PYONGYANG, KOREA KASKAZINI
KOREA Kaskazini imefanya jaribio lenye mafanikio la kombora la masafa marefu lenye nguvu ya kushambulia taifa zima la Marekani.
Taarifa ya kurushwa kwa kombora hilo ilitangazwa jana na Kituo cha Habari cha Korea Kaskazini (KCNA).
Kwa mujibu wa KCNA, majaribio ya kurushwa kwa kombora yalishuhudiwa na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un aliyekaririwa akijuvuna kuwa taifa lake limekamilisha azma ya kihistoria ya kuwa dola yenye nguvu za kinyuklia.
Vyombo vya habari mbalimbali duniani vimeripoti kuwa tayari jumuiya ya kimataifa imelaani jaribio la kombora hilo linalojulikana kwa jina la Hwangsong 15.
Jaribio hilo la kwanza la kurushwa kwa kombora lenye uwezo wa kuisambaratisha Marekani limefanyika wiki moja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuiweka Korea Kaskazini katika orodha ya mataifa yanayounga mkono ugaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis alikaririwa muda muda mfupi baada ya kurushwa kwa kombora akieleza kuwa limeruka umbali mrefu zaidi hivyo kumaanisha Korea Kaskazini inazidi kujiimarisha katika majaribio yake ya makombora.
Kombora Hwangsong 15 ambalo ni la masafa marefu linaelezwa kuwa na nguvu zaidi na uwezo wa kuruka juu na umbali mrefu kuliko makombora yaliyofanyiwa marekebisho kipindi cha nyuma.
KCNA iliripoti kuwa kombora Hwangsong 15, lenye nguvu mara mbili ya lililorushwa mwezi Julai, mwaka huu liliruka urefu wa kilomita 4,475 na kusafiri umbali wa kilomita 950, kwa dakika 53 kabla ya kuanguka baharini karibu na Japan.
Hata hivyo, mbali na kufanya jaribio hilo, Korea Kaskazini ilieleza kuwa inapenda amani na uundaji wa silaha za nyuklia inaoufanya umelenga kujihami dhidi ya ubeberu wa Marekani, vitisho na sera zake kandamizi za nyuklia.
Marekani, Japan na Korea Kusini zote zilikubaliana kuwa kombora hilo huenda ni la masafa marefu lakini Wizara ya Ulinzi ya Marekani ilisema halikuwa tishio kwa Marekani yenyewe, maeneo inayoyadhibiti wala washirika wake.