29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kususa kwawaponza upinzani bungeni

Fredy Azzah, Dodoma



Kitendo cha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kususia kuapishwa kwa wabunge wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao walihama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kujiunga na chama hicho tawala, kumewaponza upinzani baada ya kushindwa kusoma hotuba yao kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo ya Fedha wa Mwaka 2018.

Pia kususa huko, kumewafanya wabunge wawili wa upinzani ambao walikuwa kwenye orodha ya kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kunyimwa nafasi hiyo.

Leo Alhamisi Novemba 15, asubuhi baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuingia kwenye ukumbi wa Bunge, alianza kwa dua kama kawaida baadaye kuwaaapisha wabunge hao James Millya (Simanjiro), Joseph Mkundi (Ukerewe), Pauline Gekul (Babati Mjini) na Ryoba Marwa (Serengeti).

Baada ya kiapo kumalizika, Spika alianza kuita watu wa kumuuliza maswali Waziri Mkuu ambaye jina la kwanza kutajwa lilikuwa la Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko (Chadema) na la pili lilikuwa la Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (Chadema).

Spika alivyotaja jina jina la Matiko ambaye kwa wakati huo hakuwepo kwenye ukumbi wa Bunge ila Lyimo alivyotajwa alisikika akisema “Mheshimiwa Spika nipo…” hata hivyo Ndugai alisema “namfuta kwenye orodha kisha akaendelea na wauliza maswali wengine.

Baada ya kipindi hicho kwisha, aliita hati za kuwasilisha mezani ambapo wa kwanza alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philp Mpango na wa pili alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, ambaye naye aliwasilisha hati yake.

Alivyoita msemaji wa upinzani, hakuwepo kwenye ukumbi hivyo akaita wauliza maswali ya kawaida kuendelea na hata baada ya kipindi hicho ya maswali kwisha, Dk. Mpango alisoma kwa mara ya pili Muswada wa Sheria ya Huduma ndogo ya Fedha wa mwaka 2018 na kufuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene aliyesoma maoni ya amati.

Baada ya pande mbili hizo kusoma hotuba zao, upinzani nao walitaka kusoma na ndipo Spika Ndugai akawaambia jambo hilo ni kinyume cha kanuni kwa sababu hawakuwasilisha hati zao awali kama kanuni zinavyotaka.

Suala hilo lilifanya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), kusimama na kuomba busara ya kiti itumike ili waruhusiwe kusoma hotuba hiyo.

Hata hivyo, baada ya Selasini kuzungumza hayo, Mnadhimu wa Mkuu wa Kambi ya Serikali, Jenista Mhagama, alisimama na kusema ombi la upinzani ni kinyume cha kanuni na Bunge siku zote huendeshwa kwa kanuni.

Kutokana na hali hiyo, Spika Ndugai alihitimisha mjadala huo na kusema lazima kanuni zifuatwe hivyo hotuba hiyo haiwezi kusomwa na badala yake akawaambia wabunge wanaweza kusoma hotuba hiyo wenyewe kwa sababu walishagawiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles