31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 55 YA UNICEF Afya ya watoto imeboreshwa ukilinganisha awali

Na LEONARD MANG’OHA

TAARIFA ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (Unicef) ya Aprili mwaka 2017 inaonesha kuwa kiasi cha watoto 269 walio chini ya umri wa miaka mitano wanaelezwa kufariki dunia kila siku hapa nchini.

Aidha tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa idadi ya vifo vya watoto wa umri huo imekuwa ikipungua ambapo kiasi cha vifo 147 kati ya vizazi hai 1000 zilirekodiwa mwaka 2000 lakini mwaka idadi hiyo ilishuka hadi 67 katika utafiti wa mwaka 2015.

Pia vifo vya watoto wachanga vilipungua kutoka 40 mpaka 25 katika kila vizazi hai 1000 katika kipindi hicho.

Mtaalamu wa afya kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia Watoto (Unicef), Dk. Thomas Lyimo, anael;eza kuhusu hali ya afya kwa watoto hapa nchini kwa kuzingatia ilivyokuwa hapo kabla, ilivyo na matarajio ya baadaye.

MTANZANIA: Hali ya afya kwa watoto kwa ujumla ikoje ikilinganishwa na wakati ambapo mlianza kufanya kazi hapa nchini?

Dk. Lyimo Kwa ujumla hali ya afya ya watoto imeboreka ukilinganisha na miongo (decades) miwili iliyopita. Vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 147 (mwaka 2000) mpaka vifo 67 (mwaka 2015) katika kila vizazi hai 1000. Vivyo hivyo kwa watoto wachanga katika kipindi hicho vimepungua toka vifo 40 mpaka 25 katika kila vizazi hai 1000.

Hii imetokana na juhudi za serikali ikishirikiana na wadau wa maendeleo ikiwamo Unicef, kuboresha huduma za afya hasa za chanjo, lishe na matibabu bora kwa magonjwa ya Malaria, kuharisha na Nimonia ambayo yaliongoza katika kusabisha vifo kwa watoto wadogo.

Serikali pia inaendelea kupambana na maambukizo ya virusi vya ukimwi, programu ya kutokomeza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, changamoto kubwa imebakia ni maambukizi wakati wa unyonyeshaji. Na kwa wale watoto wanaoishi na virusi vya ukimwi asilimia 66 wanapata dawa za kufubaza virusi vya ukimwi.

MTANZANIA: Unicef imetoa kipaumbele katika maeneo gani ya afya ya watoto hapa nchini katika program zake za afya?

Unicef inafanya kazi kubwa kuhakikisha kila mtoto ana afya njema na lishe bora kumwezesha kukua kimwili na kiakili ili aweze kufikia malengo yake yote kimaisha. Hata hivyo program za Unicef za afya na lishe zimejikita katika maeneo makubwa ya huduma bora za afya na lishe kwa mama wajawazito ili kuhakikisha kila mjamzito anahudhuria kliniki angalau mara nane au zaidi na kwenye mahudhurio hayo anapata huduma zote stahiki ikiwamo chanjo ya Tetanus, vidonge vya kuzuia Malaria na huduma za kumkinga mtoto na maambukizi ya VVU iwapo mama ana maambukizi Pia inajikita katika kuboresha huduma za uzazi salama katika vituo vya afya kwa kuwapatia wakunga na wahudumu wa afya mafunzo ya mara kwa mara, ujenzi na upanuzi wa vituo vya afya hasa wadi za wazazi na kutoa vifaa tiba bora na vya kisasa ili kuwezesha utoaji wa huduma bora za uzazi.

Kufanikisha upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba ikiwamo upatikanaji wa chanjo zinazokinga watoto dhidi ya magonjwa mbalimbali yenye kuzuiwa na chanjo mfano Kifua Kikuu, Surua, Polio, Tetanus, Kuharisha, Nimonia na Homa ya Ini Kusaidia kufanikisha upatikanaji wa uhakika wa huduma bora za afya dhidi ya magonjwa yanayoongoza kwa kuua watoto wadogo chini ya miaka mitano kama vile Malaria, Kuharisha na Nimonia.

Pia Unicef imejikita katika huduma za afya uzazi kwa vijanabalehe (adolescent) ili kupunguza mimba za utotoni na maambukizi ya magonjwa ya zinaa ikiwamo VVU kwa kundi hilo.

MTANZANIA: Ni changamoto gani hasa za kiafya zina- zowakabili watoto wa Tanzania walio chini ya miaka mitano na Unicef inaisaidiaje serikali kupambana na changamoto hizo? Nini kinachosababisha changa moto hizo?

DK. LYIMO: Pamoja na jitihada kubwa za serikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha huduma za afya hasa kwa watoto chini ya miaka mitano, bado kuna changamoto nyingi zinazohitaji kutatuliwa.

Kumewekwa uhaba mkubwa wa wahudumu wenye ujuzi wa kutoa huduma za afya hasa waganga na wauguzi katika vituo vya kutolea huduma za afya, hasa vya ngazi za chini kama zahanati na vituo vya afya.

Unicef inashirikiana na serikali na wadau wa maendeleo kutoa mafunzo ya mara kwa mara, usimamizi na mafunzo ya vitendo kazini ili kuboresha uwezo wa wahudumu waliopo kutoa huduma bora za afya.

Kutokana na uhaba wa vituo vya kutolea huduma za afya Unicef kwa kushirikiana na serikali imejenga na kukarabati zahanati na vituo vya afya hasa maeneo magumu kufikika, pia kuvipatia vifaa tiba, ili kuviwezesha kutoa huduma bora za afya ya mama na mtoto.

Kumewapo na bajeti isiyojitosheleza kwa ajili ya huduma za afya ambayo ni chini ya azimio la Abuja la asilimia 15, kiwango kikubwa (asilimia 11) cha maambukizi ya virusi ya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto hakikubaliki, jitihada zaidi zinahitajika kwa wadau wote wa nchini.

MTANZANIA: Malaria ni moja ya ma- gonjwa yanayosababisha vifo vingi vya watoto barani Afrika ni kwa kiasi gani mmeshiriki kusaidia kupunguza tatizo hili hapa Tanzania?

DK. LYIMO: Ingawa kuna mafanikio makubwa katika kudhibiti na kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano vitokanavyo na Malaria, bado idadi ya vifo hivyo ni kubwa na haikubaliki. Katika jitihada hizo, Unicef, Shirika la Afya Auniani (WHO) na wadau wa maendeleo wamefanya kazi na serikali kwa kutoa elimu kwa jamii jinsi ya kujikinga na Malaria na pia kutafuta huduma za afya mapema hasa kwa watoto wanapokuwa na dalili za Malaria.

Pia kununua na kugawa vyandarua vyenye viwatilifu kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga, hasa kwenye kambi za wakimbizi mkoani Kigoma, kutoa mafunzo kwa Wahudumu wa Afya Jamii (WAJA/CHW) kusaidia jamii zao hasa mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kujikinga na Malaria.

MTANZANIA: Kwa muda wote ambao Unicef imekuwapo nchini ni mambo gani makubwa mnayojivunia kama mafanikio katika kuboresha afya za watoto wa Tanzania?

DK. LYIMO: Unicef kwa kufanya kazi na serikali na wadau wengine wa maendeleo, imechangia katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na hivyo kuongeza idadi ya kina mama wajawazito wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Wastani wa kina mama saba kati ya 10 (zaidi ya asilimia 70) wanajifungulia vituoni. Hii imepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya kina mama na watoto wachanga vinavyoto- kana na uzazi.

Unicef imeshiriki kuboresha huduma za kufubaza VVU/HIV kwa mama wajawazito wenye maambukizi (asilimia 93) na hivyo kuzuia maambukizi ya VVU/HIV toka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Utoaji wa dawa za kufubaza VVU kwa watoto kwa asilimia 66 ingawa asilimia ni bado ni ndogo ila imeongezeka kutoka kwenye asilimia 43 ya awali, kuboresha huduma za chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano ambapo sasa wastani wa watoto tisa kati ya 10 (karibu asilimia 90) wamepewa chanjo zote

muhimu kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Chanjo (IVD) na hvyo kuwakinga magonjwa yanayozuiwa na chanjo kama Nimonia, Kuharisha, Homa ya Ini, Tetanus. Pia imeshiriki vema kuboresha huduma za lishe kwa watoto wadogo chini ya miaka mitano na hivyo ku- punguza kwa kiasi kikubwa udumavu.

Katika kuhakikisha ajenda ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Unicef kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine imejikita kuimarisha mifumo ya serikali ili iweze kusaidia katika uboreshaji wa huduma kwa watoto wadogo.

Kwa mfano Unicef imewezesha Serikali kuandaa rasimu ya programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto. Programu hii ni ya miaka mitano na itatekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 2025/2026, lengo ni kuhakikisha watoto wanakuwa vizuri katika nyanja zote za ukuaji.

Pia Unicef imewezesha kikosi kazi cha kitaifa kuweza kukaa, kupanga na kujadili masuala mbalimbali ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto. Hii imewezesha agenda ya malezi makuzi na maendeleo ya mtoto kuanza kupewa kipaumbele.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles