THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
UONGOZI wa Yanga, umetaja viingilio vya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika kati ya timu hiyo na Pyramids ya Misri, unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 27 mwaka huu, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku cha chini kikiwa Sh10,000.
Yanga ilianguakia michuano hiyo, baada ya kutupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika na timu za Zesco ya Zambia, kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1.
Mchezo wa kwanza uliochezw Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1 na ziliporudiana mjini Ndola, Zambia, Yanga ililala kwa mabao 2-1.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fredrick Mwakalebela alisema, wanaamini viingilio vitawawezesha mashabiki wengi wa soka kujitokeza uwanjani siku hiyo na kuujaza uwanja.
“Viingilio katika mchezo huu kwa VIP kitakuwa Sh 50,000, Royal ni Sh 70,000 na kawaida kitakuwani Sh.10,000, tunaamini mashabiki watajitokeza kwa wingi kwa ajili ya kutoa hamasa kwa wachezaji wetu,” alisema.
Wakati huo huo alisema kikosi chao kinatarajia kuondoka leo jijini hapa kwenda Mwanza kikiwa na wachezaji 24.
Kuhusu wachezaji wao wawili, Feisal Salum na Abdulazizi Makame waliosafiri kwenda Sudan na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambacho jana kilitarajiwa kuumana na wenyeji wao, katika mchezo wa kusaka tiketi ya fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani(Chan), alisema wataungana na wenzao punde baada ya kurejea nchini.
Mwakalebela alisema wameamua kutumia Uwanja wa CCM Kirumba ili kupata muda mzuri wa matayarisho ya mchezo wao mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbao, unaotarajiwa kuchezwa Oktoba 22.
“ Tuna mchezo wa Ligi Kuu na Mbao Oktoba 22, hili ndilo limetushawishi tukacheze Mwanza ili kuepuka usumbufu wa kusafiri kutoka Dar es Salaam,”alisema Mwakalebela na kuongeza.
“Wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa Mohammed Issa ‘Banka’ na Issa Bigirimana ambao bado ni majeruhi, hawa ndio hawatakuwa kwenye msafara huo, bado tunaenda na kikosi kipana kwa sababu tunakabiliwa na mechi mbili Mwanza,” alisema.
Mwakalebela alisema tayari benchi lao la ufundi linazo taarifa za kutosha kuhusu wapinzani wao Pyramid, hivyo wataingia dimbani wakiwa wamejipanga vizuri kwa ajili ya kusaka ushindi.