PYONGYANG, KOREA KASKAZINI
SERIKALI ya Korea Kaskazini imewasiliana na Marekani ikisema kiongozi wake, Kim Jong Un, yuko tayari kuujadili mpango wake wa silaha za nyuklia na Rais Donald Trump.
Kauli hiyo, inaongeza uwezekano mkubwa wa kufanyika kwa mkutano wa kilele kati ya viongozi hao.
Uthibitisho huo wa moja kwa moja wa Korea Kaskazini, badala ya kutumia nchi ya tatu kama vile Korea Kusini, umeongeza imani katika utawala wa Trump kuhusu uamuzi wa kufanya mkutano wa aina hiyo, huku maofisa wa Marekani wakiendelea kufanya matayarisho kwa siri.
Kauli hiyo inakuja kutokana na msimamo wa muda mrefu wa utawala wa Trump, kuwa kama Korea Kaskazini hawako tayari kujadili suala la kuachana na mpango wao wa nyuklia, hakuna sababu ya nchi hizo mbili kufanya mazungumzo.
Trump aliishangaza Serikali yake mwezi uliopita wakati alipokubali mwaliko usio wa kawaida kutoka kwa Kim wa kufanya mkutano wa kilele.