Pyongyang Korea Kaskazini
KOREA Kaskazini imeapa kuendelea na kampeni yake ya kutuma vipeperushi vya propaganda kuelekea Korea Kusini, ikisema kwamba haifungwi na makubaliano yoyote baina yake na Kusini.
Wasiwasi unazidi kuongezeka tangu Korea Kaskazini kuliripua jengo linalotumiwa na nchi hizo mbili kama afisi ya pamoja, na kutishia hatua za kijeshi dhidi ya raia wake waliokimbilia Kusini na kutuma vipeperushi vya kuupinga utawala wa Kim Jong Un mipakani.
Shirika la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), liliripoti kwamba wananchi wenye hasira wanaandaa kampeni yao wenyewe ya vipeperushi, huku wizara yenye dhamana ya kuungana tena kwa Korea hizo mbili kwa upande wa Kusini, ikisema kampeni hiyo inakiuka makubaliano baina ya nchi hizo.