24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

KOROSHO ZATABIRIWA KULETA MAFANIKIO MAKUBWA KIUCHUMI

Mwandishi Wetu


MAPINDUZI ya kilimo yanawezekana ikiwa viongozi na wananchi watakuwa kitu kimoja na kushirikiana katika ufanyaji kazi  kama ilivyofanyika mkoani Mtwara na matokeo yake yameanza kuonekana kwa mafanikio ya zao hilo.

Korosho sasa ni zao la utajiri kwani bei yake imepaa kwa marefu na mapana na kufanya wadau kuwa na kicheko pande zote.

Inafurahisha kuona kuwa mapato yatokanayo na mauzo ya korosho katika msimu wa 2017/18 yamepanda na kufikia Sh1.08 trilioni katika mikoa minne ambayo ni kitovu  cha zao hilo ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita  na biashara bado inaendelea kufanyika.

Mikoa yenye kupata faida hiyo ni Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma amabayo imeonekana kuneemeka na bei nzuri, usimamizi bora wa mazao na Bodi ya Korosho, malipo kwa wakati mwafaka na uimara wa mfumo wa mazao ghalani.

Akizungumzia uzalishaji na mauzo ya korosho nchini hadi mwisho wa mwaka 2017, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho (CBT), Hassan Jarufu, alisema kiwango cha korosho na thamani ya mauzo kimeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma  na hususani mwaka 2015.

Alifafanua kuwa  msimu wa mwaka 2015/16 ziliuzwa kilo milioni 155.24 za korosho, zikiwa na thamani ya Sh388.4 bilioni lakini msimu wa 2016/17 ziliuzwa kilo milioni 265.24 zenye thamani ya Sh 871.4 bilioni.

Jarufu alisema katika minada kumi tu ya msimu wa 2017/18, mauzo ya korosho yamefikia kilo milioni 285.83 zenye thamani ya Sh1.08 trilioni na mnada wa kumi uliofanyika Desemba 21, mwaka jana na mambo bado yanaendelea sokoni kadiri bei inavyofurahisha wadau.

Mtwara yaongoza mauzo

Jarufu alisema Mtwara imeongoza kwa kuuza tani milioni 178.17 zenye thamani ya Sh bilioni 701.6, ikifuatiwa na Lindi ambao umeuza tani milioni 68.69 zenye thamani ya Sh247 bilioni. Jarufu alisema Ruvuma imeuza tani milioni 19.55 zenye thamani ya Sh76 bilioni na Pwani imeuza tani milioni 19.43 zikiwa na thamani ya Sh 57 bilioni.

Jarufu alitoa ufafanuzi huo  mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati alipozindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa msimu wa 2017/18 mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu, kampeni hiyo ina kaulimbiu ya ‘Korosho ni Dhahabu ya Kijani, Tuitunze, Itutunze’.

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema Bodi kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Naliendele, sekretarieti za mikoa na halmashauri imeendelea kutekeleza mpango wa miaka mitatu wa kupanda mikorosho milioni 10 kila mwaka ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo siku za usoni.

“Katika mpango huu, wastani wa mikorosho 5,000 inatarajiwa kupandwa katika kila kijiji au mikorosho 30 kwa kaya kwa mwaka, hiyo ni sawa na eka 330,000 kwa mwaka kwa nchi nzima,” alisema Jarufu.

Alisema malengo ya mpango huo ni makubwa  matatu, yaani kuongeza kiwango cha korosho kinachozalishwa nchini kwa kuongeza wigo wa idadi za halmashauri zinazozalisha na kupanda miche bora inayotokana na mbegu bora zenye uzalishaji mkubwa  na wenye ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu na kukuza ukubwa wa zao na wahusika wake.

Waziri Mkuu Majaliwa amewaasa vijana wanaoishi mikoa ambayo korosho inastawi, wajihusishe na zao hilo kwani kilimo chake kina fursa nyingi na ushindani wake si mkubwa.

Majaliwa alisema mahitaji ya korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika hotelini na kwenye mikutano mikubwa, zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe kubwa kwani liko mezani mwa wakubwa.

Wadadisi wa mambo wanasema sasa hivi korosho hutumika sana kama zawadi wakati wa sikukuu kubwa kama Krismasi badala au pamoja na maua, isitoshe kama chakula.

Rahisi kulima korosho

Mtu yeyote mwenye nguvu ya kufanya kazi na hasa kijana hawezi kushindwa kulima zao hilo, kwa sababu halihitaji uangalizi na mtaji mkubwa.

Waziri alifafanua kuwa kijana yeyote anaweza kulima zao hili kwa sababu eka moja ina miche 37 hadi 40 na kudai kuwa hakuna mtu atakayeshindwa kuangalia miche 37 hadi ikue. Aliendelea kwa kusema kuwa mbali na kilimo hicho kuwa rahisi pia ni rafiki wa mazingira, kwa kuwa miti ikikua inatunza mazingira na inasaidia kuleta mvua na kuunga mkona biashara ya ufugaji  nyuki kwa ajili ya asali ambayo inatakiwa duniani kote.

Majaliwa alirejea na kukumbusha umma kuwa mbali ya mikoa ya Pwani inayolima korosho ikiwamo ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Tanga, kuna mingine ambayo udongo wake umepimwa na kubainika kuwa zao hilo linaweza kustawi. Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe na Songwe.

Alisema mikoa ya Singida na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi kuhusu zao hilo kwani wanataka nao kushiriki katika kilimo hicho ili nchi hii iwe mbele kwenye zao hilo ambalo linaongozwa na  Vietnam kwa kilimo cha korosho na nchi ilichukua mbegu zake nchini kama vile Malaysia ilichukua michikichi kwa ajili ya mawese na migazi ambayo hutengeneza mafuta.

 

 Hadaa yaanza

Katika hali inayoonesha kupanda bei ya korosho kufanya mahitaji yake kuwa makubwa ili kunufaisha wanaostahili na wasiostahili, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wa vyama 10 vya msingi na kuwafungulia kesi ya uhujumu uchumi kutokana na uuzaji wa korosho chafu ili kujipatia fedha kiudanganyifu.

Wakulima wanadai zaidi ya Sh bilioni tano kutokana na kutolipwa korosho zao walizozipeleka katika vyama vya msingi.

Hatua ya Ndikilo kuagiza viongozi hao kukamatwa imetokana na baadhi ya wanunuzi kulalamika na kutishia kutonunua korosho kutokana na kubainika kujazwa mawe, mchanga na kokoto katika magunia.

“Inasikitisha sana wanunuzi wananunua korosho lakini zinapokaa katika maghala wakisubiri taratibu za kuzisafirisha na wanapozichukua na kuzifikisha sehemu husika, wanakuta mawe, mchanga na kokoto vikiwa vimechanganywa katika korosho hizo,” alisema Ndikilo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanunuzi wamefika katika ofisi yake wakionyesha ushahidi wa mawe, kokoto na mchanga na kudai kuwa hawana imani na minada ijayo hivyo hawatanunua tena korosho.

Ndikilo alisema anasikitishwa na hujuma ambazo zinafanywa na vyama vya msingi ndani ya mkoa huo kwa kuhujumu korosho na kusababisha hata ubora kushuka siku hadi  siku katika mnada.

Alisema wataalamu wanapopima korosho wanasema ni daraja la kwanza lakini kinachosikitisha baada ya siku nne, wanunuzi wakienda kuzinunua wanakuta ni daraja la pili na hivyo kuuzwa bei ya chini.

Anahoji bila kupata jibu juu ya tofauti kubwa ya bei kati ya Mtwara na Pwani na kugundua kinachotokea ni hujuma.

“Inakuwaje Mkoa wa Mtwara korosho zao ziuzwe daraja la kwanza kwa zaidi ya Sh 4,000, huku Pwani wakiuza Sh 2,300 daraja la kwanza?” alihoji Ndikilo.

Alisema chanzo cha kuporomoka kwa ubora wa korosho katika mkoa ni vyama vya msingi hivyo na kuagiza waliohusika wakamatwe, wahojiwe na kufikishwa mahakamani kwa mchezo mchafu wanaofanya na kuhujumu juhudi za wakulima.

Ndikilo ametaka polisi kuanza kuwakamata wenyeviti wa vyama vya msingi, watunza fedha na wasimamizi wao na kuwafikisha mahakamani ili wafunguliwe kesi ya uhujumu uchumi.

Vyama ambavyo viongozi wake wanatakiwa wakamatwe kwa taarifa ya Mkuu wa Mkoa ni Mkuchi Kibiti, Misugusugu (Kibaha), Karibu Mpakani, Baoni, Mianzi, Mahenge, Tuamke na Mkuchwi 2, vyote vya wilayani Kibiti.

Mbali na kuagizwa viongozi hao kukamatwa, pia alitaka kujua sababu za wakulima kutoka vyama vya msingi vya Msoganga, Magawa na Sangarani wilayani Mkuranga, kutolipwa fedha zao tangu kuanza kwa mnada wa korosho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles