32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kituo cha huduma kwa wateja chaongeza ufanisi utendaji kazi Ardhi

Na Munir Shemweta, WANMM

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeboresha kituo chake cha Huduma kwa Wateja kwa lengo la kuwarahisishia wananchi kupata huduma za sekta ya ardhi kwa haraka na kwa ufanisi.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam Idrisa Kayera akisisitiza jambo alipokuwa akielezea uboreshaji huduma za sekta ya ardhi katika mkoa wake kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja.

Kwa sasa kituo hicho kinahudumia idadi kubwa ya wateja wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani tofauti na hapo awali ambapo kwa sasa mara mteja anapofika Kituo cha Huduma kwa Wateja hupatiwa namba ya huduma inayomuwezesha kuhudumiwa kulingana na muda aliofika na eneo analohitaji kuhudumiwa.

‘’Unapofika kituo chetu cha Huduma kwa Wateja  pale umewekwa utaratibu maalum ambapo mteja anahudumiwa kwa wakati na taarifa zote zinazohusiana na ardhi zipo kwa kuwa kuna mfumo unganishi wenye taarifa za upimaji, mipango miji pamoja na hati na suala la  kutatua mgogoro ni rahisi zaidi,’’ alisema Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dar es Salaam Idrisa Kayera.

Kwa mujibu wa Kayera, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeamua kuboresha kituo hicho ili kuwezesha huduma za sekta ya ardhi zitolewe kwa haraka na ufanisi kwa kuwa huduma zinazohusu mipango miji, upimaji, maandalizi ya hati pamoja na taarifa za kodi zinapatikana kwenye kituo hicho.

Kamishna huyo Msaidizi wa Ardhi aliyekuwa akizungumza jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na kituo hicho, alisema Wizara yake imeweka pia maeneo ya kulipia kodi na tozo mbalimbali karibu na kituo hicho lengo likiwa kuhakikisha huduma inapatikana kwa haraka zaidi.

 ‘’Mtu akija atakuta kuna benki karibu kwa ajili ya kufanya malipo na pia kumbukumbu zake za nyaraka kuhusiana na masuala ya ardhi atazikuta, ramani za eneo na picha ya anga ya mkoa wa Dar es Salaam ipo, kwa hiyo tunaweza kutatua migogoro kwa urahisi na kushughulikia changamoto,’’ alisema Kayera.

Kwa upande wake Msimamizi wa Kituo cha Huduma kwa Wateja, Bayumu Mushi alisema uanzishwaji kituo hicho ulilenga kuondoa kero waliyokuwa wakiipata wananchi wanapofuata huduma za ardhi ambapo awali walipotaka huduma walimfuata afisa ardhi yeyote lakini sasa wanapofika eneo la mapokezi huulizwa shida na kupelekwa kwenye dawati husika.

Mmoja wa wateja waliofika kituo hicho cha Huduma kwa Wateja Charles Ndesanjo alisema ameridhishwa na huduma zinazotolewa na kituo hicho kwani aliweza kuhudumiwa haraka kupata hati yake ya ardhi katika kiwanja chake kilichopo Bagamoyo mkoa wa Pwani tofauti na matarajio yake.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya uwakili ya Idda Attorney, Eliminata Membo alikielezea kituo hicho kama mkombozi kwao kwa kuwarahisishia sana kazi za kufuatilia nyaraka mbalimbali za ardhi kutoka kwa wateja.

Alex Riwa mkazi wa Airport mtaa wa Mogo jijini Dar es Salaam alielezea kituo hicho kuwa kimesaidia kwa asilimia 80 kushughulikia kero za wananchi na kuondoa urasimu uliokuwemo awali katika ofisi hiyo. Amezitaka ofisi nyingine za ardhi katika mikoa nchini kuiga mfano wa ofisi ya Dare es Salaam kwa kuanzisha kituo cha huduma kwa wateja ili kuondoa kero kwa wananchi wanaohitaji huduma za ardhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles