Na Asha Bani, Mtanzania Digital
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro amesema ikifika Januari mwakani kila mtoto awe amesajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa.
Dk.Ndumbaro aliyasema hayo leo jijini Dar as Salaam katika viwanja vya shule ya msingi Gongo la Mboto wakati wa maadhimisho ya tano ya siku ya Matukio Muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika (CVRS).
Dk. Ndumbaro alisema ni lazima na muhimu kila mtoto awe amesajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa ambacho kitatumima kuanzia elimu ya chekechea ,shule ya msingi na chuo kikuu.
Alisema hata ikitokea mtoto akaenda kuandikishwa shule bila kuwa na cheti ni jukumu la mwalimu Mkuu kuandikisha majina yao na kuyapeleka kwa DAS ili aweze kupata cheti cha kuzaliwa.
“Kama mzazi atashindwa kumpatia mtoto cheti cha kuzaliwa atakua anamnyima haki zake za msingi na haki za mtoto,”alisema Dk.Ndumbaro.
Aliongeza kwa kusema kuwa hali ya usajili kwa upande wa Tanzania ni nzuri kutokana kupanda kwa takwimu zake.
Dk.Ndumbaro alisema mafanikio hayo pia yanatokana na mpango wa Usajili wa Watoto walio chini ya Umri wa Miaka Mitano ambapo hadi sasa bado asilimia 35 tu.
Alisema tayari Mikoa 23 imefanikiwa na kuonesha mafanikio ya zaidi ya watoto Milioni 7.7 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa bila ya malipo ya ada na hivyo kuongeza asilimia ya watoto waliosajiliwa nchini kufika 65 kutoka asilimia 13 ya mwaka 2012.
Dk. Ndumbaro amesema Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA,) wanaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha ifikapo 2025 watoto wote walio na umri wa chini ya miaka 5 wanasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Naye Kabidhi Wasii Mkuu Angela Anatory amesema maadhimisho hayo ya tano ya siku ya Usajili wa Matukio muhimu ya Binadamu na Takwimu Barani Afrika imelenga kujenga ufahamu kwa wananchi juu ya kumbukumbu muhimu pamoja na matukio muhimu ya vizazi, vifo, talaka, ndoa pamoja na kuasili watoto.
Amesema, RITA ikiwa taasisi pekee inayosimamia matukio ya Usajili wamekuwa wanatekeleza usajili wa matukio hayo pamoja na kubuni programu za maboresho ya kuongeza kasi na kupanua wigo wa utoaji huduma.
Alisema RITA wamefanikiwa na kuongea mikoa mingine mitatu ikiwemo Kagera,Kigoma na Katavi leo ni kufanikisha kwa asilimia 100 mikoa yote ya Tanzania.
Amesema Wakala itaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo kuweka mfumo wa Ndoa utakaowawezesha kutoa leseni kwa wafungisha ndoa pamoja na kupata takwimu za kitengo hicho
Naye Naibu Mkurugenzi mkaazi wa UNICEF Ousmane Niang ameimwagia sifa Tanzania kwa kuweza kuifikia idadi kuwa ya watoto kuwasajili na kuwapa vyeti katika mikoa 23 ya Tanzania na ni mfano mkubwa wa kuigwa kwa nchi nyingine Afrika.
Naye Mwakilishi wa Serikali ya Canada . Helen Fytche amesema kila mwananchi ana haki ya kusajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa na hivyo Serikali yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo.
Naye mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani (UNFPA ,) Ramadhan Hangwa amesema wamekuwa wakiboresha mifumo ya kupata cheti cha kuzaliwa kutoka miezi miwili hadi saa 24 na Zanzibar inatekeleza hilo.
Amesema, wadau waende sambamba na uboreshaji wa Usajili na ukusanyaji wa matukio ya binadamu ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ulimwenguni.
Kwa upande wake Mbunge wa Ukonga Jerry Slaa amesema suala la mirathi liangaliwe ili kuokoa familia hasa akina Mama na watoto na kuwataka wananchi wa Ukonga kujitokeza kwa wingi siku ya Agosti 23 ili wahesabiwe kwa maendeleo endelevu.
Wadau wengine waliohudhuria siku hiyo ni pamoja na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma TAMISEMI, Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA), Ofisi ya Taifa ya Takwimu( NBS), Kampuni ya mawasiliano ya Tigo na wabunge mbalimbali.