32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUMUOMBA MTOTO MSAMAHA SI KUJISHUSHA

NA AZIZA MASOUD,

NENO ‘samahani’ lina maana kubwa sana, hasa unapolitoa katika mazingira ambayo unakuwa umemuumiza ama kumkwaza mtu kwa namna moja ama nyingine.

Kuomba msamaha unapokosa kunakuwa na tafsiri kubwa ya kumjali, kumheshimu na kuona umuhimu wake kwako.

Mara nyingi watoto hujifunza tabia ndogondogo kama za kuomba msamaha kupitia wazazi wao ambao wanawaona wakifanya hivyo inapotokea wamekosea.

Watoto waliolelewa vizuri kwa maana ya kujifunza mambo mema wanapokosea wanakuwa wepesi sana kuomba msamaha, hivyo mzazi ama mtu yeyote aliyekosewa anakuwa na amani ya moyo.

Utaratibu huo pia unapaswa kufanywa na wazazi wanapowakosea watoto wao, ni vema ufahamu kwamba kuwa mzazi si kwamba unakuwa malaika na kuwa sawa kwa kila jambo.

Kama mzazi unapaswa kufahamu unaweza ukafanya ama kuongea kitu kibaya ambacho kinaweza kumkwaza mtoto wako, katika maisha kila binadamu aliye hai lazima akosee.

Wapo wazazi ambao wanadhani  ni kosa kumuomba mtoto msamaha, wengine wanadhani neno samahani linaweza kushusha hadhi na nguvu aliyonayo kwa mtoto, hasa katika kumuadhibu anapokosea, jambo ambalo si kweli.

Wapo ambao pia wanadhani kumuomba msamaha mtu uliyemzidi umri ama kukubali makosa uliyoyatenda si sehemu ya tamaduni za Afrika, hivyo huamua kuacha alilolifanya lipite kimya kimya kwa sababu tu imezoeleka siku zote mtoto anapokosea anasababisha mwenyewe.

Vipo vitu ambavyo kama wazazi tunafanya vinaweza vikachangia kumuingiza mtoto katika maumivu makali ya kimwili ama kisaikolojia na kusababisha mtoto asiwe na amani moyoni.

Yanapotokea mambo kama hayo, ni vema mzazi ukamuomba msamaha mtoto, msamaha kwanza unamfanya mtoto kuwa na furaha, pia anajiona ni mtu mwenye thamani kubwa kwako na kumjali kama walivyo watu wengine.

Mzazi akikosea na kuomba msamaha si kwamba ni  ishara ya udhaifu, isipokuwa ni njia ya kuwafundisha watoto kuomba radhi wanapokosea.

Kama uatendelea kuwa na msimamo wa kutoamini kama umekosea hauwezi kukusaidia kusahihisha makosa  yako.

Kuzuia tatizo kwa kudanganya kunaweza kukazaa tatizo kubwa, kuna vitu ambavyo huwezi kujifunza bila kufanya makosa.

Watoto wanapoombwa msamaha  wanakuwa na furaha na amani ndani ya moyo ambayo wanashindwa kuielezea mbele ya mtu.

Wazazi tujifunze kuwaomba msamaha watoto wetu ili waweze kuwa na amani na kujihisi wenye furaha kila wanapokosewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles