NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA Hemed Khalifa (40) na mwenzake, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na shtaka la kuingilia miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kinyume na sheria.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Kassian Matembele na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Maternus Marandu.
Wakili Marandu alidai washtakiwa walitenda kosa hilo Julai 29, mwaka huu eneo la Mikocheni, Dar es Salaam.
Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Abdulrazaki Said (49) mkazi wa Temeke.
Wanadaiwa kwa nia ovu waliingilia miundombinu ya Tanesco kwa kujiunganishia umeme kutoka mfumo wa shirika hilo na kupitisha pembeni ya mita kinyume na sheria.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Kesi iliahirishwa hadi Septemba 9 kwa ajili ya kutajwa.
Wakati huo huo, mfanyabiashara Anuary Hamdani (29) na fundi umeme Joseph Oswald (31) wamefikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na shtaka la kuhujumu miundombinu ya Tanesco.
Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Luboroga ambapo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Maternus Marandu alidai washtakiwa walitenda kosa hilo Agosti 7, mwaka huu eneo la Magomeni Mikumi, Dar es Salaam.
Inadaiwa kwa nia ovu, washtakiwa hao waliingilia miundombinu ya Tanesco kwa kuondoa mita ya umeme kutoka nyumba ya Ahmed Amdani iliyokuwa na deni la Sh 3,521,587.70 na kuwekwa mita nyingine mpya kwa lengo la kulikwepa.
Baada ya kusomewa shtaka hilo, washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.
Kesi imeahirishwa hadi Septemba 10 kwa ajili ya kutajwa.