KOCHA wa klabu ya Liverpool, Jurgen Klopp, amefanikiwa kufanyiwa upasuaji wa kidole tumbo baada ya kujisikia vibaya tangu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kocha huyo alianza kupata dalili ya ugonjwa huo Ijumaa iliyopita akiwa katika Hoteli ya Hope Street, kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya Sunderland ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2.
Hata hivyo, baada ya kufanyiwa upasuaji huo hali yake inaendelea vizuri kwa sasa huku akiwa katika uangalizi wa daktari wa timu hiyo, Andy Massey.
Katika mchezo wa juzi dhidi ya Sunderland, kocha huyo alikuwa hospitali huku timu yake ikishindwa kutamba mbele ya mashabiki wake huku wakiwa mbele kwa mabao mawili lakini wapinzani waliyarudisha.
“Najua hali ya klabu kwa sasa ni mbaya kutokana na matokeo yanayojitokeza, lakini ninaamini hali hii itafikia mwisho kikubwa ni kushirikiana kati ya mashabiki, viongozi na wachezaji kwa ujumla.
“Hakuna ambaye anapenda hali iwe hivi lakini ndivyo soka lilivyo na linaweza kubadilika muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa bado tuna wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo,” alisema Klopp.
Kwa sasa Liverpool inashika nafasi ya 9 ikiwa na pointi 35 katika msimamo wa ligi, hivyo mashabiki wameanza kuitupia lawama klabu yao kutokana na mwenendo mbaya.