MALABO, EQUATORIAL GUINEA
MICHUANO ya kuwania Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), inatarajia kuanza leo katika Uwanja wa Bata nchini Guinea ya Ikweta huku wenyeji wakifungua michuano hiyo dhidi ya Congo.
Guinea ya Ikweta watawakaribisha Congo katika Uwanja wa Estadio de Bata wakitumia mfumo wao wa 4-2-3-1.
Kocha wa timu hiyo, Esteban Becker raia wa Argentina, amejipa matumaini ya ushindi katika mchezo huo kutokana na uzoefu wake huku akiamini kuwa ana nafasi kubwa kwa kuwa yupo nyumbani na idadi kubwa ya mashabiki.
Kocha wa Congo, Claude Le Roy, ametamba kufanya vizuri katika mchezo huo kwa kuwa ana rekodi ya kuchukua ubingwa wa michuano hiyo mara saba.
Katika mchezo mwingine,Burkina Faso watavaana na Gabon katika uwanja huo wa Estadio de Bata, huku Burkina Faso wakipewa nafasi kubwa ya kushinda kutokana na uwezo wao ambao waliuonesha msimu uliopita katika michuano hiyo.
Gabon wanaweza kufanya vizuri katika mchezo huo kwa kuwa wana mchezaji ambaye anakipiga katika kikosi cha Borussia Dortmund, Pierre Aubameyang ambaye alikuwa ni tegemeo katika nusu fainali ya mwaka 2012.