NA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM
IKIWA unakabiliwa na hali ya msongo wa mawazo, unashauriwa kuanza kunywa mara kwa mara maziwa, hasa yatokanayo na wanyama kwani yana uwezo mkubwa wa kupunguza tatizo hilo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, mtaalamu wa lishe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Elizabeth Lyimo, alisema hiyo ni kwa sababu yana ‘utajiri’ wa vitamin D.
“Vitamin D inayopatikana kwenye maziwa husaidia utengenezwaji wa Serotonin, hiki ni kichocheo ambacho kinahusiana na mambo ya ‘mood’, hamu ya kula na kulala,” alisema.
Alisema mwili ukipunguza kirutubisho cha vitamin D wakati mwingine hujihisi mchovu na kukosa raha, hivyo iwapo atakunywa kinywaji hicho kitamsaidia kukabili hali hiyo.
Elizabeth alisema maziwa mazuri zaidi ni yale yatokanayo na wanyama kwani yana protini inayopatikana kwa kiwango cha hali ya juu.
“Maziwa yana virutubisho vingi ambavyo huhitajika mwilini, ni kinywaji kinachohusishwa na afya bora, kwa mfano maziwa ya ng’ombe yana madini ya calcium kwa wingi, ambayo ni muhimu kwa afya ya mifupa, husaidia kuzuia ugonjwa unaoitwa kitaalamu oesteoporosis,” alisema.
Alisema maziwa hayo pia yana vitamin D ambayo husaidia katika kuimarisha afya ya mifupa ya meno.
Mtaalamu huyo alisema maziwa husaidia pia kuimarisha afya ya moyo wa mwanadamu na kumwepusha kupata shinikizo la juu la damu.
“Kwa sababu yana potassium ambayo yenyewe husaidia kutanua mishipa inayokwenda kwenye moyo, hali hiyo husaidia damu kupita kwa urahisi jinsi inavyotakiwa,” alisema.
Alisema protini inayopatikana katika maziwa husaidia pia katika utengenezaji na uimara wa misuli ya mwili.