30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

KUNYIMWA DHAMANA SI ISHARA YA MTUHUMIWA KUKANDAMIZWA

DHAMANA ni ruhusa ya kuwa huru anayoweza kupewa mshtakiwa wakati uchunguzi wa kosa lake unaendelea au shauri lake likiendelea kusikilizwa mahakamani, au akisubiri uamuzi wa rufaa yake.

 

DHAMANA YA POLISI

Dhamana ya polisi ni ruhusa anayoweza kupewa mtuhumiwa wakati shauri lake likiendelea kuchunguzwa na polisi. Hii hutolewa bure, hakuna malipo yoyote yanayotakiwa kutolewa ili mtuhumiwa au mshtakiwa akubaliwe dhamana.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20, kifungu cha 64, na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 kifungu cha 31, zimeainisha dhamana ya polisi, utaratibu wake na masharti.

Dhamana ya polisi hutolewa na mkuu wa kituo cha polisi ambako mtuhumiwa ameshikiliwa.

Jambo la kuzingatia katika dhamana ya polisi ni mtuhumiwa anapaswa kuomba apewe dhamana na kutimiza vigezo, masharti na taratibu zote kama zilivyoainishwa kwa mujibu wa sheria.

Vigezo vya kuzingatia kabla ya mtuhumiwa kupewa dhamana ni pamoja na polisi kujiridhisha kwamba mtuhumiwa atatimiza masharti atakayopewa, ikiwamo kufika siku na saa atakayoamriwa. Kujua makazi ya mtuhumiwa, kuwafahamu ndugu na jamaa wa mtuhumiwa, kufahamu ajira  yake/zao na ikibidi hali ya maisha ya mtuhumiwa na familia yake.

Pia kufuatilia kama mtuhumiwa hana kumbukumbu za kihalifu, mazingira ambayo kosa limefanyika, ukubwa wa kosa na uzito wa ushahidi dhidi ya mtuhumiwa, taarifa nyingine na uwezekanao wa mtuhumiwa kutokutii masharti ya dhamana nayo yanazingatiwa kabla ya kutoa dhamana kwa mtuhumiwa.

Dhamana ya polisi hutolewa kutokana na umuhimu wa mtuhumiwa kuwa nje kwa dhamana, ili aweze kujiandaa kukabiliana na tuhuma zinazomkabili kabla ya kufikishwa mahakamani mfano, kupata msaada wa kisheria.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 67  kinaeleza, mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa polisi anaweza kukataliwa maombi yake ya dhamana.

Yapo makosa ambayo ikiwa mtuhumiwa anashitakiwa nayo hawezi kupewa dhamana ya polisi kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Kifungu cha  148, kifungu kidogo cha 5 (i), (ii) ambayo ni pamoja na; kosa la kuua kwa kukusudia; uhaini; unyang’anyi kwa kutumia silaha; ugaidi; kunajisi na kusafirisha dawa za kulevya.

Pia mtuhumiwa anaweza kunyimwa dhamana hata kama kosa alilolifanya linaweza kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria kutokana na sababu zifuatazo: Iwapo  mtuhumiwa alishawahi kupewa dhamana akaikiuka; kwa mahitaji ya  usalama wa mtuhumiwa mwenyewe. Wapo watuhumiwa ambao kutokana na makosa waliyoyafanya, kuonekana kwao jamii inaweza kuwadhuru au hata wakati mwingine kuwaua.

Pia mtuhumiwa anaweza asipewe dhamana kwa usalama wa jamii, kwamba kwa kumpa dhamana mtuhumiwa, anaweza kwenda kuidhuru jamii; kuchelea kumwachia nafasi ya kuvuruga upelelezi, sababu nyingine kama atakavyoona mkuu wa kituo.

Dhamana ya mtuhumiwa inaweza kufutwa na mkuu wa kituo, chini ya kifungu cha 68 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai endapo itabainika mtuhumiwa anapanga mipango ya kutoroka ama kwa makusudi anakiuka au yupo karibu kukiuka masharti ya dhamana.

Endapo mtuhumiwa atakiuka dhamana inayotolewa na polisi, atapewa adhabu kali kwa mujibu wa kifungu cha 69 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinatoa adhabu kali kwa mtuhumiwa na mdhamini/wadhamini wanapokiuka masharti ya dhamana waliyopewa.

Pamoja na kuwa dhamana ni haki ya mtuhumiwa, ni vema kufahamu kuwa si kila mtuhumiwa anaweza kupatiwa dhamana kama ilivyoainishwa huko juu kutokana na sababu za kisheria ama za kiusalama kama ambavyo mkuu wa kituo husika ataona inafaa.

Ni vema kufahamu kuwa kunyimwa dhamana si ishara ya kukandamizwa ama kuonewa na ni vizuri kuomba ufafanuzi zaidi kutoka kwa mkuu wa kituo ili uweze kufahamu sababu zilizosababisha mtuhumiwa wako anyimwe dhamana.

Lakini pia ni vema kwa watuhumiwa ambao wamepewa dhamana kuzingatia na kutimiza masharti ya dhamana ili kuepuka adhabu ambazo zinaweza kutolewa dhidi yao na hatimaye kupoteza haki hiyo ya msingi kikatiba.

Mtuhumiwa kupewa dhamana ni haki yake kikatiba isipokuwa asivunje sheria za nchi, na katika kuzingatia utawala wa kisheria na haki za binadamu ndipo polisi huwajibika kutoa dhamana kwa watuhumiwa, wakati mtuhumiwa naye anawajibika kutekeleza wajibu wake wa kufuata na kutimiza vigezo na masharti ya dhamana.

Makala hii imeandaliwa na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

S.L.P. 9141,

DAR ES SALAAM.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles