Na Mohamed Hamad
Wananchi wilayani Kiteto mkoani Manyara wameshindwa kutumia kituo cha elimu (maktaba) kupata maarifa tofauti na baadhi maeneo mengine nchini.
Kituo hicho kilijengwa kwa ufadhili wa watu wa Marekani chenye hadhi ya kitaifa ambacho kiliwekwa jiwe la msingi na aliyekuwa waziri wa elimu, Jeseph Mungai Machi 1, 2004 na kufungukiwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa Novemba 15, 2006.
Kituo hicho kina chumba cha elimu ya awali, msingi, Sekobdari, watu wazima ambapo wanafundisha wasiojua kusoma kuhesabu na kuandika hadi elimu ya juu (chuo kikuu huria) pamoja na elimu ya kompyuta.
Akizungumza na MTANZANIA, Katibu wa kituo hicho, Mwalimu Jeremia Gibayi amesema pamoja na hamasa inayotolewa kwa jamii bado wameshindwa kukitumia kikamilifu.
“Kituo hiki ni kikubwa kina hadhi ya Kitaifa na ambacho maeneo mengine wamekuwa wakinufaika sana na kituo kama hiki lakini Kiteto imekuwa ni kinyume chake na kubaki wakikiangalia tu.
“Nitumie fursa hii adhimu kuwaambia wananchi wa Kiteto kuwa wamepata bahati kuwa na jengo kubwa ambalo limesheheni maarifa na ujuzi hivyo kinachotakiwa ni utayari wao,” amesema Gibayi.
Mkurugenzi wa kituo hicho, mwalimu Paulo Gwacha amesema baada ya mtu kuhitimu anapatiwa cheti cha mafunzo aliyopata akidai kituo kimethibitishwa na Wizara ya Elimu kutoa mafunzo hayo.
Amesema lengo la kuanzishwa kituo hicho ni kuondoa adha waliokuwa wanapata wanafunzi kujiendelea baada ya mwalimu wa kimarekani aliyekuwa anafundisha Kiteto Sekondari, Jenifa kubaini tatizo hilo.
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Kiteto, Kanali Patrick Songea amewaasa wananchi wilayani humo kujitokea na kutumia kituo hicho kikamilifu ili kiweze kuwanufaisha.