29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kwa ishara hizi kama Taifa tuko pabaya

NILIWAHI kusikia mahali kuwa ukitaka kuifahamu dhamira ya mtu basi yatazame matendo yake, hapo ndipo utakapojua kama mtu huyu ana dhamira ya dhati ama ni mbabaishaji. Kama taifa ili tusonge mbele yatupasa kuwa na uchaguzi wa nini cha kufanya nini si cha kufanya kuanzia mtu mmoja mmoja mpaka kitaasisi na ukiona jambo linafanywa kwa mzaha kwenye ngazi ya kitaasisi basi fahamu fika kuwa kama jamii au taasisi mko pabaya.

Leo nataka nizungumze na vyombo vya habari, juma lililopita kuna mambo ya kijinga kama si upuuzi yalienea kwenye vyombo mbalimbali haswa kwenye mitandao ya kijamii, ujinga uliofanywa na mtu yule yule anayefahamika kwa kufanya mambo ya kijinga yale yale aligeuka kuwa gumzo tena kwa kueneza picha za mambo ya faragha, kwake yeye imekuwa kama mtindo kufanya mambo ya ovyo. Leo wala sitaki kumzungumzia yeye  maana utakuwa ni mwendelezo wa kufanya yale yale ninayotaka kukemea.

Sote tunafahamu kuwa ukiacha sababu ya kujipatia kipato kwenye sekta ya habari bado dhamira kuu ya vyombo vya habari ni kuhabarisha umma juu ya nini kinachoendelea, na Wazungu wana msemo wao unaosema “Information is powe” ikiwa na maana taarifa ama habari ni nguvu yaani ukiwa na taarifa juu ya jambo fulani ndipo unapopata nguvu ama mamlaka ya kuongea juu ya jambo Fulani.

Leo hii huwezi kutoka mbele ukataka kutetea ama kusema juu ya jambo lolote kama huna taarifa juu ya jambo husika, hata kwenye mambo ya biashara ushauri wa kwanza ambao anapatiwa mfanyabiashara ni kuwa na taarifa za kutosha juu ya masuala ya masoko na ndio iko hivyo hivyo kwenye idara nyingine na kwa kusema haya sitosita kusema kuwa tasnia ya habari inahusika moja kwa moja ama kujenga taifa imara ama kulibomoa.

Kwa miaka ya karibuni taifa letu limekuwa linaendeshwa mno na mambo ya kipuuzi, kama taifa ni mara chache sana tumekuwa tunajikita kwenye mijadala mizito na hapa ndipo tunaposhangaa na kujikuta tunatengeneza watoto wengi wanaotamani kuwa kama watu fulani na si kuwa kama Mama Anna Makinda ama Mama Samia.

Baadhi ya watu wanaofanya madudu kesho yake huita vyombo vya habari kuomba msamaha niliona vyomo vya habari vingi vikijitokeza kwenda kusikiliza lakini wanachokifanya ni kile kile ambacho huwa wanafanya siku zote, kubomoa na kujaribu kujenga lakini kuna siku Mheshimiwa Zitto wakati wa Bunge la Bajeti alijaribu kuichambua Bajeti na sikuona wingi wa vyombo kama walivyojitokeza kwa wanaofanya madudu na hata juzi kwenye ‘press’ iliyofanywa tena na Mheshimiwa Zitto kuhusu suala la Usalama wa Taifa na sakata la korosho bado sikuona vinasa sauti vya  ‘mainstream media’ mezani nikajiuliza kama taifa tuna shida gani? Ina maana habari za wanaofanya madudu zina umuhimu sana kuliko suala la usalama wetu kama taifa? Ni wapi tunaelekea?

Kiukweli kama taifa bado tuna changamoto na safari ndefu, bado hatuweki mbele vipaumbele vyenye maslahi mapana kwa taifa, bado sisi kama vyombo vya habari tuna kazi kubwa ya kufanya, mimi binafsi wakati niko mdogo pamoja na kusikiliza nyimbo nyingi za  wasanii wa bongo fleva bado nilivutiwa zaidi na Mwalimu Nyerere kuliko Juma Nature na hilo si kwamba lilitokea tu hapana, hayo yalikuwa ni matokeo ya elimu niliyoipata pamoja na mchango wa vyombo vya habari lakini miaka ya karibuni nimeshuhudia watoto kadhaa wa shule wakiulizwa Rais wa Tanzania ni nani wanajibu Diamond Platinum hapo ndipo tulipofika kama taifa ila suala kama hilo halikuwa rahisi kutokea miaka ya nyuma mtoto wa shule akujibu rais ni Profesa Jay badala ya Mkapa.

Watanzania tuna tabia ya kula kile ambacho kipo mezani hivyo tunacholetewa na vyombo vya habari ndicho tunachopokea huwa hatuna muda wa kutafuta kisicho mezani. Siku moja nikiwa na mzee mmoja aliniuliza hivi inawezekana kabisa Diamond akawa na ushawishi mkubwa kuliko rais wa taifa? Nikamuuliza kwa nini? Akanijibu mimi leo ni kwa mara ya pili nimewashuhudia Watanzania wengi  wakisikiliza redio kwa wingi, mara ya kwanza nilishuhudia kipindi cha vita ya Kagera Taifa zima lilimsikiliza Mwalimu wakati anatangaza kumshughulikia Idd Amin na leo ndio mara ya pili tunamsikiliza huyu Diamond sijui ameenda kwenye vyombo vya habari kumkubali mwanae aliyezaa na mwanamke mwingine.

Ilikuwa ni ngumu kumkatalia Yule mzee lakini huo ndio ukweli mchungu, kama taifa tuko pabaya, vyombo vya habari tuna deni kubwa na jamii na tukijisahau taifa linateketea mikononi mwetu, tubadilike tujenge nchi, kwa hali ya taifa letu sidhani kama tunahitaji kuwa tunasikiliza masuala ya watu binafsi haswa yale ya kijinga, tusisahau ule msemo wa akili ndogo hujadili watu.

Nawasilisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles