27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kubenea aunganishwa kesi ya kumjeruhi RAS

Saed-Kubenea-na-Jabir-Idrissa-620x311Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MBUNGE wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuunganishwa katika kesi ya kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam (RAS), Theresia Mbando.

Mshitakiwa mwingine aliyefikishwa mahakamani hapo jana kutokana na kosa hilo wanalodaiwa kulifanya wakati wa uchaguzi wa meya na naibu meya wa Jiji la Dar es Salaam na kuunganishwa katika kesi hiyo ni Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (Chadema).

Washitakiwa hao waliunganishwa katika kesi hiyo inayowakabili wabunge wengine wa Chadema, Halima Mdee (Kawe), Mwita Waitara (Ukonga), Diwani wa Kata ya Kimara (Chadema), Ephrein Kinyafu na mfanyabiashara Rafii Juma.

Kubenea na Njema walifikishwa mahakamani hapo mapema jana asubuhi na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa, alidai mara ya mwisho washitakiwa wenzao walishasomewa shitaka na waliomba hati ya kufika mahakamani kwa mshitakiwa Njema.

Alidai Njema yupo na ameongezeka Kubenea, hivyo aliomba kuwasomea shitaka washitakiwa hao.

Ombi hilo lilikubaliwa na Mkeha na wakili huyo aliwasomea Kubenea na Njema shitaka wanalodaiwa kulitenda Februari 27, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee, ulioko wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa washitakiwa hao kwa pamoja walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha. Hata hivyo, walikana shitaka hilo na upande wa Jamhuri ulidai upelelezi unaendelea.

Mkeha aliwaambia washitakiwa hao kuwa watajidhamini wenyewe kama walivyofanya wenzao kwa kutia saini dhamana ya Sh milioni mbili kila mmoja.

Kubenea na Njema walitimiza masharti hayo ya dhamana na hivyo kuachiwa kwa dhamana hadi Machi 16, mwaka huu, shauri hilo litakapotajwa tena.

Kubenea alipandishwa kizimbani ikiwa ni siku moja baada ya kutiwa mbaroni akiwa mahakamani hapo kuhudhuria shauri la kumtolea lugha ya matusi Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.

Kubenea alikamatwa juzi na askari akiwa mahakamani hapo na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Kati na baadaye walimrudisha tena kusikiliza shauri hilo.

Baada ya shauri hilo kuahirishwa askari waliondoka tena na Kubenea kwenda kituoni kwa ajili ya kuhojiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles