NA AZIZA MASOUD,
MTOTO anahitaji kuwa katika mazingira ya usafi wa hali ya juu muda wote ili kumkinga na mambo mbalimbali, ikiwamo maradhi .
Usafi, hasa upande wa mavazi ni njia pekee ya kumwepusha mtoto na baadhi ya maambukizi ya maradhi yatokanayo na uchafu, ikiwamo ugonjwa wa ngozi na mengineyo.
Aidha, nguo chafu, hasa za ndani kwa watoto, mfano nepi na chupi humfanya mtoto kuchunika mapaja, hali inayosababishwa na kukaa na unyevunyevu kwa muda mrefu.
Mbali na madhara hayo, mtoto msafi huwa na mvuto na kuwafanya baadhi ya watu wapende kumbeba.
Kuna baadhi ya wazazi wanakuwa wavivu kuwaweka watoto wao katika hali ya usafi, hivyo humvalisha mtoto nguo moja siku nzima bila kumbadilisha.
Mtoto mdogo anapaswa kubadilishwa nguo hata zaidi ya mara nne kwa siku kulingana na mazingira yake ya kucheza na eneo analoishi.
Muda wa asubuhi mtoto anapaswa kuoga mara mbili sambamba na kubadilishwa nguo, ambapo mara nyingi inakuwa saa moja ama mbili baada ya kunywa uji, vivyo hivyo kwa mchana.
Mpe uhuru acheze na wenzake, huku ukimwangalia kama amejisaidia kwenye nguo katikati ya saa tano na sita, unapaswa kumrudisha nyumbani na kumbadilisha tena nguo baada ya kumwogesha.
Baada ya hapo, mwache mtoto achague kama anahitaji kulala au kucheza, lakini ikifika saa nane hakikisha unamwogesha na kumbadilisha tena nguo.
Usafi wa usiku, hasa katika kuoga, utategemea na hali ya hewa, ikiwa baridi sana unaweza ukamfuta kwa kitambaa laini, kumbuka kumbadilisha nguo anapojisaidia kipindi chote huku akiwa anasubiri kulala.
Jinsi ya kufua nguo za mtoto
Mzazi unapaswa kuwa makini katika kufua nguo za mtoto, hakikisha unatenganisha nguo za rangi na nguo nyeupe, hasa nepi.
Mbali na kuangalia rangi, pia unapaswa kuangalia aina ya uchafu, epuka kuchanganya nguo za mtoto aliyejisaidia haja kubwa ama zenye uchafu mwingi na nguo za mikojo.
Gauni za rangi na nguo nyingine zinapaswa zifuliwe tofauti na nyeupe.
Baada ya kufua tafuta dawa za kunyunyizia nguo za watoto ili kuondoa harufu ya shombo ya maziwa.
Hakikisha unaanika kwenye kamba na zinakauka sawasawa na baadaye zinyooshwe pasi ili kuua vijidudu, zikunje vizuri na kuziweka kabatini.