesha, Mkurugenzi wa Ugavi, Misanga Muja, Mkurugenzi wa Manunuzi, Heri Mchunga na Mkurugenzi Kanda na Huduma kwa Wateja, Cosmas Mwaifani.
Siku hiyo pia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliwahamisha kazi watendaji wa juu wa TPA baada kuisababishia Serikali hasara kwenye upotevu wa makontena katika bandari ya Dar es Salaam.
Watendaji waliohamishwa ni Piter Gawilo ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi wa TPA, Mashaka Kishanda ambaye nafasi yake imechukuliwa na Benito Kalinga ambaye awali alikuwa mtumishi wizarani hapo na Kaimu Mkurugenzi wa TEHEMA, Kalian Charles.
Februari 16, 2016
Waziri wa Elimu Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisitisha mkataba wa kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, George Nyatenga.
Pia aliwasimamisha kazi wakurugenzi watatu wa bodi hiyo ambao ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo.
Siku hiyo hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliwasimamisha kazi watumishi wawili wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ambao ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Matukio, Mbwilo Kitujime na Meneja wa Vipindi, Edna Rajab. Uamuzi huo ulifikishwa kwenye Bodi ya TBC kwa hatua zaidi.
 Februari 18, 2016
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alitengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Mji wa Tunduma, Halima Mpita kwa kutumia vibaya madaraka yake.
Siku hiyo pia Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alitoa taarifa ya kuwasimamisha na kuwastaafisha kwa manufaa ya umma baadhi ya wakurugenzi wa TCRA.
Hatua hiyo ilitokana na kutofungwa kwa kifaa kinachowezesha mtambo wa kufuatilia Mapato ya Simu (TTMS) hali iliyosababisha Mamlaka ya Mawasiliano na Mamlaka ya Kodi kushindwa kubaini mapato halisi ya makampuni ya simu, na hivyo kushindwa kukokotoa kodi stahiki zinazotakiwa kulipwa na makampuni ya simu nchini na kuikosesha Serikali mapato ya kiasi cha shilingi bilioni 400.
Waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkurugezni wa Idara ya Sheria, Elizabeth Nzagi na wasaidizi wao akiwemo Kaimu Mkurugenzi anayesimamia Mtambo wa Kuchunguza Mapato katika Mitandao ya Simu (TTMS), Injinia Sunday Richard na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Modestus Ndunguru.
 Februari 19, 2016
Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Michezo (BMT), Henry Lihaya aling’olewa kwenye nafasi hiyo huku Nape akimwagiza Katibu Mkuu wa wizara yake amtafutie nafasi nyingine wizarani.