30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

ORODHA YA MAKONDA YAMPA MTIHANI RPC SIRRO

Na AGATHA CHARLES,

IKIWA ni zaidi ya wiki mbili tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atangaze kwa mara ya kwanza orodha ya majina ya watu aliodai kushiriki ama katika matumizi au biashara ya dawa za kulevya, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro, bado anaonekana kuhangaika kukamilisha kazi ya uchunguzi, ikiwa ni pamoja na kuwahoji, kuwachukulia hatua au kuwaachia watuhumiwa.

Miongoni mwa watuhumiwa waliotajwa katika orodha hiyo na ambao wanaonekana kuumiza kichwa polisi, ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ambaye tangu ametajwa katika orodha hiyo siku 11 zilizopita, amegoma kuripoti polisi akitaka utaratibu ufuatwe.

Jambo ambalo linaonekana kumpa mtihani Sirro katika kukamilisha kazi yake hiyo ni msimamo binafsi wa Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wa kufungua kesi namba 1 ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya Makonda, huku zikiwapo taarifa za Jeshi la Polisi kupelekewa wito wa kuitwa mahakamani keshokutwa.

Mtihani mwingine unaoonekana kumkabili Sirro ni katazo la Spika wa Bunge, Job Ndugai la polisi kukamata wabunge pasipo kufuata utaratibu wa kibunge.

Jana, Kamanda Sirro aliitisha mkutano wa waandishi wa habari, kueleza juhudi za kuendelea kuwakamata na kuwachunguza wale wote waliotajwa katika orodha mbili za Makonda.

Katika mkutano huo, Sirro alimtaka Mbowe asitafute namna nyingine bali afike Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (Central) kuhojiwa, vinginevyo atakamatwa.

Wakati Sirro akitoa kauli hiyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili jana kutoka kwa chanzo cha uhakika kilicho karibu na Mbowe, zilisema mwanasiasa huyo hayuko tayari kwenda polisi kwa sababu ya kesi ambayo ameifungua Mahakama Kuu.

Pamoja na hilo, Sirro alisisitiza wote waliotajwa katika orodha hizo kufika kituoni hapo mara moja, huku akilitaja jina la Mbowe tu kati ya majina 65 yaliyotajwa katika orodha ya pili.

“Bado nasisitiza kuwa waje. Mbowe kupitia kwa baadhi ya viongozi, alijulisha kwamba Februari 15, mwaka huu, siku ya Jumatano angekuja kuripoti Central Police, sisi tulikubaliana na ile taarifa yake, lakini jambo la ajabu na la kusikitisha hiyo tarehe hakuonekana.

“Mbaya zaidi jana (juzi) tumejitahidi kumtafuta hapatikani, tulikwenda nyumbani kwake hakupatikana, tulikwenda mahali anakoishi sasa, pia hakupatikana,” alisema Sirro.

Alisema jeshi hilo linamheshimu Mbowe kutokana na kuwa kiongozi mkubwa wa chama cha siasa, hivyo linamhitaji afike mwenyewe kituoni hapo kwa kuwa pia alisikika bungeni akipiga vita dawa za kulevya.

“Mimi nimwambie tu Mbowe tunamheshimu sana, asitafute namna nyingine, tunamhitaji kwa ajili ya kumhoji kutokana na hizi tuhuma za dawa za kulevya. Sitegemei kiongozi kama yeye tunayemheshimu awe mtu wa kutafutwa, najua anajua kama tunamtafuta na ndiyo maana tumejitahidi sana kumpigia simu akawa hapatikani na baadaye akazima simu.

“Kwa hiyo ni rai yangu kwamba akisikia huu ujumbe ninaousema, Jumatatu (kesho) atafika ofisini kwangu tuweze kumhoji. Other ways, sioni kama kuna namna nyingine ya kuzuia sisi kumuhoji kama Jeshi la Polisi, inanishangaza kwanini anataka tuvutane,” alisema Sirro.

Alisema Mbowe asiporipoti kituoni hapo kesho, sheria iko pale pale na hakuna aliye juu ya sheria na kwamba lazima watamkamata na kufanya naye mahojiano.

Mbowe alitajwa katika sakata la dawa za kulevya Februari 8, mwaka huu katika orodha ya majina mengine 65 ambayo yalitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda, wakitakiwa kuripoti polisi.

Akizungumzia kuhusu wito huo wa polisi, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema: “Sirro amsubiri Mbowe Mahakama Kuu, kesi ya kikatiba namba moja iliyofunguliwa inaanza kusikilizwa Jumamne ijayo, hiyo ndiyo kesi ya msingi na huko ndiko mahakama itasema nani yuko sahihi kisheria. Mambo hayo ya kisheria yanaamriwa mahakamani, Mbowe yupo mjini hapa na anaendelea na majukumu yake wala hajajificha.”

Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi limesema linatarajia kuwafikisha mahakamani kesho watu watatu akiwamo Agness Gelard ‘Masogange’, Rashid Said ‘Chid Mapenzi’ na mfanyabiashara wa kuuza magari, Wallid Nasher (34) baada ya kubainika kutumia dawa za kulevya.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Kamishna Sirro alionyesha baadhi ya vielelezo kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambayo ni majibu ya vipimo vitakavyopelekwa kama ushahidi mahakamani katika kesi za dawa za kulevya.

“Tunaendelea vizuri na operesheni za dawa za kulevya na watuhumiwa wafuatao; Agness Gelard (Masogange), Rashid Said maarufu kama Chid Mapenzi na mfanyabiashara wa kuuza magari, Wallid Nasher, hawa Jumatatu (kesho) tutawapeleka  mahakamani kwa tuhuma za kupatikana na madawa. Kuna wengine ambao ni 17 watakwenda ili kutoa kiapo kwa ajili ya kuwa chini ya uangalizi wa polisi,” alisema Kamishna Sirro.

Kuhusu wale ambao hawajaripoti polisi wakiwamo wasanii wa muziki wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee na Herry Sameer ‘Mr Blue’, alisema bado wanaendelea kuwafuatilia na kuwataka kuitika wito wa Jeshi la Polisi mara moja.

Alisema watuhumiwa 31 ambao wamo katika orodha ya watu 65 walikamatwa na kwamba baadhi walipatikana na makosa ya kutumia dawa hizo.

Katika orodha hiyo alimtaja mfanyabiashara huyo wa kuuza magari, Wallid, mkazi wa Ocean Road, Mtaa wa Chimala ambaye alisema alikamatwa akiwa ofisini kwake jengo la Victory Plaza akiwa na unga unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya kiasi cha gramu 95.

Kamishna Sirro alisema pia jeshi hilo lilipata taarifa kuwa wapo watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaojaribu kukimbilia Zanzibar na kwamba baadhi walifukuzana na polisi na kuwakamata wakiwa visiwani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles