Kulwa Mzee na Asifiwe George, Dar es Salaam
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), amekamatwa na polisi na kuwekwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kuhusika na vurugu zilizotokea katika Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam Febaruari 26, mwaka huu.
Kubenea alikamatwa katika eneo hilo saa tatu asubuhi wakati akisubiri kuingia katika kesi inayomkabili dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
“Nilikamatwa na askari sita asubuhi, wakaniambia niko chini ya ulinzi, nikawauliza kosa, wakaniambia nikatoe maelezo kuhusiana na vurugu zilizotokea katika Uchaguzi wa Meya.
“Niliwaeleza nina kesi mahakamani, lakini hawakunisikiliza, wakanichukua hadi Kituo Kikuu cha Polisi, nilipofika niliwaeleza viongozi wa polisi wakaniruhusu nirudi mahakamani, baada ya kumaliza kesi niende kutoa maelezo.
“Nashangaa kwanini nituhumiwe kwa sababu mimi nilikwenda kushtaki waliotoa zuio la kuzuia uchaguzi nikitaka wachukuliwe hatua kwa sababu walitoa zuio lililopitwa na wakati, badala ya kushughulikia hayo wananikamata mimi,” alisema Kubenea na kuondoka na askari waliokuwa wakimsubiri.
MAHAKAMANI
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, mashahidi wawili wa utetezi, Shaabani Matutu na Joseph Isango walitoa ushahidi wakieleza kuwa Kubenea hakumtukana Makonda katika mgomo wa wafanyakazi.
Kubenea anakabiliwa na kesi ya kumtolea lugha chafu Mkuu wa Wilaya ya Konondoni, Paul Makonda kwamba ni mjinga, cheo alichonacho cha kupewa.
Akitoa ushahidi wa utetezi, Matutu alidai kuwa Desemba 14, 2015 katika Kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kilichopo Mabibo External kwenye mgomo wa wafanyakazi, hakusikia Kubenea akimwambia Makonda kuwa ni mjinga, mpumbavu, kibaka na cheo chenyewe kapewa.
Katika ushahidi wake, Isango pia alikana kusikia matusi hayo. Mashahidi wote waliongozwa na Wakili Peter Kibatala.
Kubenea kwa upande wake alifunga ushahidi kwa kuwa na mashahidi wake.
POLISI
Katika Kituo cha Polisi Kati, Kubenea alihojiwa kuhusu tuhuma za kumpiga Mwenyekiti wa Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Teresia Mmbando.
Mwanasheria wa Kubenea, John Kibatala, alisema mteja wake alikamatwa saa 3:35 akiwa nje ya Mahakama ya Kisutu.
Katika hatua nyingine, madiwani wanne wa Ukawa wanatakiwa kujisalimisha polisi kutokana na tuhuma hizo za kufanya vurugu ambao ni Dorcas Lukiko wa Viti Maalum Ukonga, Edwin Mwakatobe (Segerea) na Diwani wa Kata ya Liwiti aliyetajwa kwa jina moja la Mwaipaja huku Diwani wa Tabata, Patrick Asenga ameanza kuhojiwa baada ya kujisalimisha.