29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kiwalani, Kinyerezi, Segerea kuanza kutoa huduma za upasuaji

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wajawazito waliokuwa na changamoto za uzazi na kushindwa kujifungua katika Zahanati za Kiwalani, Kinyerezi na Segerea wataondokana na kero hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo hayo.

Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli (kushoto), akiangalia baadhi ya vifaa tiba vilivyotolewa katika Kituo cha Afya Segerea. Watatu kulia ni Diwani wa Kata hiyo, Robert Manangwa.

Vituo hivyo ambavyo vimejengwa kupitia fedha za Serikali Kuu vinatarajiwa kufunguliwa rasmi mwishoni mwa mwezi huu na tayari vifaa tiba vimepatikana.

Akizungumza Oktoba 5,2023 wakati wa kukabidhi vifaa tiba katika vituo hivyo Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuwaondolea kero kinamama wa jimbo hilo.

“Tuna mkataba na wananchi wa miaka mitano, ikifika 2025 tunatakiwa tuwaonyeshe yale tuliyowaahidi kuwafanyia. Tunamshukuru sana mheshimiwa Rais kwa namna anavyotupigania wana Segerea.

“Jimbo la Segerea lina watu wengi na tulikuwa tunategemea kituo cha afya kimoja kilichopo Mnyamani, lakini tunamshukuru sana mheshimiwa rais na Wizara ya Afya, tunaomba tuendelee kupata vituo vya afya ikiwezekana jimbo zima.

“Ujenzi wa vituo vya afya na ununuzi wa vifaa tiba utasaidia kuokoa wajawazito na watoto wachanga ambao wakati mwingine walilazimika kupewa rufaa kwenda Hospitali ya Amana,” amesema Bonnah.

Diwani wa Kata ya Segerea, Robert Manangwa, amesema ujenzi wa kituo cha afya ni miongoni mwa mambo waliyoahidi wakati wakiomba kura kwa wananchi na kwamba watahakikisha yote waliyoahidi wanatekeleza.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Zaituni Hamza, amesema vifaa hivyo vina thamani ya Sh milioni 300 na kila kituo kimekabidhiwa vifaa vya Sh milioni 100.

Amevitaja vifaa hivyo kuwa ni vitanda 75 vya kujifungulia 75, mashine za usingizi, meza za kufanyia upasuaji, mashuka 900, viti 15 vya kubebea wagonjwa, mashine 30 za kupima presha na vingine.

“Katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuna ukurasa unaozungumzia sekta ya afya kwahiyo kazi yetu ni kuhakikisha tunatekeleza maelekezo yote, hili tunalolifanya leo ni miongoni mwa utekelezaji kuhakikisha kwamba kila kata inakuwa na kituo cha afya ifikapo 2025.

“Tumekubaliana kama watendaji ifikapo mwisho wa mwezi huu tuhakikishe vituo vyote vitatu viwe vimefunguliwa, vina vifaa tiba na wananchi wanapata huduma. Zoezi hili litafanyika kwenye majimbo yote matatu ndani ya Wilaya ya Ilala.

“Shukrani za dhati ziende kwa mheshimiwa rais anaiheshimisha sekta ya afya, deni letu kwake ni kuhakikisha tunakwenda kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Dk. Zaituni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles