28.6 C
Dar es Salaam
Saturday, January 28, 2023

Contact us: [email protected]

HUYU NDIYE ANAYUMBISHA URAIS WA TRUMP

WASHINGTON, MAREKANI

TANGU Novemba 8 alipotangazwa kushinda kiti cha urais wa Marekani, Donald Trump alitajwa kusaidiwa kwa karibu na Serikali ya Urusi. Awali ilikuwa tetesi juu ya uhusiano wa karibu kati ya Trump na Rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Mara kadhaa timu ya kampeni ya Trump ilikanusha suala hilo, lakini hali imekuwa ngumu sana. Wananchi wa Marekani wanafahamu fika sasa kulikuwapo na ukaribu baina ya Trump na Putin.

Kulikuwapo ukaribu kati ya maofisa wa kampeni wa Trump na Serikali ya Urusi. Tatizo linalowasumbua wananchi hao ni kitu gani au mambo gani yalikuwa yakizungumzwa baina ya pande hizo mbili mbali ya kushinda uchaguzi wa mwaka jana?

Kabla ya kuapishwa na baada ya kuapishwa, bado Trump amekuwa akiandamwa juu ya uhusiano wake na Putin. Hatua hiyo imesababisha Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Jeff Sessions, kujiondoa rasmi kutoka kwenye uchunguzi kuhusu uhusiano kati ya timu ya kampeni ya Donald Trump na Urusi.

Wabunge kutoka chama cha Democrat wameshikilia bango suala hilo, huku kiongozi wao bungeni, Nancy Pelosi akimlaumu Sessions kwa kuidanganya kamati iliyokuwa ikimuidhinisha mwezi Januari.

“Kwamba mwanasheria mkuu, mlinzi mkuu wa sheria nchini alidanganya Wamarekani kwa kula kiapo, ni msingi tosha kwake kujiuzulu. Amethibitisha kuwa hajahitimu na hastahili kutumikia wadhifa unaohitaji uaminifu,” alisema Pelosi.

Akizungumzia suala hilo, mwanasheria Sessions alisema maelezo yake mbele ya Bunge la Seneti iliyomuidhinisha yalihusu ikiwa kulikuwa na mahusiano yoyote na Warusi kwa niaba ya au kuhusu kampeni za urais, huku akiongeza kuwa yeye na Sergey Kislyak walizungumzia tu siasa za kimataifa.

Hapo ndipo swali lilipoulizwa, Sergey Kislyak ni nani hadi asababishe mjadala mkali ndani ya taifa la Marekani? Ana nguvu gani kisiasa ndani ya nchi yake na nje ya mipaka?

Sergey anatajwa kuwa mwerevu, ndiye mtu wa katikati au tuseme kiungo cha mawasiliano kati ya Putin na Trump. Mawasiliano yake na aliyekuwa mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani, Michael Flynn, yalisababisha Flynn kulazimishwa kujiuzulu mnamo Februari 13, kwa madai ya kumpotosha Makamu wa Rais Mike Pence.

Tukio la kwanza

Balozi Sergey Kislyak alifanya vikao viwili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeff Sessions, iliyosababisha mwanasheria huyo ajitoe kwenye uchunguzi wa endapo Urusi ilihujumu uchaguzi mkuu wa Marekani. Hata hivyo, baada ya vikao hivyo Sessions anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu.

Tukio la pili

Tukio hili limekuja wakati Trump alipohutubia Bunge la Kongresi, ambalo linatajwa kuashiria uhusiano wa ndani kati ya Urusi na urais wake.

“Kislyak alitekeleza mikakati ya Serikali ya Urusi kupenya ndani ya serikali mpya iliyokuwa ikiingia Marekani. Kitu kinachoshangaza ni namna walivyofanikiwa. Jeff Sessions ni kiongozi wa pili baada ya Michael Flynn kuthibitisha kwamba kulikuwapo vikao vilivyofanyika kwa upande wa timu ya kampeni ya Trump na Urusi, kwahiyo halitakuwa jambo la kushangaza kama kutaibuka mambo mengine siku zijazo,” alisema Alina Polyakova, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Dinu Patricia Center, mjini Washington.

SERGEY KISLYAK NI NANI?

Balozi Kislyak, mwenye umri wa miaka 66, alihitimu masomo yake ya shahada ya Uhandisi mjini Moscow, kabla ya kujiunga na Taasisi ya Biashara za Nje na baadaye mwaka 1977 akajiunga na Wizara ya Mambo ya Nje. Mwaka 1985 hadi 1989 alikuwa balozi wa Urusi nchini Marekani, chini ya uongozi wa Mikhail Gorbachev, kipindi ambacho serikali yake ilikuwa imekusudia kudhibiti uuzwaji wa silaha.

Akimzungumzia balozi huyo, Steven Pifer, Mkurugenzi wa Taasisi ya Bookings huko New York na balozi wa zamani wa Marekani alisema: “Sergey alikuwa akifanya kazi ya majadiliano kati ya Marekani na Urusi, akijaribu kuleta mwafaka juu ya udhibiti wa silaha. Sikuwa karibu naye, lakini nilifanya kazi na wanadiplomasia kadhaa wa Urusi wakati huo. Sergey ni mwerevu mno. Anazungumza kwa ufasaha lugha ya Kiingereza, ni muungwana. Kwa wakati huo, aliwakilisha nchi yake hata kama hakuwa na taarifa za kutosha juu ya mambo yanayojadiliwa, kwa mfano suala la kuingilia kijeshi nchini Ukraine. Ni balozi mtiifu kwa nchi yake (Urusi). Nakisia ni mtu wa karibu sana wa Rais Putin, lakini hakuwa miongoni mwa mashushushu.”

Awali Balozi Kislyak aliwahi kuwa mwakilishi wa Urusi katika Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) mwaka 1998, kisha kuwa Naibu waziri wa mambo ya nje mwaka 2003.

Mwaka 2008 aliteuliwa kuwa balozi wa Urusi nchini Marekani, muda mfupi kabla ya Barrack Obama kuingia madarakani. Desemba mwaka jana, Obama alitangaza kuwafukuza nchini mwake maofisa 35 wa Balozi Sergey Kislyak.

Akizungumza kwenye mkutano wake na vyombo vya habari mwaka jana, Balozi Kislyak alisema: “Tupo tayari kuhitimisha vita baridi, lakini bahati mbaya hatupo tayari kuwa na amani baada ya vita hiyo.”

Ripoti zinasema kuwa, Kislyak ni miongoni mwa maofisa wa juu kabisa wa Shirika la Kijasusi la Urusi, SVR, licha ya serikali ya nchi hiyo kukanusha.

Kwa mujibu wa Steven Pifer, ambaye alikuwa balozi wa Marekani nchini Ukraine kati ya mwaka 1998 na 2000:

“Kuhusishwa kwa Balozi Kislyak kuwa jasusi limekuwa jambo linalonisumbua pia. Kila kitu ninachokiona kwake ni mwanadiplomasia kutoka Urusi.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Dinu Patricia Center mjini Washington, Alina Polyakova, anapingana na Steven Pifer, anasema: “Upo uwezekano kuwa Balozi Kislyak ni jasusi mbobezi. Kipindi cha serikali ya USSR ubalozi wao ulifahamika kwa kufanya kazi za ujasusi.

Bado swali la nafasi ya Balozi Kislyak kusababisha viongozi wawili kuwekwa kwenye misukosuko halijajibiwa. Pengine wanaosema balozi huyo ni jasusi wa Urusi wapo sahihi na mtu wa ndani wa Rais Putin. Vilevile wanaopingana na madai hayo kama Michael McFaul ambaye amewahi kuwa balozi wa Marekani nchini Urusi kati ya mwaka 2012 hadi 2014, alisema: “Hebu tuache kuwa wajinga, Kislyak kukutana na Jeff Sessions au Michael Flynn ni kwasababu ya nafasi yake mbele ya Serikali ya Trump. Hiyo ni kazi yake.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles