Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD
KUOGELEA ni zoezi muhimu na lenye faida chungu nzima. Japo si kila mmoja wetu huweza kupata nafasi ya kuogelea, ni muhimu kwa wale wenye fursa kuitumia nafasi hiyo ipasavyo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuogelea kunazo faida nyingi ambazo huwezi kuzipata katika mazoezi mengine.
Kuogelea huufanyisha mazoezi mwili mzima
Unapoogelea mikono, miguu na kiwiliwili hufanya kazi kwa pamoja. Unajitahidi kwenda mbele au nyuma huku ukiwa umeelea. Kufanya hivyo huifanya misuli takribani yote katika mwili kufanya kazi.
Hujumuisha aina zote tatu za mazoezi
Tunazifahamu. Mazoezi ya aerobics au cardio, mazoezi ya nguvu au kunyanyua na kuvuta uzito (resistance exercises) na mazoezi ya kulainisha na kunyoosha viungo (Flexibility exercises). Unapooogelea kwa kasi unafanya mazoezi ya aerobics. Haya huimarisha afya ya mapafu na mzunguko wako wa damu ikiwamo afya ya moyo. Unapojisukuma mbele au nyuma unatumia nguvu na misuli. Haya ni mazoezi ya resistance. Unaponyoosha miguu na mikono pamoja na kunyonga kiwiliwili chako unajinyoosha hivyo kunyoosha na kulainisha viungo vyako.
Ni zoezi linaloshauriwa kwa wajawazito
Kutokana na ukinzani wa maji, kuogelea hushauriwa kwa wajawazito. Zoezi hili ni mojawapo ya mazoezi machache yaliyo salama kabisa kwa wajawazito. Kuogelea ni zoezi salama kwa watoto wadogo pia endapo wataogelea chini ya uangalizi.
Husaidiakudhibitimatatizoyaviungo
Mazoezi mengine kama kukimbia huweza kuwa si sawa endapo mtu ana matatizo ya maungio (joints). Ukinzani unaosababishwa na maji wakati wa kuogelea hulinda maungio hivyo kuondoa uwezekano wa madhara.
Huufanyisha ubongo mazoezi
Hii ni faida nyingine kubwa ya kuogelea. Unapoogelea unatumia akili na weledi wa hali ya juu ili kuweza kuelea. Kufanya hivi huufanyisha kazi ubongo kitu ambacho ni muhimu kwa afya ya ubongo. Inashauriwa kuweka ratiba ya kuogelea husussani umri unapokwenda kutokana na ukweli kwamba akili zetu huanza kuchoka katika kipindi hiki.
Hukufanya upumzike
Japo ya kuwa ni mazoezi, hali ya maji (moto, baridi au uvuguvugu) huufanya mwili kupumzika. Hali hii huchukuliwa katika ngozi na kusafirishwa katika sehemu mbalimbali mwilini mwishowe kutafsiriwa katika ubongo. Tafsiri hii ya kibaiolojia husababisha furaha na mapumziko.
Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa kutumia namba 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: