Na FARAJA MASINDE -DAR ES SALAAM
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), imemfikisha mahakamani mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Saed Kubenea baada ya kupatikana na makosa mawili, likiwamo la kuingia nchini kinyume na sheria za uhamiaji na kuingiza fedha bila kutoa tamko.
Taarifa iliyotolewa jana na DPP Biswalo Mganga iliyataja mashtaka mawili yanayomkabili Kubenea kuwa ni kuingia nchini kinyume na Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 Marejeo ya mwaka 2016 na kuingiza nchini fedha za kigeni bila kutoa tamko kinyume na kanuni za utoaji tamko la fedha mpakani za mwaka 2016.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Septemba 5 mwaka huu, Jeshi la Polisi lilimkamata mbunge huyo wa zamani wa Ubungo akiwa katika gari la abiria lenye namba ya usajili T 645 DKR akitokea kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo la Namanga akielekea Arusha mjini.
“Mara baada ya upekuzi, mtuhumiwa huyo alikutwa pamoja na vitu vingine, Dola za Marekani 8,000, Sh za Kenya 491,700, Sh za Tanzania 71,000, tiketi ya basi la Super Couch lenye namba ya usajili KCP 4230 ya Septemba 5, mwaka huu kutoka Nairobi, Kenya kwenda Namanga, ‘Memorandum of Understanding’ kati ya Hali-Halisi (Tanzania) na Buni Media Limited (Kenya).
“Pia alikutwa na risiti ya malipo ya hoteli iitwayo After 40 Hotels Limited iliyopo Nairobi, Kenya yenye jina la Kubenea Saed Ahmed kama mgeni kuanzia Septemba 3 hadi 5, mwaka huu na pasi yake ya kusafiria (Passport),” ilisema taarifa hiyo.
DPP Mganga alisema kuwa mara baada ya kukamatwa, mtuhumiwa alieleza kuwa alifika mkoani Arusha Septemba 2, mwaka huu akitokea Dar es Salaam na kufikia katika hoteli iliyopo Arusha mjini.
“Alieleza zaidi kuwa Septemba 3, mwaka huu alienda kulala kwa kaka yake na Septemba 4 alienda Namanga na kupokea fedha taslimu tajwa hapo juu kutoka kwa raia wa Kenya,” alisema Mganga.
Alisema hata hivyo, mara baada ya kupitia ushahidi uliokusanywa, alibaini kuwa mtuhumiwa hakufikia katika hoteli aliyoitaja Arusha mjini, wala kulala kwa kaka yake kama alivyoeleza.
Mganga alisema pia mtuhumiwa tajwa alivuka mpaka usio rasmi na kuelekea Nairobi nchini Kenya na kisha kurejea nchini Tanzania bila kutumia mpaka rasmi Septemba 5, mwaka huu.
“Aliingiza nchini fedha za kigeni bila kutoa tamko rasmi la kisheria kinyume na masharti ya kanuni za the Anti-Money Laundering (Cross – Border Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments) Regulations, 2016 zikisomwa pamoja na kifungu cha 28B(1)(a) cha Sheria ya kuzuia utakasishaji wa fedha haramu, Na. 12 ya mwaka 2006.
“Hivyo, leo (jana) Septemba 7, mara baada ya kujiridhisha na uwepo wa ushahidi wa kutosha dhidi ya mtuhumiwa tajwa, sambamba na misingi ya kikatiba inayoniongoza kama ilivyoanishwa katika Ibara ya 59B(4)(a) hadi (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, nimeidhinisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa Saed Kubenea,” alisema DPP Mganga.