NA EVANS MAGEGE – DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kitafanya uchaguzi wake mkuu wa viongozi Machi 18.
Viongozi watakaoibuka washindi katika uchaguzi huo wanatakuwa na jukumu la kukiongoza chama hicho kwa mwaka mmoja kwa mujibu wa taratibu zake.
Urais wa chama hicho, ndio unaonekana kugusa hisia za wengi na tayari majina matano yamepitishwa kuwania nafasi hiyo.
Majina hayo ni Francis Stola, Lawrance Masha, Victoria Mandali, Tundu Lissu na Godwin Mwapongo.
Gazeti hili limeanzisha kolamu maalumu ambayo kila mgombea wa nafasi hiyo atachambuliwa na leo tunaanza na Lissu.
LISSU NI NANI?
Ni wakili anayefanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amejipambanua vyema masikioni na machoni mwa watu kupitia taaluma yake ya sheria na siasa za upinzani.
Ndani ya duru za siasa, mbali na jukumu la kuwa mwanasheria mkuu wa Chadema, pia anatumikia nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Kwa nafasi ya kisiasa katika jamii, anatumikia muhula wa pili wa uwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lissu alizaliwa Januari 20, 1968 na kusoma Shule ya Msingi Maambe mwaka 1976-1982.
Alipata elimu ya sekondari mwaka 1987-1989 katika Shule ya Galanos na mwaka 1983-1986 aliendelea na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Iliboru.
Mwaka 1991-1994 alisoma masomo ya sheria kwa ngazi ya shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Baada ya kuhitimu ngazi hiyo, mwaka 1995-1996, aliendelea na masomo ya sheria kwa ngazi ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Warwick huko nchini Uingereza.
KWA NINI ANAGOMBEA URAIS?
Sababu za Lissu kuwania urais wa TLS amezitanabaisha kupitia ujumbe wake alioutuma katika mitandao ya kijamii katikati ya wiki hii.
Kwa uthibitisho wake baada ya MTANZANIA Jumapili kumuuliza kama kaandika ujumbe huo, alikiri kuwa ndiye aliyeandika.
Kupitia ujumbe huo, anasema kwamba ana misimamo thabiti ya kutetea utawala wa sheria, utawala wa kikatiba na utawala bora.
“Kazi yangu bungeni imejengeka katika misingi hiyo. Kama nikichaguliwa kuwa Rais wa TLS, huo ndiyo utakuwa msimamo wangu. Kwa bahati nzuri, misingi ninayoisimamia ndiyo pia malengo ya kisheria ya TLS kwa mujibu wa sheria iliyoianzisha, yaani Sheria ya Chama cha Mawakili wa Tanzania, Sura ya 307,” anatanabaisha.
Anaendelea kusema kwamba kwa miaka mingi, TLS imeacha kusimamia misingi hiyo kwa hofu ya kuwaudhi watawala.
“Kumekuwa na dhana kwamba tukiwa wapole basi mambo yetu yanaenda vizuri. Mambo ya nchi yetu hayataenda vizuri kwa sababu ya ukimya wa TLS. Na wala mambo ya mawakili walio wengi hayajaenda vizuri licha ya ukimya huu. Nikiwa wa TLS ukimya huu utaisha,” anasema.
Katika maelezo yake hayo, anafafanua mazingira ya kazi kwa kusema kazi ya Rais wa TLS si ya muda wote.
Anasema kwamba hadhani kama Rais wa TLS ana ofisi ya kudumu katika ofisi za makao makuu ya chama hicho.
“Hata kazi ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema si ya muda wote. Sina ofisi Makao Makuu ya Chadema. Kazi ya ubunge ni kazi ya muda wote, lakini inaweza kunipa nafasi ya kutekeleza majukumu mengine. Nje ya vikao vya Bunge na kamati, mimi ndiye ninayepanga ratiba yangu. Kwa sababu hiyo, licha ya majukumu mengi niliyonayo, ninaamini nitapata muda wa kutekeleza majukumu ya Rais wa TLS.
“Hofu ya baadhi sio Chadema, ni hofu kwamba wanasheria wakiamka katika umoja wao wana nguvu kubwa ajabu kwa sababu ya unyeti wa nafasi waliyonayo kisiasa na kijamii. Kwa hiyo kwenye uchaguzi huu wa TLS, chaguo lililopo mbele ya wapigakura sio chaguo la Chadema au CCM, bali ni chaguo kati ya TLS inayotambua wajibu huo,” anasema.