SEOUL, KOREA KUSINI
RAIS wa Korea Kusini, Moon Jae-In, ameitaka Marekani kusitisha kwa muda mazoezi yake ya kijeshi nchini hapa ili kupisha michuano ya Olimpiki itakayofanyika mapema mwakani.
Amesema hii itasaidia pia kuifanya Korea Kaskazini kutokuwa na shaka juu ya uwepo wa wanamichezo wake kwenye michuano hiyo.
Korea Kusini ni mwenyeji wa michezo hiyo itakayofanyika kwenye mji wa Pyeongchang Februari, kilomita 80 kutoka mpaka wake na Korea Kaskazini.
Mapema Canada na Marekani ziliapa kuendeleza mazoezi hayo ili kuishinikiza Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia.
Michuano ya Olimpiki ya majira ya baridi inatarajiwa kuhusisha pia wanamichezo kutoka Korea Kaskazini jambo ambalo Rais Jae-In anaeleza ni fursa ya kuimarisha uhusiano zaidi.