23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kiu ya Damu

kiu

ILIPOISHIA…

Msamaha wa dhambi niliyoitenda mimi, nilistahili kumsamehe. Thamani yake ilikuwa kubwa sana huko asikokujua. Niliamua kutomsamehe.

Kwa roho nyeusi katikati ya doa la damu nilimtamani. ‘Buriani Ndisa. Ulimpenda sana Latifa. Wako wa kufa na kuzikana. Wako wa huba na hiba.’ Yalikuwa maneno yaliyoogelea kwa fujo kichwani mwangu.

Kono langu la kulia lilikuwa na panga. Nilikuwa nimeliweka juu ya koromea lake kama vile nifanyavyo wakati wa sherehe kwa kuutoa uhai wa jimbi kwa ajili ya kitoweo.

SASA ENDELEA…

 

MBELE kisha nyuma, nililisukuma. Nilikandamiza kidogo nikasikia na kuhisi likizama kisha kulipasua koromea. Damu ya moto ilinirukia na kuufunika uso na kifua changu. Hukumu hukumuni. Nilimaliza kuhukumu. Kiu yangu ya damu iliendelea.

Nilisimama na kuuachia mwili wa Ndisa pale gizani ukiwa bado haujatulia. Juu kisha chini wakati mwingine ulizunguka zunguka kule kisha huku.

Kichwa kilikuwa kikifurukuta mikononi mwangu kwa kuutoa ulimi nje na kuutanua mdomo. Alitaka kuongea pengine kunijuza juu ya maumivu aliyoyahisi. Isivyo bahati, maskini alikuwa si mtu tena. kwa unyama nilimtwaa, haraka kumfuata aliyempenda.

Akili yangu ilihama. Ilisafiri hadi kwenye shamba la watu katili. Katikati ya wanyama wakali wenye kiu ya damu wasio na hofu ya mkuki wala risasi. Nilipiga hatua kuelekea maskani kwangu.

Bado kimya kilikuwa kimya. Hapakuwa na mtu ambaye alikuwa mbele yangu kutokana na siahi za Ndisa. Nilisikia wengi wakingo’ona ndani ya majumba yao. Kwa hebedari za mji, mla naye si mfa naye, walijichuma ndani kimya kwa hofu ya karaha za mjini.

Ndugu yangu na rafiki yangu, tayari nilikuwa nimetwaa maisha ya watu watatu kwa mkono wangu. Tena kwa ncha kali ya upanga nilioununua kwa fedha kichele, alfeni tatu. Maisha yangu yalikuwa katikati ya damu, damu za watu si wanyama wa sadaka ya tambiko.

Kwa bashiri watu wangedhani nilihitaji kutoroka, hapana. Sikuwa mtoro. Niliingia ndani ya nyumba yangu hadi chumbani. Niliiwasha taa iliyoutapika mwanga mkali. Macho yangu hayakuweza kuamini kile nilichokiona ingawaje nilikitenda mimi.

Nilisogea kitandani kisha kulifungua sanduku la nguo za mke wangu. Moja kwa moja nilikutana na ua jekundu ambalo nilimnunulia miaka mingi ambayo tulianza mapenzi. Kumbukumbu zilinirejesha hadi kule, alivyokuwa mwaminifu kwangu. Kila nilipojaribu kupotezea, taswira kuu ilijaa akilini mwangu.

Mara kumbukumbu zilinifikisha wakati ule naunyanyua mkono wangu kumkatili maisha yake. Mhamo wa mauaji hadi tukio la kumuua Ndisa. Mwili ulipigwa ganzi kisha niliyoyoma sakafuni na kutulia. Sikuweza tena kufikiri jinsi ya kujificha hata kuificha miili ile ya watu nilio waangamiza. Machozi niliyahisi kunifunika machoni. Hisia za utu zilinijia, nilijiona mkosaji.

Nilikuwa tayari katika hali ya mwili kupoa, hali ya kuwa mtu mwenye kujuta. Roho ya ukatili ilitoweka, hofu ilinijaa. Uoga ulinigubika hadi mwili ulijawa baridi. Kwa kujitazama, niliyaagiza macho yangu kuukagua mwili wangu, damu zilitapakaa.

Shujaa wa kifo siku zote rafiki wa kifo. Sikutaka tena kukubali kuwa nilikuwa shujaa. Nilikubali kuwa dhaifu, tena dhaifu niliyeua kwa hisia na hofu ya kuonewa.

Ningali sakafuni, nafsi yangu haikuwa hai. Niliuendea mkoba wa mke wangu kisha kuufungua. Nilikutana na kila aina ya dawa ambazo mjamzito huzipata kwa uimara wa afya yake. Nilizikupua zote kisha kulichukua jagi la maji lililokuwepo pale kisha kuzitupia mdomoni. Nia yangu kifo.

Nilitaka kufa, lakini si kwa mvujo wa damu. Mchanganyiko wa dawa nyingi, zilizozidi thelathini nilizitumbukiza ndani ya domo langu lililokuwa limegeuka na kuwa chungu kwa hamaki. Nilizimeza zikashuka kisha nilijilaza sakafuni.

***

BANGILI ZA MHALIFU

Baada ya dakika chache kupita, mwili haukuwa wangu. Nilihisi zilizala na jasho jekejeke likinitoroka na kuufanya mwili wangu kuwa chepechepe.

Uono wangu ulikuwa hafifu nikawa sioni zaidi ya ukungu. Ghafla macho yalizima na fahamu zilinihama. Sikijua yaliyoendelea usiku ule na wala simkumbuki nani alikuwa wa kwanza kunifikia.

 

***

Kwa shida niliyafumbua macho yangu. Niliyazungusha kushoto kisha kulia, juu chini na kuambaa ndani ya chumba nilimokuwa nimelala. Nilijaribu kunyanyuka kwa haraka ili niketi kwa uhuru, nilishindwa.

Haraka nililiangalia shuka, lilikuwa na nembo ya hospitali. Mguuni kulikuwa na bangili iliyofungwa kwenye kitanda kile. Mkono wangu wa kushoto pia ulikuwa na bangili ambayo nayo ilikuwa imenishikiza kwenye kile kitanda.

Harufu ya dawa ambayo sikuwahi kuipenda nifikapo hospilalini ilikuwa imetapakaa na kuzichafua pua zangu. Macho yangu kisha niliyaagiza kuutazama mkono wangu vizuri, ulikuwa bado na sindano iliyokuwa imeganda karibu na kiganja. Nilijiweka sawa kutaka kuketi.

Nilijikagua kila sehemu ya mwili wangu kwa haraka lakini nilihisi kuwa sikuwa hata na chembe ya mkwaruzo. Hamaki zilinijaa.

Nikiwa katika tafakari, ghafla aliingia mwanamke mmoja mrefu, mweusi mwembamba. Alikuwa msichana, si mzuri wa sura lakini umbo, ngozi nzuri ambayo naihusudu. Alikuwa mweusi ambaye hakuwahi kuuchuna uso wake kwa vipodozi. Alisimama wima mbele yangu kisha kuchanua kwa tabasamu.

 

Je, nini kitatokea? Usikose wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles