Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amewataka Wakala wa Barabara Nchini (TANROAD), kuhakikisha wanakuja na mpango wa muda mrefu wa kutengeneza njia sahihi ya maji.
Pia amewataka kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye kingo za madaraja hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha nchini.
Maagizo hayo ameyatoa leo Januari 22,2024 jijini Dar es Salaam wakati akikagua miundombinu katika maeneo mbalimbali yaliyoathirika na mvua hizo ikiwamo Jangwani, daraja la Kunduchi na mengine.
Amesema TANROAD wafanye ukaguzi huo ili waweze kuweka alama za tahadhari kuwasaidia wananchi pindi athari zinapotokea.
“Nyinyi TANROAD ndio wenye kujua changamoto na viashiria vya hatari, sasa ni vyema muwe mnafanya ukaguzi ili mtoe tahadhari ya haraka kwa wananchi kuepuka madhara kama haya yaliyojitokeza,” amesema Mhandisi Kasekenya.
Aidha rai kwa wananchi kuchukua tahadhari wanapopita katika maeneo ya madaraja, wakiona maji mengi na sehemu ya ardhi haionekani wasipite.
“Niipongeze sana serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake pindi Mamlaka ya Hali ya Hewa(TMA) ilipotangaza uwepo wa mvua hizi kubwa alitoa maelekezo kwa wizara zote kujiandaa na kukabiliana na changamoto zozote zitakazotokea ndio maana unaona changamoto hii ilipotokea wenzetu TANROAD makao makuu na mkoa wameshughulikia hizi changamoto kwa haraka,”amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Saad Mtambule ameipongeza TANROAD na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) kwa jitihada kubwa waliyoofanya za kurudisha huduma ya usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mhandisi Suzana Lukasi amesema mvua imeharibu miundombinu ya madaraja na barabara lakini juhudi kubwa imefanyika ya kuhakikisha miundombinu hiyo inarejeshwa kwa wakati.
“Mvua hizi zilizonyesha zimesababisha uharibifu mkubwa lakini tumejitahidi kuhakikisha miundombinu hiyo tunairekebisha na sasa tumefungua njia zinapitika huku ukarabati mwingine unaendelea,”amesema Mhandisi Suzana.