Na MWANDISHI WETU – Dar es Salaam
HAKUNA shaka kwamba wanasiasa kutoka vyama viwili vinavyopambana vikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameanza kuteswa na kivuli cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Ikiwa ni mwaka mmoja na ushei tangu uchaguzi wa mwaka 2015 ufanyike na kuacha alama ya kuwapo kwa upinzani mkali dhidi ya CCM, kuibuka kwa kauli za wanasiasa hao juu ya uchaguzi wa mwaka 2020, kunaelezwa kunatokana na yanayojiri katika uongozi wa sasa ulio madarakani.
Kauli ambazo zimepata kutolewa kwa nyakati tofauti na Rais Dk. John Magufuli mwenyewe, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, zote zinaashiria uchaguzi wa mwaka 2020 umeanza kuwanyima usingizi.
Kauli ya hivi karibuni ni ile iliyotolewa na Nape wakati alipokwenda kuzungumza na wananchi wa jimbo lake la Mtama mkoani Lindi.
Nape ambaye alizungumza siku kadhaa baada ya Rais Dk. Magufuli kumwondoa katika wadhifa wake, alikuwa akirejea matukio kadhaa ya utekaji watu akisema yasipodhibitiwa yataipa shida CCM mwaka 2020.
“Naomba hatua zichukuliwe tukomeshe hii tabia, Ben Saanane amepotea miezi mingi na mazingira ya kupotea ni ya kutatanisha. Matendo haya yasipotatuliwa na kukomeshwa, tutapata shida sana 2020,” alisema.
Kauli hiyo ya Nape aliyepata kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, ilitanguliwa na kauli mbili zinazorandana, alizozitoa Rais Magufuli katika matukio mawili tofauti miezi kadhaa iliyopita, ambazo zote zimetoa taswira ya ugumu anaouona kuelekea mwaka 2020.
Wakati alipofanya ziara Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa CCM, alisema ni heri awe rais wa kipindi kimoja kuliko kuacha madudu anayoyaona.
Kauli nyingine ni ile aliyoitoa wakati akizindua ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambazo kwa sasa tayari ujenzi wake umekamilika.
“Ni vizuri uwe unpopular president (rais asiye maarufu), lakini utimize yale uliyoyahidi,” alisema Rais Magufuli.
Oktoba 8 mwaka jana, Waziri Mkuu wa zamani, Sumaye, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwaambia wanachama wa chama hicho kuwa wanapaswa kujitoa katika shughuli za ujenzi wa chama ili kuweza kufikia lengo la kushika dola ifikapo mwaka 2020.
Sumaye alitoa kauli hiyo wilayani Mkuranga, Pwani wakati wa shughuli ya kuchangia ujenzi wa ofisi ya Chadema.
“Ninaamini wote tuliopo tutajitoa kwa moyo mmoja, najua ni kazi ngumu kuwa na chama tofauti na chama tawala, lakini tunapaswa kupambana kufikia malengo,” alisema Sumaye ambaye kabla kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, alijitoa CCM na kuhamia Chadema kwenda kumwongezea nguvu aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.
Sumaye, alisema mazingira yanaonyesha hata CCM inajua kuwa Chadema itashika dola, hivyo vijana waijenge kuanzia ngazi ya matawi.
“Lazima tujitolee, dola haipatikani kiurahisi, tunapaswa tuwaeleze wananchi tutawafanyia nini, hatuwezi kufanya kazi za chama kwenye nyumba ya mtu au ofisi za vichochoroni kuanzia mwaka 1992,” alisema Sumaye.
Baada ya kauli hiyo ya Sumaye, miezi mitano baadaye, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mbowe alisema atajiuzulu siasa iwapo Rais Magufuli atashinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai mkoani Kilimanjaro, alitoa kauli hiyo akiwa Muheza mkoani Tanga wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho.
“Huyu atakuwa rais wa kwanza kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano tu. Na kama Magufuli akishinda tena uchaguzi mwaka 2020, mimi nitajiuzulu siasa,” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa chama chake tayari kimeanza kujiandaa na uchaguzi wa 2020, akisisitiza kwamba kumalizika kwa uchaguzi mmoja ni maandalizi ya uchaguzi mwingine.
USHINDANI TAASISI KWA TAASISI
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa kwa hali iliyopo sasa, kuelekea kwenye uchaguzi mkuu 2020 kumekuwa na mchuano wa kimya kimya kati ya CCM na Chadema kupitia taasisi mbalimbali.
Miongoni mwa taasisi hizo ni Chama cha Wanasheria (TLS) ambacho rais wake ni Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki anayeshikilia nyadhifa za uanasheria wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Inaelezwa kuwa kitendo cha makada wawili wenye nguvu kugombea urais wa TLS, Lawrence Masha na Lissu, ilikuwa ni kuiingiza Chadema kwenye mpambano na CCM wa kuwania kuzishika taasisi mbalimbali.
Duru za mambo katika medani ya siasa, zinadai kwamba miaka mingi CCM imekuwa na ‘watu wake’ katika taasisi mbalimbali za kitaaluma ambazo zimekuwa zikiwaongezea nguvu kwenye jamii.
Mifano ya taasisi hizo ambazo zimekuwa zikitajwa tajwa ni TLS, Chama cha Walimu (CWT), Chama cha Wafanyakazi (Tucta) na vyama vingine vya kitaaluma.
Nchi nyingi duniani tangu zama za ukoloni, vyama vya kitaaluma au wafanyakazi vimekuwa chachu ya ushindi katika chama cha kisiasa.
Huko nyuma, baadhi ya viongozi wa TLS majina yao yalipata kutajwa kuwa na mfungamano wa namna moja ama nyingine na CCM.
Wataalamu wa sayansi ya siasa wanasema hatua ya kupambanisha taasisi dhidi ya taasisi ni miongoni mwa mbinu kuntu zinazotumika na wanasiasa wenye mrengo wa kimapinduzi, akiwamo waziri mkuu wa zamani, Lowassa.
Mara kadhaa Lowassa amekaririwa akipingana na siasa za kiharakati, hususani za maandamano, huku akielekeza kuwa hazina na tija zielekezwe kwenye mbinu mbadala ambayo hajawahi kuitaja.