27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KUNA UMUHIMU KUUNDA TAASISI RASMI YA DIASPORA

Rais Dk. John Magufuli
Rais Dk. John Magufuli

NA TENGO KILUMANGA,

IFUNGULIWE Taasisi ya Diaspora, kuna umuhimu na iwepo miundombinu ya kukusanya habari na wako wangapi duniani na vizazi vyao. Katika ukusanyaji wa data kama hizi kutakuwapo pia na uwezo wa kufahamu wapi tutapata ujuzi au utaalamu katika masuala ya maendeleo yanayogusia Taifa letu, mikoa, jimbo na hata watu binafsi.

Kuwe na taasisi yake pekee chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Chuo kikuu na hata Usalama wa Taifa, iboreshwe na kupatiwa uwezo wa kufanya utafiti na uchunguzi madhbuti wa kuweza kufahamu nani ni Diaspora, wanaishi wapi, wana watoto wangapi, wajukuu na kadhalika.

Hii itatuwezesha kama nchi kupata picha kamili ya ukubwa wa Diaspora wetu, uwezo na taaluma zao. Hatuna tena haja ya kusaka watu ambao wana ujuzi wa aina fulani katika masuala kadhaa ambayo yanahusu nchi yetu, ni kuingia katika mtandao na hifadhi data ambayo ipo chini ya taasisi ya Diaspora. Kwa usalama wetu ni muhimu pia kutafuta watu ambao wataweza kutumiwa katika masuala ambayo yatahitaji utaalamu wa namna fulani.  Iwe lugha, au kufahamu fikra na utamaduni wa wenzetu kwenye masuala ya biashara na utamaduni wao kabla ya kuingia katika mikataba mikubwa na mizito.

Kwa sababu Diaspora ni jumuiya ya watu wenye uchumi mzuri, yaani kwa Tanzania uchumi wa kati na daraja la chini juu basi kufahamu wapi walipo na kuwashughulisha katika maendeleo ya nchi yao hatutahitaji tena kuomba wafadhili wa kigeni au Serikali za kigeni watupatie fedha kufanikisha mahitaji ya nchi, mkoa,  jimbo, au wilaya kwenye sehemu  tofauti ya mahitaji yetu. Iwe afya (madaktari), iwe kwenye ujenzi au miradi mikubwa mikubwa na kadhalika, uwezo utakuwapo. Itachukua muda kujenga asasi kama hiyo lakini msingi utakuwapo.

Kwa hali na kasi jinsi nchi inavyoendelea kuna umuhimu mkubwa kuupa  muundombinu huu kipaumbele na kuwaza kujenga. Tanzania inavyokua na pia mahitaji ya wataalamu yapo na kama tukiweza kufunguka macho na kuona kwamba watoto wanasomeshwa nje na wazazi wao ambao wanaishi nje ya Tanzania taasisi kama hizi zinaweza kuwa mwongozo kwa wazazi na watoto kwa fursa ambazo zinajitokeza nyumbani na wakati nchi inajenga uwezo wake.

Ukamilifu wa malengo ya taasisi hiyo itahitaji nidhamu kubwa na watu kujitolea sana, sio kazi rahisi. Kuna msemo kule ”undambani” unasema, ”…Ya Waisraeli, waachie Waisraeli lakini mafanikio yao ni ya kuiga..” Wandamba kwa misemo kama hiyo hapo ni kwao.

Na kuambatanisha na kuunganisha na chuo kikuu ni kwa sababu ya miundo na mifumo ya taasisi hiyo itahitaji kuufuatilia kwa makini ili tuweze kuelewa changamoto zinazojitokeza, kuweka kumbukumbu na kuhifadhi utaratibu uliofanyika kupata suluhisho katika masuala magumu. Hii yote pia ni kwa sababu ya vizazi vijavyo na wasomi ambao wataona makosa na mafanikio ya kuunda taasisi kama hii.

Kwa jamii ya Diaspora kuwa na imani na jamii za Tanzania kuwa na imani kwenye taasisi kama hii lazima kuwapo na nidhamu na pia kazi ifanyike kwa uwazi. Katika mfumo huu utatuwezesha kutuma na kupokea fedha zitazohitajika katika kutengeneza mazingira fulani Tanzania. Kwa mfano kama hakuna fedha za kuwasomesha watoto waliofaulu vizuri lakini wazazi hawana uwezo wa kuwapeleka shule, kupitia mfumo huu fedha zinaweza kukusanywa na kupelekwa Tanzania. Kila mtu kwa uwezo wake, lakini bila imani kwa chombo kama hiki kazi basi itakuwa ya bure. Kwa hiyo kuna umuhimu wa kujenga imani ya taasisi yetu. Haitakuwa tena kazi ya mtu mmoja, itakuwa ni kazi ya wote.

Katika Usalama wa Taifa pia ni muhimu sana kuwapo na utaratibu kwani si wote wenye nia nzuri na sio wengi wenye nia mbaya. Kwa hiyo kunahitaji kuwa na umakini kwa kufahamu nani ni nani na ni watoto wa Mtanzania au Watanzania wepi. Hakuna ubaya katika kuchunguza na kuhifadhi habari ambazo baadaye zitaweza kusaidia kufafanua na kujibu masuala muhimu na njeti.

Kutokana na kasi ya maendeleo Tanzania kunahitajika mifumo ya kijamii kama taasisi au shirika rasmi la Diaspora. Kuna umuhimu mzito na hapa sio kwamba ni kitu cha kupita, hapa ni kuelewa kwamba kumejitokeza haja kwa pande zote kutengeneza hili daraja la mawasiliano na haja ya kuunda taasisi ya kudumu kubeba masuala mazito na haja na mahitaji za jamii na nchi.

Jamii zetu zinakuwa na pande zote tunahitajiana, Diaspora wanahitaji kuunganishwa na asili yao na kupata fursa ya kuchangia katika maendeleo ya nchi yao na nchi inahitaji, ujuzi, uwezo na werevu wa Diaspora katika jamii wanayoishi.

Tukiweza kuiga na kuchukua yale ambayo yana manufaa kwa jamii zetu nchini, yale ambayo hayapingani na utamaduni wetu basi Tanzania na kasi ambayo ilikuwapo na ipo sana. Tanzania itakuwa nchi ambayo inatoa misaada, hasa kwa nchi jirani. Kiusalama tumekaa vizuri sana na miongoni mwa nchi ambazo zina ushawishi mkubwa sana kanda hizo za Afrika Mashariki na Kusini

Ukishafahamu haya yote, basi iliyobaki ni kasi tu ya kutekeleza uliyoyalenga..

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles