NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA msaidizi wa Azam FC, Denis Kitambi, amesema kuwa mbeleko ya mwamuzi Kennedy Mapunda, imewasaidia Yanga kuwabania ushindi katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguko wa pili juzi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Timu hizo zilimaliza dakika 90 za mchezo kwa kupata sare ya mabao 2-2, ikiwa ni sare ya pili kuipata kwani kwenye mzunguko wa kwanza walimaliza kwa sare ya bao 1-1.
Kwa matokeo hayo, Azam imeendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, ikilingana pointi na wapinzani wao ambao wanaongoza kwa kujikusanyia pointi 47 kila mmoja kwa tofauti ya magoli.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kitambi alisema hawakufurahishwa na maamuzi ya kocha huyo ambayo yalionekana dhahiri kuwasaidia wapinzani wao hivyo kuchezesha bila haki.
“Mara nyingi tumekuwa hatutendewi haki na maamuzi ya baadhi ya waamuzi, hasa tukicheza na hizi timu ambazo zimekuwa zikiongoza ligi na tukilalamika kocha wetu anafungiwa ndio maana hata leo (juzi) hakutaka kuja kuzungumzia mchezo, kwani anahofia adhabu hiyo isimpate, tunawaomba waamuzi wafuate sheria za soka zinavyosema,” alisema.
Alieleza, licha ya maamuzi hayo ya uonevu wanawapongeza wachezaji wao kuonyesha mchezo mzuri kwa kuweza kujituma katika dakika zote za mchezo.
Alisema dakika 25 za awali walianza vizuri lakini baada ya kuruhusu wapinzani wao kupachika mabao 2 katika kipindi hicho cha mwanzo, waliona ipo haja ya kuwapa mbinu zaidi wachezaji wao wakati wa mapumziko na waliweza kuzifanyia kazi na kusawazisha.
Kitambi alisema, walikuwa na nafasi zaidi ya kuongeza bao jingine kutokana na uimara waliouonyesha wachezaji wao, lakini maamuzi hayo mabovu ya mwamuzi yalisitisha mipango yao.