Na Upendo Mosha,Moshi
Wizara ya Maliasili na Utalii, imewataka wadau na wawekezaji katika sekta hiyo hapa nchini kutumia fursa zilizopo na kuwa wabunifu katika uwekezaji jambo ambalo litawanufaisha kikamilifu na rasilimali za Taifa badala ya kuachia makampuni ya kigeni.
Akizungumza jana, Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Allan Kijazi, wakati akifungua warsha ya utalii endelevu Kanda ya kaskazini,alisema wanufaika wakubwa wa utalii hapa nchini ni makampuni ya kigeni na sio wazao jambo ambalo sio sahihi.
Alisema ni vema sasa wadau na wawekezaji kuona umuhimu wa kutumia frusa zilizopo katika utalii na kunufaika nazo moja kwa moja tofauti na ilivyo sasa ambapo makampuni ya kigeni ndio yamekuwa wakitumia frusa hizo zaidi ya watanzania.
“Makampuni ya kigeni ambayo yamewekeza kwenye utalii hapa nchini ni mengi wazawa mmekuwa hamchangamkii frusa …wafanyabishara wetu ni kweli bado mmekuwa na changamoto katika ubunifu ni wakati sasa wa kuamka na kuwa wabunifu ili mnufaike,”alisema
Aidha, alisema ni wakati muafaka sasa kwa wataalamu kufanya utafiti na kufahamu ni kwa nini wafanyabishara katika sekta ya utalii hapa nchini wanashindwa kuwa wabunifu na kushindwa kumudu soko la utalii tofauti na wafanyabishara wa nchi jirani
“Ufanyike utafiti ni kitu gani wafanyabishara wetu wanakwama na kutafutwe namna ya kuwajengea uwezo ili na sisi kama nchi tuwe na sekta binafsi ambayo ni imara na yenye uwezo wa kushindana kwenye soko la utali dunia,”alisema
Katika hatua nyingine Dk. Kijazi alisema wizara hiyo ilifanikiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka watalii milioni 1.1 Mwaka 2015/2016na kufikia watalii milioni 1.5 Mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 34 na kwamba ongezeko Hilo Ni dogo ikilinganishwa na vivutio vikivyopo nchini.
“Licha ya kufanikiwa kuongeza watalii Ila ongezeko ni dogo sana na sasa tumepewa jukumu la kuongeza watalii kutoka milioni 1.5 ya sasa na kufikia watalii milioni tano ifikapo Mwaka 2025 na Hilo litaenda sambamba na kuongeza mapato ya utalii kutoka Dola billion Moja kwa mwaka 2018/2019 na kufikia Dola bilioni sita,”alisema
Naye, Mtafiti wa masoko ya utalii katika chuo kikuu cha Dar es Salam, Prof. Wineaster Anderson, amesema tafiti zilizofanywa kwa zaidi ya miaka 40 na chuo hicho zinaonyesha changamoto zinazoikumba sekta ya utalii nchini zinatokana na makampuni ya utalii kushindwa kuwa waaminifu katika shughuli zao na kutapeli wageni.
“Changamoto nyingine ni makampuni ya utalii kushindwa kutangaza vizuri vivutio vikivyopo hapa nchini pamoja na wageni kushindwa wanazotozwa pindi waingiapo nchini,”alisema
Aidha alisema ipo haha kubwa ya makampuni hayo kuwa wabunifu katika shughuli zao na kuacha mara moja tabia ya kuwalaghai wageni ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyopo nchini.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Makampuni ya talii hapa nchini (TATO), Hendry Kimambo,alikiri kuwepo kwa changamoto hizo hususani kwa makampuni yasiyokuwa na usajili na yaaiyo tambulika kisheria.